visa

Kaa Chonjo! Mastaa Hawa, Ukizubaa Unapigwa Mamilioni

DAR ES SALAAM: Mjini shule! Ni msemo maarufu unaosherehesha elimu ya maisha ambayo watu huweza kuipata katika miji mbalimbali duniani, kwani kuna mengi ya kujifunza zaidi ya yale unayoweza kuyapata darasani.

Gazeti la Risasi Jumamosi lina ripoti nzito juu ya namna utapeli unavyofanyika ukiwahusisha watu mbalimbali maarufu nchini.

 

TUJIUNGE NA SINGIDA

Wakati Risasi Jumamosi likiwa na listi ya mastaa kadhaa ambao wamewahi kuripoti au kuripotiwa majina yao kutumika katika utapeli, mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Naomi kutoka mjini Singida alipiga simu katika chumba chetu cha habari na kulalamika kutapeliwa.

 

Katika maelezo yake, Naomi ambaye mwanzo alikuwa na uhakika kuwa ametapeliwa na staa wa filamu Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ alisema aliahidiwa na msanii huyo kusaidiwa kutimiza ndoto yake na kwamba alimtaka atume fedha ya kiingilio kwenye kundi lake.

“Mimi Dude huwa namuona sana kwenye filamu na hasa hivi karibuni kwenye Bongo Dar es Salaam, navutiwa sana na kazi zake na nilitaka kujiunga naye. Kwa muda mrefu nilikuwa natafuta mawasiliano na wasanii.

 

“Sasa nikaona kwenye Facebook ametangaza anahitaji wasanii kwa ajili ya kushiriki kwenye tamthilia yake mpya. Nikamfuata inbox, tukachati kwa kirefu, akaniambia kuna kiingilio cha kulipa. Alisema ni laki moja (100,000), akasema nikilipa hizo fedha atanitumia fomu kwa njia ya email, halafu atanipa utaratibu wa kwenda Dar kambini.

 

“Mimi nikamtumia hizo hela, tena kuna rafiki yangu Mwaju naye ni msanii mwenzangu huku Singida, nilipompa huo mchongo, akaupenda. Naye yeye akaongea na shangazi yake, akampa hizo fedha, akatuma. Baada ya hapo, simu haikupokelewa tena,” alisema Naomi na kuongeza;

“Nikaona bora niwapigie simu ninyi waandishi wa habari, mnaweza kutusaidia hili jambo. Maana sielewi inakuwaje msanii mkubwa hivyo kuwa tapeli.”

 

DUDE KIKAANGONI

Gazeti hili lilimvutia waya Dude na kumweleza yote kuhusiana na madai ya Naomi, kwanza alikiri kusikia malalamiko ya watu wengi kutapeliwa kwa jina lake, lakini akasema siyo yeye anayefanya huo utapeli.

 

“Nimesikia malalamiko hayo sana, lakini sihusiki kabisa. Kuna mtu anatumia jina langu Facebook, anakusanya pesa kwa watu mikoa mbalimbali akijifanya anatafuta wasanii. Jamani mimi sitafuti wasanii, hata kama nikitafuta huwa hakuna pesa yoyote mtu anayotakiwa kulipa,” alisema Dude.

Dude akaongeza; “Watu wanatumia vibaya majina yetu wasanii kutapeli. Mimi nimefurahi sana ulivyonipigia, ninyi waandishi wa habari mtusaidie jamani katika hili, tunachafuliwa sana.”

 

DC JOKATE MWEGELO

Staa mkubwa wa filamu na urembo nchini, Jokate Mwegelo anaingia kwenye listi hii akihusishwa na utapeli isivyo sahihi.

Jokate aliye Miss Tanzania namba 2 mwaka 2006, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, aliwahi kulalamika kuhusu kuwepo kwa watu wanaotumia vibaya jina lake kutapeli mitandaoni.

“Hili jambo limenichosha, kuna watu wanajaribu kufanya utapeli kwa kutumia jina langu, wanajifanya eti ninatoa mikopo, hapana, hakuna kitu kama hicho. Hata hivyo, ninawashauri wananchi na mashabiki wangu wote nchini kuwa makini na jambo linalohusiana na pesa mitandaoni na kunihusisha mimi.

