The House of Favourite Newspapers

Jua Cali mkali wa rap Kenya anayefifia taratibu

0

OLYMPUS DIGITAL CAMERA Paul Julius Nunda, Jua Cali.

JINA lake halisi ni Paul Julius Nunda, lakini mashabiki wa muziki wa kizazi kipya katika Tanzania na Afrika Mashariki wanamtambua zaidi kwa jina lake la kisanii kama Jua Cali, staa mzaliwa wa Kenya aliyeiona dunia kwa mara ya kwanza Septemba 12, 1979.

Wakati ule Bongo Fleva ikiwa juu na kuanza kuonekana kama ndiyo muziki wa vijana kwa eneo lote la Afrika Mashariki na Kati, mmoja kati ya wasanii wa Kenya waliojitokeza na kufanya vizuri katika nyimbo zao zilizokubalika na kupendwa nchini Tanzania ni yeye.

Jua Cali ni mmoja wa waanzilishi wa lebo kubwa na maarufu ya muziki huo huko Kenya inayojulikana kama Calif Records, akiwa pamoja na Clement Rapudo (Clemo) na yeye mwenyewe anachukuliwa kama baba wa staili ya rap ya nchi hiyo inayofahamika kama Genge.

Jina lake la Jua Cali aliliakisi kutoka katika mtaa aliokulia mjini Nairobi, uutwao California na alianza kupenda muziki tangu akiwa na umri wa miaka 12. Kiasili, msanii huyo ni mpole aliyelelewa katika maadili ya dini ya kikristo Dhehebu la Katoliki.

Awali, aliamini atakuwa mchezaji wa timu ya taifa ya mpira wa kikapu, lakini hakuweza kufanikisha ndoto yake na hivyo kujiunga na kundi la muziki la Sita Futi ambalo lilivunjika mapema, ndipo yeye na rafiki yake wa toka utotoni, walipobuni na kuanzisha Calif Records, ambayo baadaye ilikuja kuwa kubwa na maarufu sana.

40c2896c1c9a5ccda1dd81a9e6e3720dWimbo wake wa kwanza kabisa kurekodiwa uliitwa Ruka, uliotolewa mwaka 2001, ukifuatiwa na Nipe Asali, PiliPili (2004), Kamata Dame na baada ya miaka kadhaa, 2006, ndipo alipotoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa Juacali Sekta.

Moja ya nyimbo zake zilizofahamika sana nchini ni ile ya Ngeli ya Genge iliyovuma miaka ya 2008 na 2009 ambayo pia ilibeba jina la albamu, iliyomfanya kupata mialiko mbalimbali katika mataifa mengi ya Afrika, Ulaya na Marekani. Kwa mujibu wa gazeti la Standard la Kenya, mwaka 2007 alikuwa miongoni mwa watu 100 maarufu nchini humo.

Licha ya muziki, Jua Cali pia ni mfanyabiashara na anachukuliwa kama msanii wa kwanza kupata dili la fedha nyingi Kenya, pale mwaka 2007 alipoingia mkataba na kampuni ya simu ya Motorola ili kutangaza simu zake za muundo wa W, uliomuingizia kiasi cha shilingi milioni moja za Kenya.

Baada ya umaarufu wake kuwa juu sana sawa na wasanii wenzake wa nchi hiyo jirani, taratibu makali yake yakaanza kupungua, kwani kazi nyingi alizotoa, ama zilikosa moto wake wa awali, au zilishindwa kupenya katika lundo la kazi za vijana wa Kibongo zinazosumbua kwa sasa.

Hata hivyo, Jua Cali anabakia kuwa mmoja kati ya wasanii kutoka nje ya Bongo, ambao kazi zao zilipata kupendwa sana na hivyo kutoa mchango wake katika maendeleo ya muziki wa kizazi kipya tunaojivunia nao hivi sasa.

Leave A Reply