The House of Favourite Newspapers

Kabila Linalohusudu Vitambi Linalotembea Utupu

0

BAADA ya wiki zaidi ya 20 kukuletea kabila la wala watu lililopo Papua New Guinea, leo tutaanza kukuleta kabila dogo nchini Ethiopia katika Bara la Afrika ambalo ni la ajabu kutokana na vitendo vyao visivyo vya kawaida katika jamii yetu.

Naamini utafuatilia habari za kabila hilo kuanzia leo hadi nitakapofika tamati ambapo utakuwa umeelewa mila na desturi za baadhi ya makabila yaliyopo barani Afrika.

Kabila hilo kama nilivyosema hapo juu, linaitwa Bodi ama hapa kwetu tungewaita Wabodi lakini pia huitwa Wame’en, jamaa hawa huishi katika Bonde la Omo Kusini mwa Ethiopia na baadhi ya wanaume hutembea uchi wa nyama; wanapofika sehemu zilizostaarabika hushangaza wengi.

Kwenye bonde hilo hawapo peke yao kwani kuna makabila mengine mengi madogomadogo arobaini na tano lakini kwa mila na tabia wanafanana na Wabodi japokuwa hao wengine hawana tabia ya kipekee ya Wabodi ya kujinenepesha kwa sababu maalum kama tutakavyoona mbele.

Arbore ni moja ya kabila linaloishi katika Bonde la Omo na linalofanana kwa baadhi ya tabia na Wabodi kwani hawa nao huishi katika bonde hilo na ni majirani na makabila mengine mengi kama tutakavyoona.

Waarbore nao kama walivyo wenzao, ni wakulima wafugaji ambao hufuga ng’ombe na mbuzi.

Tofauti yao na Wabodi ni kwamba hawa hupendelea kucheza ngoma na kuimba nyimbo za kienyeji wakiamini kwamba kwa kufanya hivyo, wanatukuza mila na desturi zao, hivyo imani yao ni kwamba kitendo hicho huwaongezea utajiri wao ambao ni kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe na mbuzi wanaowafuga.

Wanawake wa kabila la Waarbore ni tofauti na Wabodi kwani hawa hufunika vichwa vyao kwa kutumia nguo nyeusi na huvaa shanga za rangi tofauti shingoni pia kwenye masikio yao huweka hereni maalum kwa ajili ya kujiremba wakati wanawake wa Wabodi wao hunyoa vipara au ‘viduku’.

Licha ya kuwa wafugaji Wabodi ni wakulima na mazao yao huyalima katika miteremko ya udongo uliotokana na milipuko ya volcano.

Lakini Wabodi mara nyingi wengi wao wake kwa waume na watoto, hawapendelei kufuga nywele na badala yake hupendelea kunyoa kwa mitindo mbalimbali ambayo vijana wa leo hapa nchini wamekuwa wakinyoa, ‘kiduku’.

Unyoaji huo hufanywa hata kwa watoto wadogo wanaobebwa mgongoni na hauchagui jinsia.

Watoto wao wengi hunyolewa viduku na hata wasichana hunyoa mitindo hiyo na bila shaka mtindo huo ulienea hadi Ulaya ambapo sasa tunaona jinsi hata wachezaji wa mpira wa miguu wakubwa huko wanavyouiga.

Kutokana na utamaduni huo kuenea duniani ni wazi kwamba bila shaka waanzilishi wa mtindo huo ni Wabodi kwa sababu wao wamekuwa wakinyoa hivyo enzi kwa enzi.

Wengi wa wenyeji hawa wana miili midogo na siyo wanene, hivyo basi wale wanaume wenye umbo kubwa na vitambi hupendwa na wanawake wa huko kuliko wanaume wembamba.

Lakini ili kupata umbo kubwa na vitambi kuna kazi kubwa hufanyika kwani kuna mbinu ambayo hutumika na ni ya gharama kubwa kwa wanaohitaji kuwa na kitambi kikubwa.

Kuna wakati vijana hushindanishwa ili kuwa na umbo kubwa na vitambi vikubwa vilivyochongoka kwa mbele.

Zamani mshindi alikuwa anapewa zawadi ya ng’ombe au mbuzi lakini siku hizi zawadi zimeongezwa kwani mshindi hupewa pia kombe ambalo ni tuzo kwa kushinda kutokana na kujinenepesha na kuwa na kitambi kikubwa kuliko washindani wenzake.

Mara nyingi vijana wa kiume ndiyo hushirikishwa kwenye kuwania ubingwa wa kitambi na wahusika huweza kushinda baada ya kukaa kambini kwa miezi wakila vyakula ambavyo siyo vya kawaida lakini hawana budi kufanya hivyo ili kuwa wanene.

Je, wanafanya nini hadi kuwa wanene kupindukia? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

(STORI:ELVAN STAMBULI | UWAZI JUNI 20)

Leave A Reply