 

DC Jokate ambaye tayari ana mafanikio makubwa katika wilaya yake katika muda mfupi tangu ateuliwe, alisisitiza; “Mimi sina akaunti yoyote ya vikoba na sijihusishi na jambo hilo, kwa vyovyote waliofungua akaunti hiyo kwa jina langu ni matapeli, wana nia ya kuwaibia wananchi. Sifanyi hivyo vitu kabisa…kama nina jambo basi lazima nitaliendesha kiofisi, siyo mitandaoni. Kitu ninachoweza kufanya mitandaoni ni kutoa taarifa tu,” alisema Jokate Mwegelo akizungumza na gazeti hili.

 

Mpaka sasa, pamoja na mambo mengine DC Jokate ameweza kuonesha mwanga wa kusaidia elimu katika wilaya yake huku akiendesha kampeni yake ya elimu aliyoipa jina la Operesheni Tokomeza Ziro Kisarawe iliyolenga zaidi kuwasaidia watoto wa kike walio masomoni.

 

Naye Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Kisarawe, Mtela Mwampamba ambaye yupo chini ya Jokate, alikiri kuwepo kwa matapeli wanaotumia jina la DC Jokate.

“Juzi tu ofisini tulimpokea mgeni binti mmoja kutoka Tabora, anasema amekuja kumuona Jokate baada ya kuwasiliana naye na kumtumia pesa za viboka. Ni kero kwa kweli,” alisema DAS Mwampamba.

 

IRENE UWOYA

Staa daraja la kwanza kwenye filamu za Kibongo, Irene Uwoya naye ameingia kwenye kadhia hiyo, lakini kwake wajanja walikwenda mbali zaidi hadi kuingia kwenye shughuli zake za ujasiriamali.

Wakati akiwa kwenye hatua za mwisho za kufungua baa yake ya Last Minute iliyopo Sinza-Mori, Dar, kulitokea utapeli kwa watoto wa mjini kujifanya wanahusika na utoaji kazi kwenye baa hiyo.

 

“Wakati usahili ukiendelea ndani ulioendeshwa na Uwoya na Johari (Blandina Chagula), kuna watu walikuwa wakichukua 50,000 kwa wasichana waliokuwa wakitafuta kazi, wakiwaahidi kuwasaidia,” kilieleza chanzo chetu.

Katika mazungumzo na Risasi Mchanganyiko, Uwoya alikiri kusikia uwepo wa jambo hilo na kutoa tahadhari kwa watu waliokuwa wakisaka ajira.

 

UKIZUBAA UNAPIGWA

Risasi Jumamosi limebaini kuwa, gia kubwa inayotumika na matapeli wengi ni kufungua akaunti zenye majina ya wasanii wakubwa na viongozi wa kiserikali kisha kujifanya wanatoa mikopo.

Wanachofanya matapeli hao ni kuweka vigezo rahisi na kutaka fedha kidogo kama kianzio au dhamana ya mkopo, wakitoa ahadi ya kutoa mkopo wa fedha nyingi.

 

Mastaa ambao matapeli wengi huwatumia kufanya utapeli wao ni wale ambao wana majina makubwa kwenye fani zao.

Baadhi ya mastaa waliongia kwenye makabrasha ya Risasi Jumamosi, mbali na Dude, Uwoya na Jokate ni Kajala Masanja, Aunt Ezekiel, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Jacqueline Wolper na Wema Sepetu (Bongo Muvi).

Wengine ni Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, Faustina Charles ‘Nandy’, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, Hamisa Mobeto na Rajab Abdul ‘Harmonize’ (Bongo Fleva).

 

KUTOKA KWA MHARIRI

Watu wenye nia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wapo wengi sana siku hizi, ambao hutumia majina ya mastaa wakubwa kufanya utapeli.

Ni vizuri kuwa makini na mawasiliano yoyote unayofanya kwa njia ya simu au mitandaoni na mtu anayejiita staa kwani huenda utakuwa umeingia mikononi mwa matapeli.

Epuka kufanya muamala wowote wa fedha baada ya kufanya makubaliano na mtu uliyejuana naye kupitia mtandao.

 

Mwisho, lazima kuwa makini na mtu ambaye anaonyesha nia ya kukupatia mkopo wa fedha nyingi kwa dhamana ya fedha kidogo, kwani kwa kawaida hakuna mkopo wa fedha nyingi kwa dhamana ya fedha kidogo, tena kupitia mtandaoni tu.
Toa comment