K-LYIN SIRI NZITO KIFO CHA MENGI

 

HAKUNA mtu mwingine wa kumuuliza siri ya kifo cha mfanyabiashara maarufu nchini, bilionea Dk. Reginald Abraham Mengi (75) zaidi ya Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lyin.’ 

 

K-Lyin ambaye ni mke wa marehemu Dk. Mengi ndiye amekuwa karibu na mfanyabiashara huyo kipenzi cha watu hadi kifo chake.

 

MAMBO ANAYOJUA K-LYIN

Inaelezwa kuwa, Dk. Mengi amefia Dubai nchi za Falme za Kiarabu, haijulikani huko alikweda kwa sababu gani? Lakini K-Lyin ambaye sasa anatumia jina la Jack Mengi anaelewa. Nini kilitokea hadi mzee huyo kipenzi cha watu akapoteza maisha, alisema neno gani la mwisho kwake, alikuwa na tatizo gani la kiafya katika siku za hivi karibuni na pengine wosia wake kwa familia ni upi, mambo yote haya K-Lyin ana nafasi kubwa ya kuyajua kuliko mtu mwingine yeyote.

UKARIBU WA K-LYIN NA MENGI

Tangu Novemba 1, mwaka jana, Dk. Mengi alipofiwa na mke wake aitwaye Mercy-Anna Mengi amekuwa karibu zaidi na mke wake huyo mdogo (K-Lyin) ambaye amewahi kumuelezea kuwa alikuwa ni mtu muhimu katika maisha yake.

 

“Kama nisigekuwa naye (K-Lyin) huenda ningelikuwa nimekufa,” alisema Dk. Mengi wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari kutoka nchini Kenya kilichofanya naye mazugumzo mwishoni mwa mwaka jana. Kutokana na ukweli huo, K-Lyin ndiye ambaye anaweza kujua kilichokuwa kinamsumbua mfanyabiashara huyo ambaye kwa siku za hivi karibuni afya yake ilionekana kudhoofu.

 

Dk. Mengi amewahi kuandika katika akaunti yake ya Mtandao wa Kijamii wa Twitter hivi karibuni kuwa anaumwa na kwamba aliomba aombewe. Hata hivyo, hakueleza bayana kilichokuwa kinaitatiza afya yake hadi pale ilipokuja taarifa ya kushtua kuwa amefariki dunia akiwa Dubai.

MAISHA YA  K-LYIN NA MENGI

Mwaka 2010, Dk. Mengi na K-Lyin ambaye siku za hivi karibuni alipenda aitwe Jack Mengi walianza uhusiano wa kimapenzi uliojaa siri kubwa.

 

Hata hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda uhusiano wao ulikuwa wa uwazi hadi kufikia kupata watoto wawili mapacha na baadaye kufunga ndoa. Hakuna shaka, maisha ya mapenzi kati yao yalizidi kuchipuka kiasi cha kila mmoja kuona fahari kuposti picha na video wakiwa pamoja kwenye mitandao ya kijamii kuonesha namna walivyokuwa na ukaribu. Ukaribu huu unaondoa shaka kwamba K-Lyin anajua mengi yaliyofichika kuhusu maisha ya Dk. Mengi na kifo chake kwa jumla.

 

K-LYIN APEWA POLE KILA KONA

Kufuatia kifo cha mumewe, watu kutoka kila kona ndani na nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakimpa pole mwanadada huyo ambaye kabla ya kuolewa na Dk. Mengi alikuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya. “Pole dada, Mungu akushike mkono na kukuimarisha katika kipindi hiki kigumu,” aliandika mmoja wa wachangiaji katika ukurasa wa Instagram wa K-Lyin.

NINI KIMEMUUA MENGI?

Hata hivyo, pamoja na kumiminika kwa pole hizo watu wengi walitaka kujua kilichosababisha kifo cha mfanyabiashara huyo, lakini hadi tunakwenda mitamboni hakuna chanzo cha kuaminika ndani ya familia kilichoeleza sababu za kifo hicho.

 

Msemaji wa marehemu Dk. Mengi, Abdulrahaman Njovu alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu undani wa kifo cha Dk. Mengi alisema hafahamu kwa kuwa alikuwa hajapata taarifa na kuahidi kuzitoa zikipatikana. Habari za chini ya kapeti ambazo hazikuthibitishwa kitabibu zinaeleza kwamba, Dk. Mengi alipatwa na ugonjwa wa shambulio la moyo ‘heart attack.’ Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni taratibu za mazishi ya Dk. Mengi zilikuwa zinaendelea.


Loading...

Toa comment