JPM, LOWASSA WAUNGANA NA FAMILIA KUAGA MWILI WA MAMA MENGI

Jeneza lenye mwili wa Mwanzilishi Mwenza wa Makampuni ya IPP, Mama Mercy Anna Mengi,  ukiwa katika Kanisa la Azania Front lililopo Posta ya Zamani jijini Dar es Salaam wakati wa ibada kuaga mwili huo leo Alhamisi, Novemba 8, 2018.

 

RAIS John Magufuli na mkewe Mama Janeth leo wameshiriki ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa mke wa Dkt. Reginald Mengi, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Makampuni ya IPP, Mama Mercy Anna Mengi,  katika Kanisa la Azania Front Dar es Salaam.

 

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili huo, Rais Magufuli amesema: “Ushuhuda uliotolewa hapa na waumini mbalimbali, nina hakika Mama Mercy Anna Mengi ni mtu ambaye alimpenda Mungu na alimtegemea Mungu, na nina uhakika Mungu atamsamehe dhambi alizonazo ili aweze kupumzika kwa amani.”

Rais Magufuli na mkewe, Mama Janeth Magufuli wakiwapa pole familia ya Reginald Mengi kwa kuondokewa na mpendwa wao, Mama Mercy Anna Mengi kanisani hapo.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili na Kiluteri Tanzania (KKKT)  Dayosisi na Mashariki na Pwani, Askofu Alex Malasusa, amewataka watu waendelee kumuombea mama huyo ambaye alifariki dunia Oktoba 31 mwaka huu.

 

Akizungumza katika ibada maalum  kanisani hapo, ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, Askofu Malasusa alinukuu neno la Biblia kutoka Paulo 4 mstari 13 hadi 14 na Paulo 5 mstari 1 hadi 2.

Rais Magufuli akitoa heshima za mwisho.

“Jambo kubwa na la maana kwetu sisi ni kuwa na uhakika kwa Mungu kwa kushika mapenzi yake, na hata katika hili tuyakubali mapenzi yake kama inavyosema sala yake, ili tuendelee kuishi kwa mapenzi yake.

 

“Mungu ameweka siri kubwa kwenye suala la kifo, hata sisi wachungaji Mungu ametuficha, ni siri yake yeye mwenyewe Mungu.  Niwaombe ndugu na jamaa tuendelee kujiweka karibu na yeye ili kila mtu afikie tamanio la kwenda mbinguni,” amesema Dkt Malasusa.

 

Mbali na Rais Magufuli, miongoni mwa viongozi wengine walioshiriki ibada hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

 

Mercy alifariki nchini Afrika Kusini ambapo alikuwa akipatiwa matibabu katika Hosptali ya Mediclinic Morningside ya Johannesburg.

 

Ibada hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ilianza majira ya saa sita mchana na kuongozwa na Askofu Malasusa akisaidiwa na Chadiel Luiza.

Watoto wa marehemu Regina na Abdiel Mengi wakiingia kanisani katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu Mama yao.

Mama Mengi atakumbukwa kama mmoja ya waanzilishi wa makampuni ya IPP ambayo inamiliki vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo EATV, EA Radio, ITV, NIPASHE, The Guardian, Radio One, na Capital Radio.

 

Mwili wake utasafirishwa hadi Machame, Moshi, kwa ajili ya maziko Jumamosi Novemba 10, 2018.

JPM , LOWASSA MSIBANI KWA MERCY ANNA MENGI

Toa comment