The House of Favourite Newspapers

KAA CHONJO STAILI MPYA YA WANAWAKE KUWALIZA WANAUME YAIBUKA

 UKIAMBIWA kaa chonjo usifikiri kuna jambo la heri linakuja, ni hatari tupu! Onyo hili liwafikie wanaume wote kutokana na kuibuka kwa staili mpya ya wanawake ‘kuwaliza’ kwa kuwafanyia kitu mbaya.  

 

Vyanzo vya habari na uchunguzi wa Uwazi wa hivi karibuni umebaini kuwa jijini Dar es Salaam na maeneo mengi ya mijini kumekuwepo na matukio mengi ya wanaume kuingizwa katika mchezo mchafu wa kufumaniwa na wanawake wanaodaiwa ni wake za watu kisha kupigwa mamilioni ya fedha.

 

Tukio bichi la hivi karibuni ni kunaswa laivu kwa tukio la mtu mwenye asili ya Kiasia ‘Mdosi’ (jina halikupatikana) ambaye alijikuta matatani baada ya kudaiwa kumsarandia mke wa mtu.

 

Paparazi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia chanzo chake alitonywa majira ya saa 4:00 usiku kuwa eneo la Mikocheni, Kinondoni jijini Dar kulikuwa na vurugu ya Mdosi kudaiwa kufumaniwa na hivyo kutakiwa awahi kufika eneo la tukio. Kama kawaida, paparazi wetu alijisogeza eneo la tukio na kukuta sakata hilo likiendelea kwa Polisi walioitwa kutuliza ghasia wakichukua maelezo kutoka kwa walalamikaji na mtuhumiwa.

 

“Nani amekuruhusu kupiga picha?” Polisi mmoja anayedaiwa kuwa ni wa Kituo cha Mwenge, Dar alimhoji na kumkataza paparazi wetu kuendelea kupiga picha na kufanya zoezi la kuchukua tukio kuwa na ushahidi wa picha chache zilizopigwa harakaharaka katika hatua za mwanzo.

 

MAELEZO YA MTU ALIYEDAI KUIBIWA MKE

“Afande huyu jamaa anatembea na mke wangu, muulize humu ndani kwangu amekuja kufanya nini?” Alisema mwanaume huyo huku akikatizwa na maneno aliyotamka Mdosi, “NO, NO, NOOO,” akimaanisha hapana.

 

“Amekuwa akiwasiliana na mke wangu muda mrefu, leo kama bahati nilikuwa nimeaga nasafiri, lakini safari imekufa ghafla narudi nyumbani nakuta hali siielewi. “Braza, braza…” Mwanaume huyo alionesha hasira kwa Mdosi ambaye alikuwa ameketi kwenye sofa akiendelea kutikisa kichwa kuashiria maelezo yanayotolewa hayakuwa na ukweli.

MDOSI AFUNGUKA YAKE

Mara baada ya kutolewa kwa maelezo marefu yaliyomtuhumu mdosi kuiba mke wa mtu, Polisi walilazimika kumuuliza mtuhumiwa shida iliyompeleka nyumbani kwa mwanamke huyo usiku ilikuwa ni nini?

 

Akizungumza kwa Kiswahili kilichonyooka kuonesha kuwa ni mwenyeji wa Bongo hii, Mdosi huyo alisema; “Sikiliza kaka, hawa watu wamenifanyia mchezo, huyu mwanamke amekuwa akinisumbua kuwa anataka kazi. “Tumekuwa tukiwasiliana mara nyingi, leo alinipigia simu na kuniambia kuwa nije kwake ameniandalia chakula cha jioni.

 

“Kwa kuwa nimemchukulia kuwa kama rafiki, nikasema ngoja nije, nafika hapa nakaa kidogo huyu mwanamke anaingia chumbani akiwa amevaa kanga moja, ghafla naona watu wanaingia wanasema wamenifumania,” aliwaambia Polisi huku yule mwanaume na jamaa zake aliowaita kushuhudia tukio hilo nao wakipinga maelezo yake kwa ukali na vitisho.

 

WATAKIWA KWENDA POLISI

Baada ya kutokea kwa utata wa maelezo, Polisi walimwamuru mtuhumiwa na walalamikaji kwenda Kituo cha Polisi cha Mwenge kwa ajili ya kuweka sawa mambo.

