Jumba La Kifahari Zaidi La Shilingi Bilioni 312 Lateketea Kwa Moto Marekani! – Video
Hebu vuta picha, unaacha jumba la kifahari, unarudi unakuta kifusi cha majivu meusi, kufumba na kufumbua jumba lako la kifahari mfano wake hakuna duniani, limetekeketea kabisa na kubaki kama kifusi cha takataka kule dampo!
Moto mkubwa unaoendelea kuteketeza maeneo ya Los Angeles umesababisha uharibifu wa kihistoria, ukiteketeza moja ya majengo ya kifahari zaidi duniani, lililokuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 125, zaidi ya shilingi za kibongo bilioni 312, katika eneo la majengo ya kifahari la Pacific Palisades, nchini Marekani.
Picha za kipekee zilizopatikana na DailyMail.com zinaonyesha mabaki ya jengo hilo, ambalo lilikuwa na vyumba 18 vya kulala, likiwa limebaki kuwa kifusi kikubwa cha majivu na bustani zilizokuwa za kifahari sasa zikiwa hazitamaniki kwa kufunikwa na moshi mzito.
Jengo hilo, linalomilikiwa na bosi wa kampuni ya Luminar Technologies, Austin Russell, bilionea mtoto mwenye umri wa miaka 29 tu, lilijulikana kwa muonekano wake wa kisasa na lilikuwa sehemu ya kuandaa tamthilia maarufu ya Succession, iliyokuwa inarushwa na televisheni ya HBO ya Marekani katika msimu wake wa nne mwaka 2023.
Nyumba hiyo ya kifahari, ambayo pia ilikuwa ikipangishwa kwa dola laki nne na nusu kwa mwezi, sawa na shilingi bilioni moja na milioni 125, sasa imeporomoka kabisa kutokana na moto wa Palisades ambao bado haujazimwa kikamilifu, ukiwa tayari umeteketeza asilimia 92 ya jiji hilo.
Uharibifu wa Kihistoria
Moto huo umeharibu zaidi ya majengo 10,000 na kusababisha vifo vya watu 11 mpaka sasa. Mbali na nyumba hii ya kifahari, alama nyingine za kihistoria, kama vile Topanga Ranch Motel, ambazo zilikuwa sehemu muhimu ya historia ya Los Angeles, pia zimeteketea.
Nyumba ya kifahari ya Russell, ambayo ilinunuliwa mwaka 2021 kwa dola milioni 83, ilikuwa moja ya alama kubwa zaidi za kifahari, ikiwa na vyumba 18 vya kulala, ukumbi wa sinema wa viti 20, na bustani ya kifahari yenye bwawa kubwa.
Hata hivyo, bwawa hilo sasa limebaki kuwa shimo lililojaa maji meusi, huku sakafu ya mbao na vifaa vingine vya kifahari vikiwa vimeporomoka. Scanner ya retina iliyokuwa nje ya chumba cha kulala cha mmiliki, vyumba viwili vya dharura (panic rooms), spa ya kifahari, na jumba la magari lenye teknolojia ya kisasa vote viliteketezwa kabisa.
Hasira na Maswali magumu kwa Mamlaka
Uharibifu huu umeibua maswali mengi kwa maafisa wa Los Angeles, hasa kwa nini hifadhi muhimu ya maji iliyokuwa ikihudumia eneo la Pacific Palisades ilikuwa tupu wakati moto huo ulipotokea. Hii imeleta changamoto kubwa katika juhudi za kuzima moto huo na kuzuia uharibifu zaidi.
Austin Russell, mmiliki wa jumba hilo, alifichua utajiri wake alipokuwa na umri wa miaka 25 baada ya kampuni yake, Luminar Technologies, kuingia kwenye soko la hisa mwaka 2020. Alianzisha kampuni hiyo akiwa na umri wa miaka 17 tu, akiacha masomo yako katika chuo kikuu cha Stanford baada ya kusoma kwa miezi mitatu tu na kuamua kujikita katika biashara yake.
Sasa akiwa mmoja wa matajiri wachanga zaidi duniani, Russell amekumbana na pigo kubwa katika maisha yake kutokana na hasara hii ya kihistoria.
Moto wa Palisades, ambao ripoti zinasema unaelekea yaliko majumba mengine mengi zaidi ya kifahari, unaendelea kuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa Los Angeles, na juhudi za kuzima moto huo zikikumbana na changamoto za kimfumo na hali mbaya ya hewa.