The House of Favourite Newspapers

JPM: “Hakuna Kazi Ngumu Kama Kuongoza Nchi”, Ataja Sababu – Video

Rais Dkt. John Magufuli amesema anapitia changamoto nyingi katika uongozi wake kwani kuongoza nchi ni kazi ngumu na wakati mwingine anashindwa kulala kutokana na kukabiliwa na mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya wananchi wake.
Magufuli ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Novemba 1, 2018 katika Kongamano la Uchumi na Siasa lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuhudhuriwa na wasomi mbalimbali nchini wakiwemo wahadhiri, maprofesa, wanasiasa, wadau wa uchumi, viongozi na wanafunzi.
“Kwa kweli uongozi ni kazi ngumu sikutegemea ingekuwa ngumu hivi. Yaani ukiingia chumbani kwangu mafaili yamejaa hadi kitandani na kila moja lina umuhimu wake, huwezi kulipeleka kwa mtu mwingine, Ndoto ya kuipeleka Tanzania kwenye Uchumi wa Kati najua itafika pamoja na changamoto zake. Fedha nyingi zilikuwa zinatumika kwa safari, chai na semina. Tulipobadilisha, fedha za maendeleo zimefikia asilimia 40. Mpaka sasa tumejenga KM 1,500 (za barabara) na tunajenga Interchange hapo Ubungo na tukikosa fedha tunajenga wenyewe
“Katika miaka 3 viwanda 3,066 vipya vimejengwa, najua tulikuwa na viwanda ambavyo tulishindwa kuviendeleza. Tumeanza kuchukua hatua na najua kuna baadhi ya watu wataguswa. Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi ndani ya Afrika lakini tujiulize tuna viwanda vingapi vya ngozi?Wangapi hapa wamevaa viatu vilivyozalishwa hapa nchini? Tujiulize (nikiwemo na Mimi) kiatu nilichovaa ni cha wapi?
“Tulikuwa tunaongoza kwa kuwa na watumishi hewa na tulikuwa tunalipa mabilioni kwa watumishi hewa takribani 14,000. Kwa mwezi tulikuwa tunatumia zaidi ya Sh. Bilioni 700. Baada ya kuwaondoa watumishi hewa mishahara imerudi kuwa bilioni 237. Mpaka sasa kwenye hazina yetu tuna Dola za Kimarekani Bilioni 5.4! Hatujawahi kuwa na hifadhi fedha za nje kiwango hiki. Tunaweza kununua bidhaa kwa miezi 6 ijayo. Na ukiwa na fedha unakuwa na jeuri,” amesema Magufuli.
Pia, amezungumzia jinsi anavyopenda kuzungumza lugha ya Kiswahili akibainisha kuwa ndio lugha inayowaunganisha Watanzania.

“Nasikia watu wanasema hajui Kiingereza nimekuwa waziri nikasafiri nchi nyingi kwenye vikao huko nilikuwa napewa uongozi wakati mwingine wa mikutano mikubwa sasa nilikuwa nazungumzaje kama sijui, Ukiniambia kusafiri sijui wapi sijafika, nimetembea karibu dunia yote kwa sasa sina haja kwangu ni Utanzania kwanza na kipaumbele changu ni kuwatumikia Watanzania.

Wakati wa Kampeni 2015 niliahidi Elimu Bure na nikajiuliza: “Nitaweza?” lakini nilipoingia nikakuta kuna fedha zimelala lala, nikasema ziende huko. Tunatoa bilioni 21 kila mwezi na tunazipeleka moja kwa moja kwenye shule ili anayekula naye aliwe, Chuo kama cha Kampala ni cha ajabu! Kuna wanafunzi nimeongea nao wamemaliza Masters na sasa wanaenda kuanza shahada ya kwanza – UDOM inaweza kuchukua wanafunzi 43,000 lkn ilikuwa inapewa wanafunzi 15,000 wengine wanapelekwa vyuo ambavyo havina hata madarasa,“ amesema Magufuli.

VIDEO: MAGUFULI AKIFUNGUKA HAPA

Comments are closed.