The House of Favourite Newspapers

JWTZ Wazungumzia Vifo vya Wanajeshi 14

Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania limesema kikundi chake cha ulinzi na usalama kilichopo DRC kwaajili ya kutekeleza jukumu la ulinzi na amani kilivamiwa na Waasi waliojilikana kuwa ni ADF na kusababisha mauaji kwa wanajeshi 14.

 

Amesema kwamba tukio hilo lilitokea katika eneo la kambi iliyopo daraja kwenye mto Simulike barabara ya kutokea Oicha kwenda Kamango mpakani mwa nchi ya Uganda Kaskazini Mashariki ya wilaya ya Beni Jimbo la Kivu Kaskazini.

 

Akithibitisha mauaji hayo muwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania (CDF) Luteni Jenerali James Mwakibolwa amesema shambulio hilo lakuvamiwa lilizusha mapigano baina ya kikundi hicho na kile cha waasi na yalidumu kwa takribani masaa kumi na tatu (13) na kusababisha vifo vya askari wa Tanzania 14 na wengine 44 kujeruhiwa na askari wawili bado hawajulikani walipo ambapo jitihada zaidi za kuwatafuta zinaendelea.

 

Amesema shambulizi la tarehe 7 kuamkia tarehe 8 Desemba lilikua baya zaidi kuwahi kuitokea tangu vikosi hivyo vianze kushiriki ulinzi wa amani nchini DRC mwaka 2011 kwakua limeleta madhara makubwa, hata hivyo kikundi hicho ambacho bado kipo huko kinauwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu husika kwa uhodari wa hali ya juu ,ushupavu, weledi mkubwa na umahiri stahiki.

 

Kwa niaba ya mkuu wa majeshi Luteni Jenerali Mwakibolwa amewathibitishia watanzania kuwa tukio hilo halitawavunja moyo na kamwe Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania halitatetereka kupeperusha bendera yake ndani na nje ya nchi kwani tukio hilo limewaongezea nguvu, ari ,ushupavu na uhodari zaidi katika kutekeleza majukumu yake.

 

Aidha amesema nchi pia iko salama na itaendelea kuwa salama na yeyote ambaye anataka kuwajaribu atashughulikiwa ipasavyo kwani historia ya jeshi inadhihirisha uwezo thabiti.

 

Kuhusu taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini zinafanyika chini ya utaratibu wa Serikali na umoja wa mataifa na JWTZ na serikali wanaendelea kuchukua hatua stahiki kufuatia tukio hilo ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika sambamba na kuangalia taratibu za kuwajulisha familia za wafiwa zimekamilika na ndio maana hawakuweza kutoa taarifa hizo bila kuwaweka sawa familia za mashujaa hao.

 

Kwa umoja wa watanzania amewataka kuwaombea dua roho za mashujaa hao zipumzike mahali pema peponi kwa amani na majeruhi wote wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ulinzi wa taifa na dunia nzima.

Comments are closed.