The House of Favourite Newspapers

JPM Kuwawajibisha Wasiohamasisha Kujiandikisha

RAIS John Magufuli, amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua viongozi wa mikoa na wilaya ambao watashindwa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kupigia kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

 

ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2019, mkoani Katavi, alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa ndege wa Mpanda, ambako amezindua safari za ndege za ATCL.

 

“Jana Waziri wa TAMISEMI alitoa takwimu kwa mikoa na wilaya ambazo zimefanya vizuri kwenye kuhamasisha watu kujiandikisha, nasubiri zoezi limalizike na kwa viongozi ambao mikoa na wilaya zao zitafanya vibaya najua watanzania hawatanilaumu kwa hatua nitakazochukua kwa viongozi,” amesema.

 

Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Katavi kwenda kujiandikisha ili kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

 

Pia  ameeleza hatua zilizofikiwa mpaka sasa baada ya kutoa msamaha kwa washtakiwa wa uhujumu uchumi kwa sharti la kukiri na kurejesha fedha walizoiba.

 

“Leo nimezungumza na DPP (Mwendesha Mashtaka wa Taifa) , amenieleza kuwa mpaka sasa watu 138, waliokuwa wameiba mabilioni ya fedha, wamejitokeza na kuomba msamaha na wameshalipa fedha hizo na tayari wameachiwa huru.”

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, jana Ijumaa Oktoba 11, 2019,  alimwomba Rais Magufuli, kupokea dokezo lake la mapendekezo ya kuwachukulia hatua viongozi wa mikoa na wilaya ambao watafanya vibaya kwenye uandikishaji wapiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa.

 

Alisema uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo si wa kuridhisha kwa mikoa yote nchini na kwamba kinachokosekana ni uhamasishaji.

 

Kwa mujibu wa Jaffo, mikoa iliyofanya vizuri ni pamoja na Iringa ambao imefikisha asilimia 53 ukifuatiwa na Mbeya, Songwe na Tanga.

Alisema katika tathmini hiyo, Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia nane huku Kilimanjaro ikiwa na asilimia 12 na Arusha asilimia 13.

 

“Naomba uridhie uandikishaji unaisha Ocktoba 14, mwaka huu. Haiwezekani siku ya mpira wa Simba na Yanga watu wote wanaenda uwanjani lakini siku ya uandikishaji watu wanasuasua. Endapo siku saba zitakwisha na kuna mikoa haijafika hata asilimia 50 nitaomba nilete dokezo kwako,” alisema.

 

“Kuna wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, kuna wakurugenzi itakapobainika watu walizembea katika kuhamasisha watu kujiandikisha, nitaomba wachukuliwe hatua,” alisema.

Comments are closed.