JPM: Kenyatta ‘Aniombe Radhi’, Hatukukubaliana Watufunge Mabao 3-2- Video

RAIS  John Magufuli, leo Julai 05, amempokea Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye amewasili  nchini kwa ziara binafsi ya siku mbili.

Rais Kenyatta amepokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita ambako Magufuli yupo nyumbani kwao kwa ajili ya mapumziko.

 

Akijibu hotuba fupi ya Rais Kenyatta, Magufuli alisema:

Rais Kenyatta alinipigia simu na kuniambia nakuona ndugu yangu upo Chato, nataka nije nikusalimu na kumsalimu mama yako. Nikasema huyu Kenyatta ananifuatilia nyendo zangu, nikajua kuwa hii ni njia ya kuja kuniomba msamaha baada ya kutufunga mabao 3-2. 

 

Tulikubaliana ilikuwa tufungane goli mbili kwa mbili, sisi tulipofunga tukatulia lakini wao wakaongeza la tatu, nilijua leo ataomba msamaha, ila nimeshakusamehe ndugu yangu Rais Kenyatta.

 

Ukiacha ujirani tulionao Watanzania na Wakenya ni marafiki, sidhani kama kuna mkoa wowote wa Tanzania ambao hakuna Wakenya, na wengine wananyumba kubwa Tanzania, nyumba ndogo Kenya.

 

Biashara kati ya Tanzania na Kenya 2018 ilikuwa ya sh. trilioni moja, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Tsh. bilioni 400, na kuagiza bidhaa za Tsh bilioni 500, kwa mujibu wa TIC, Kenya ni miongoni mwa nchi tano zinazowekeza Tanzania, kuna miradi 504.

 

Nikupongeze Rais Kenyatta na Serikali yako kwa hatua mlizochukua, dhidi ya mtu aliyetoa kauli ya kuwagawa Watanzania na Wakenya, maneno ni sumu kali sana, nakuthibitishia sisi Watanzania tunawapenda sana Wakenya.

 

Ile hatua ya kumleta kijana wako aje kutafuta huku, aje tu tutampokea vizuri, tunajua akija kuwekeza Watanzania watapata ajira. Rais Kenyatta umeweka historia kuwa rais wa kwanza wa nchi ya nje kufika hapa Chato na naomba nikuambie wananchi wa Chato wamefurahi sana. Walikuwa hapa tangu saa moja asubuhi wakikusubiri. Ukiachilia mbali ujirani, Watanzania na Wakenya ni marafiki na ndugu. 

 

Watanzania wengi wanakaa Kenya na Wakenya wengi wanakaa Tanzania, wengine wana nyumba ndogo Kenya na kubwa Tanzania na kinyume chake vivyo hivyo. Tumekuwa na ushirikiano mzuri kama alivyosema Rais Kenyatta tunaongea lugha moja.

 

Nchi zetu zimekuwa zikishirikiana katika maendeleo hasa miundombinu, ambapo barabara zimejengwa na sasa tunakamilisha miundombinu ya umeme. Ujio wako unaashiria kuwa sisi ni marafiki na tunashuruku sana. Na ni azma ya Tanzania kukuza uhusiano wetu.

 

Nikupongeze wewe na Serikali ya Kenya kwa namna mlivyoshughulikia suala la mtu mmoja aliyetaka kutugawa. Na ujumbe ulionitumia kupitia kwa Balozi niliupata na nakusisitizia, sisi tunawapenda sana Wakenya na hapa wapo.

 

Sasa hivi tunatengeneza meli katika Ziwa Victoria. Ikitoka Mwanza hadi Kagera, Kemondo itakuwa haina maana. Tunataka iwe inaenda hadi Kenya na Uganda, wafanyabiashara waitumie na ndiyo maana nchi za Ulaya nyingi zimeungana kwa namna hii.

 

Nchi zenye watu ndiyo zenye maendeleo makubwa. China na India zina watu wengi sana. Sisi Tanzania tupo milioni 55 na kuzaliana sio shida. Watu wakiwa wengi uchumi unakua, bora kuwa na watu wengi wanaofanya kazi. Ndiyo maana nchi za Ulaya zinaungana.

 

Mgeni wetu alipanga kuja na kuondoka lakini sasa amesema analala hapahapa. Nashukuru sana. Nawashukuru wote na sasa acha niende nikamtembeze mgeni wetu huku Chato,” amesema Magufuli.

MSIKIE JPM HAPA

Loading...

Toa comment