The House of Favourite Newspapers

JWTZ Yazindua Mashindano ya Sanaa na Utamaduni ya Jenerali Jacob Mkunda

0

Dar es Salaam 10 Agosti 2024: Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) leo limezindua mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda yanayotarajiwa kuanza kufanyika Agosti 19 mpaka 30 mwaka huu Msasani Beach Club jijini Dar ambayo yatahusisha muziki wa dansi na ngoma za asili kutoka vikosi vya majeshi ya ulinzi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhalizi ya mashindano hayo, amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60, ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Meja Jenerali Mkeremy aliendelea kusema; “Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda aliona ni vyema kuyarudisha baadhi ya mambo ya sanaa na utamaduni yaliyoonekana kupotea, hivyo ameona ni vyema kuyarudisha mambo hayo ikiwemo ngoma za asili kwa staili ya mashindano.

“Mashindano haya yatakuwa endelevu na matarajio yetu ni kufanyika kila mwaka lakini kwa mwaka huu 2024, tutanza na bendi kumi za muziki wa dansi na vikundi tisa vya ngoma za asili ambavyo vitashindanishwa ambapo vyote hivi vinamilikiwa na Jeshi la Wananchi.

Ingawa kwa mwaka huu vinashindanishwa vikundi hivyo tu hapo baadae katika kuyaboresha mashindano hayo tunatarajia kuvishirikisha na vikundi vya kiraia na wasanii binafsi kulingana na sanaa waliyonayo.

“Vikundi hivi vyote vilishapewa taarifa miezi sita iliyopita hivyo vitakuwa vimejipanga kisawasawa kwenye mashindano hayo ambapo kila mwaka kutakuwa na kauli mbiu yake lakini kauli mbiu ya mwaka huu ni Miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Na katika kuhakikisha tunawapata washindi bila utata tutawatumia wanatasnia wazoefu wa masuala ya sanaa ya muziki na utamaduni akiwemo Mzee John Kitime ambao watatusaidia katika hilo.

Pia katika mashindano hayo tutashirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa nchini (Basata) na zawadi ambazo zitatolewa kwa washindi ni pamoja na nyimbo zao kurekodiwa kwa video na audio na nyimbo hizo zitapewa nafasi ya kutumbuiza kwenye kilele miaka 60 ya JWTZ hapo Septemba 1 mwaka huu.

Katika kilele cha maadhimisho hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.” Amesema Meja Jenerali Mkeremy.

Katika uzinduzi wa mashindano hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo Mhe. Dk. Damas Ndumbaro na kufungwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mh. Dk. Stergomena Lawrence Tax (Mb) ambapo hakuna kiingilio kwenye mashindano hayo na wananchi wote wanakaribishwa kwenda kujionea burudani kutoka vikundi hivyo. Alimaliza kusema Meja Jenerali Mkeremy.

Leave A Reply