Wanaokula nyama za watu waliona bora miili wale wao kuliko kuoza na kuliwa na funza!
ELVAN STAMBULI NA MTANDAO | UWAZI | SIMULIZI
Naendelea kusimulia simulizi ya kweli kuhusu makabila ya Papua New Guinea yanayokula nyama za watu; endelea.
MAKABILA yanayojulikana kula nyama ya watu ni Wakorowai na Wafore ambao huishi katika milima au miinuko.
Wafore walikuwa hawajulikani duniani hadi mwaka 1950 baada ya watafiti kuwafanyia utafiti huku watafiti hao wakiwa kwenye hatari ya kuuawa na kuliwa miili yao.
Wakati wa utafiti huo, waligundua kuwa watu hao walikuwa wakila wenzao waliokuwa wakifariki, hivyo kujikuta wakikumbwa na maradhi yaliyoitwa ugonjwa wa kifo cha kucheka yaani laughing death.
Ugonjwa huo uliua wanawake na watoto wengi kutokana na kula nyama za watu.
Walikuwa wanakula miili ya wenzao waliokufa, badala ya kuwazika, wakawafanya kitoweo kwa madai kwamba walikuwa wakiwaokoa wapendwa wao hao ili wasiliwe na funza pindi watakapooza.
Nyama ya miili ya watu walikuwa wakiita ‘nyama ya nguruwe mrefu’ yaani Long pig.
Wafore walisema ni bora miili hiyo ikaliwa na wao na ikae kwenye matumbo yao badala kuliwa na funza kwa madai kwamba roho zao zitazidi kuishi kwenye matumbo hasa ya wanawake.
Kwa imani hiyo, wanawake walikuwa wakipewa ubongo waupike na kuula kisha nyama kutengenezwa ‘rosti’, hivyo kula na watoto wao.
Hata hivyo, ulaji huo wa miili ya wenzao pamoja na ubongo ulifanya wapate maradhi ambayo waliyaita kwa kabila la kwao kuru na uliua watu wengi wa jamii hiyo. Mtu aliyekuwa akipata ugonjwa huo alikuwa anapoteza nguvu na kushindwa kutembea kisha mwili kukonda.
Mtafiti aliyeitwa Dk. Jekly alisema kilichokuwa kikisababisha maradhi hayo siyo bakteria au virusi isipokuwa protini iliyokuwa kwenye ubongo wa maiti ambayo ikiliwa ilikuwa inaharibu ubongo kwani ilikuwa inasababisha kucheza au kutikisika na kuharibika, jambo ambalo kitaalamu huitwa brain’s cerebellium.
Ugonjwa huo uliwaandama watu hao wala miili ya watu hadi mwaka 2009 ambapo mtu mmoja aliripotiwa kufariki dunia kwa maradhi hayo.
Lakini tukio baya lilitokea Julai, 2012 ambapo watu 29 wa makabila hayo waliwala watalii kwa kupika miili yao huku wanaume wakitengeneza supu, sehemu ‘nyeti’ na ubongo.
Kitendo hicho kilisababisha serikali kuingilia kati na kwa mujibu wa Gazeti la The Nationa Newspaper la huko, Kamanda wa Polisi Madang, Anthony Wagambie alithibitisha hayo.
“Huwa hawafikirii kwamba wanafanya kitu kibaya, wanakiri hayo waliyoyafanya waziwazi,” alisema kamanda huyo kwa njia ya simu.
Alisema wauaji wanaamini kuwa waliowaua walikuwa wachawi ambao kwa kabila lao huitwa Sanguma na kwamba walikuwa wakiwapa kilevi wenyeji huku wakifanya nao mapenzi wanavijiji maskini kwa njia ya kishirikina.
Kwa kula viungo vya binadamu waganga wao walikuwa wanawaambia kuwa watapata nguvu ya ajabu na kwamba hata wakipigwa risasi, hazitaingia kwenye miili yao.
Kamanda Wagambie alisema waligundua kulikuwa na kundi la watu kati ya 700 na 1,000 wa vijijini Kaskazini Mashariki ambao walikuwa wana imani hiyo.
Alisema walikamata watu 28, wake kwa waume na aliwapandisha mahakamani kujibu tuhuma za mauaji ya binadamu wenzao. Wakipatikana na kosa watahukumiwa adhabu ya kifo.
Akasema watuhumiwa wote waliwaweka rumande na kuendelea kuwatafuta wengine waliokula nyama za watu.
Anasema watu hao walifanya ukatili mkubwa kwa kuwaua watalii saba na anaamini kwamba walikula miili yao.
Itaendelea wiki ijayo, usikose mwendelezo wake.
Comments are closed.