Jambo la kushangaza walalamikaji hawakutaka kwenda kituoni na kulazimisha walipwe fedha ili mambo yaishe kwa kuwa ugoni hautambuliki kisheria. “Unaona afande, wanakataa kwenda kituoni, sasa wao si wamewaita ninyi, lakini mimi nami nafahamiana na askari wangu nawaita waje, naona nataka kuibiwa fedha,” alisema Mdosi huku akinyanyuka kutoka kwenye sofa na kutaka kutoka nje.

 

Haiwezekani, inawezekana zilipokuwa nyingi, safari ya kwenda Polisi iliafikiwa na pande mbili, lakini walalamikaji walionesha kuwa walikuwa na wasiwasi na kwamba hawakutaka suala lao lifike Polisi na hata mwandishi wetu alipowauliza majina, hakuna aliyekuwa tayari kutaja jina. Hata baada ya kufika kituo cha Polisi mwanaume aliyekuwa akidai kumfuma mkewe alisikika akisema: “Sasa wewe si unajifanya mjanja, baki na mke wangu mimi nakuachia.”

 

Mwanaume huyo pamoja na wenzake walijaribu kutaka kuondoa na kuzuiliwa na Polisi ambao walimwamuru paparazi wetu kuondoka eneo la kituo kwa kuwa alikuwa hahusiki na tukio hilo. “Wewe unafanya nini hapa kituoni? Naomba uondoke kama ni suala la habari utalifuatilia kesho kwa kamanda wa mkoa, unauliza majina, utayapata kwa kamanda,” askari mmoja alisema.

 

HII NDIYO STAILI MPYA YA KUWALIZA WANAUME

Siku za hivi karibuni uchunguzi na matukio mengi ya wanaume kudaiwa kufumaniwa yameibuka, lakini ukweli ni kwamba mengi kati ya hayo yanatengenezwa ili kuwafanya wanaume watoe fedha. “Wanawake hawa hatari wana kundi lao ambalo linahusisha wanaume, wanachofanya wanatuma meseji kwa mwanaume wanayemfahamu au kukosea namba.

 

“Ukiwajibu na wakabaini wewe ni mwanaume wanaanzisha urafiki na wewe wanajilegeza, sasa ukiwa dhaifu unaweza kudhani umepata mwanamke. “Mwanzo atakuambia hana mume na kwamba anasoma, anaweza kukurushi na picha utakazopenda, sasa siku mkipanga kukutana hotelini au nyumbani, ukiingia tu kabla hujafanya chochote unavamiwa na watu na wanasema wamekufumania.

“Hapo wanakupiga picha na kukuambia kuwa wanakwenda kuzisambaza mtandaoni, mwisho wanakuambia utoe fedha mmalizane,” alisema kijana mmoja ambaye ni miongoni mwa wanaume waliowahi kulizwa shilingi milioni mbili na kundi hilo la wanawake hatari.

KAA CHONJO

Kutokana na uwepo wa taarifa za matukio mengi ya wanaume kudaiwa kufumaniwa, Uwazi linawatahadharisha wanaume kuwa makini na mtindo wa kutongozatongoza wanawake wasiowafahamu kwani siku moja watajikuta wamenasa katika mtego hatari. Mbinu wanazotumia kwa mujibu wa uchunguzi wetu ni kujitongozesha kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na hiyo ya kujifanya wamekosea kupiga namba za simu.

 

MATUKIO MENGI YAFICHWA

Kutokana na aina ya matukio wanaume wengi ambao ‘wamepigwa’ pesa wamekuwa wakishindwa kwenda kutoa taarifa katika vituo vya Polisi kwa kuhofia kuwa habari zao zitajulikana.

 

“Kaka kama hasara nimeshapata, lakini kwenda Polisi siwezi kwa sababu nakwenda kujishtaki mwenyewe ndugu yangu, mimi nina mke na watoto,” alisema kijana mwingine ambaye alifika hivi karibuni kuomba msaada katika chumba chetu cha habari namna anavyoweza kufikisha ujumbe wake kwenye jamii bila kufahamika. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Musa Athumani Taibu hakupatikana mara moja ili aelezee jinsi ya kuthibiti uhalifu huu mpya ulioingia jijini.

Comments are closed.