Jux Kunogesha Shindano la Miss Kilimanjaro

 

WAKATI warembo 15 kutoka mkoani Kilimanjaro wakitarajiwa kupanda jukwaani Ijumaa hii pale Kili Home mjini Moshi kuwania taji la Miss Kilimanjaro 2019, msanii wa Bongo Fleva, Juma Jux,  ndiye amethibitishwa kutumbuiza katika shindano hilo.

 

Shindano hilo ni la kuwasaka warembo wanne ambao wataenda kuuwakilisha Mkoa wa Kilimanjaro katika ngazi ya Kanda ya Kaskazini baadaye mwezi huu jijini Arusha kusaka tiketi ya kushindana kwenye mashindano ya Miss Tanzania.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Dees Bridal Entertainment ambayo ndiyo wandaaji wa shindano hilo, Dotto Olafsen,  amesema maandalizi mpaka sasa yamekamilika huku akiweka wazi kuwa mwaka huu wamejipanga kufanya mashindano yaliyo bora kuliko misimu yote kwani warembo wameonyesha uwezo wa hali ya juu.

Amesema msanii wa nyimbo za Bongo Fleva, Juma Jux,  ndiye atatumbuiza kwenye shindano hilo ambalo litaanza saa tatu za usiku siku ya Ijumaa na kuongeza kuwa kiingilio ni shilingi 10,000 kawaida, VIP ni Sh 30,000, VVIP Sh 40,000 huku meza ya watu kumi ikiwa ni shilingi 200,000.

 

Amesema katika hatua ya awali walijitokeza zaidi ya warembo 22 kushiriki mashindano hayo kabla ya mchujo kufanyika na kupatikana warembo 15 ambapo walitumia kigezo cha umri, mvuto, uwezo wa kujitambua na kujieleza na mengine mengi,  lengo ikiwa ni kuwapata wale ambao watauwakilisha vyema Mkoa wa Kilimanjaro na kuiletea heshima.

 

Dotto amesema warembo hao wamekaa kambini kwa zaidi ya mwezi mmoja wakiwa wanafundishwa stadi za maisha na walimu wa fani mbalimbali yakiwemo mafunzo ya elimu ya mabadiliko ya mwili, mzunguko wa hedhi, usafi wakati wa hedhi (hedhi salama) pamoja na utengenezaji wa pedi za kike kwa njia rahisi ili washiriki hao ambao ni sehemu ya uwakilishi wa wasichana nchini waweze kuwa mabalozi wazuri juu ya hedhi salama.

 

Amesema wao wanataka kuitumia vyema tasnia ya urembo kutoa mabalozi wazuri wa kusaidia harakati mbalimbali hapa nchini katika sekta ya afya, mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU, utunzaji wa mazingira na shuguli mbalimbali za kijamii.

 

Ameongeza kuwa warembo walipata fursa mbalimbali ya kutembelea vituo vya watoto yatima, ofisi za serikali na taasisi ikiwemo ofisi ya Mkurugenzi na Meya wa na Manispaa ya Moshi,  na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Kilimanjaro (KIA).

Kwa upande wa zawadi,  alisema zimeboreshwa mwaka huu tofauti na msimu uliyopita,  hivyo siku ya mashindano yatawekwa wazi.

Habari na Kennedy Lucas, Kilimanjaro

Loading...

Toa comment