The House of Favourite Newspapers

Kabila Linalohusudu Vitambi, Linalotembea Utupu-4

0
Washindi wa shindano la vitambi.

 

MAISHA ya watu wa Kabila la Wabodi waishio Ethiopia katika Bonde la Mto Omo wanategemea ufugaji.

Japokuwa huwa wanakula chakula kitokanacho na mahindi na mtama, hawa watu huwa hawalimi.

Chakula hicho hukinunua kwenye masoko mbalimbali na wao kujikita zaidi katika ufugaji wa ng’ombe, mbuzi pamoja na kondoo.

Kwa kawaida kabila hili ambalo hawana dini, yaani wapagani, wana tabia ya kuhamahama ili kutafuta sehemu nzuri kwa uchungaji wa mifugo yao. Wanaume wanaokwenda kuchunga hutumia kati ya wiki tatu au nne wakiwa mbali na familia zao.

 

Wakichukua damu mbichi ya ng’ombe ili wanywe.

 

Watu hawa wanakadiriwa kufikia 9,000, wanapenda sana kunywa uji wa mtama au mahindi na damu ambayo huchanganywa, huku kwetu Wachaga huiita kisusio au mlasu, kwani huchanganywa na supu au maziwa.

Pamoja na kuwa ni wafugaji, Wabodi hawali nyama hovyo hovyo, hula wakati maalum kama vile kuna sikukuu au shughuli maalum.

Kwa kawaida kabila hili huwa halichinji ng’ombe au mbuzi kwa kisu badala yake humponda kichwa kwa kutumia jiwe kubwa au nyundo.

“Wazee wetu waligundua kwamba kumchinja ng’ombe au mbuzi ni kupoteza damu bure, hivyo wakaamua kumpiga nyundo ili damu iweze kukingwa kirahisi anapokuwa amekufa,” alisema mwenyeji mmoja wa kabila hilo aliyekutwa akimgema damu ng’ombe wake.

 

Washiriki wa shindano la vitambi

 

WANAWAKE

Wanawake wa Kibodi ni tofauti sana na wanawake wa makabila mengine, kidogo wanafanana na wale wa Kabila la Mursi. Wanavaa ngozi ya mbuzi na kwenye masikio yao huweka mapambo ya vipande vya miti lakini kwenye midomo yao, mdomo wa chini huutoboa na kupachika kipande cha mti uliochongwa kimaridadi au kipande cha chuma baada ya kutobolewa kisha kupona na matundu hayo kutumika.

NDOA

Wanawake wa Kibodi huolewa kwa kutolewa mahari ambayo wenyewe huita ‘dauri’, ambapo mwanaume hulazimika kulipa ng’ombe kati ya 10 hadi 36, kutegemea koo za mwanamke. Ng’ombe hao hutolewa na baba wa mwanaume kwa ajili ya kumuoza mwanaye wa kiume.

Wanawake kabila la Wabodi.

 

Wanaopokea mahari huwa ni wajomba wa mwanamke ambao ndiyo wana uwezo wa kuruhusu binti kuolewa kuliko upande wa baba wa binti na aliyeolewa yeye hupewa ng’ombe watatu majike wanaonyonyesha na kuwa mali yake.

Mgawanyo wa ng’ombe kama ni 36, wajomba hupewa ng’ombe watano, baba hupewa ng’ombe wawili na babu hupewa ng’ombe mmoja.

Wakati wa sherehe za kimila, ng’ombe huuawa na wazee maalum humtumbua mnyama huyo na kufanya utabiri wa mwaka kupitia utumbo wa ng’ombe husika.

Ng’ombe anayechaguliwa kwa shughuli hiyo huwa yule mwenye afya njema kwa kumuangalia, yaani mnene. Utabiri huo hupewa kiongozi wao ambaye wenyewe humtaja kwa jina la Komoro. Akishepewa utabiri huo wa mwaka, huwatangazia watu wake na Kabila la Bodi huamini kwamba baada ya utabiri huo huwa ndiyo mwanzo wa mwaka wao wa kimila yaani kati ya Juni na Julai kila mwaka.

Baada ya utabiri wazee wa kimila hupewa damu yake na kuinywa baada ya kuchanganywa na uji wa mtama au mahindi.

Wakimaliza kazi hiyo, ndipo ngoma maalum huchezwa huku wanaume waliokuwa wakijinenepesha wakiwa watupu nao hushiriki kucheza ngoma hiyo inayoitwa Ka’el ambayo ni maalum kwa ajili ya mtu mnene.

Hii maana yake ndiyo siku ya kuchaguliwa mwanaume mnene kuliko wote. Ni wale ambao walikaa ndani kwa miezi sita wakitumia damu ya ng’ombe na maziwa pamoja na uji wa mtama.

Mfalme wao, yaani Komoro akifariki dunia hufanywa mambo ya ajabu. Fuatilia wiki ijayo ili uyafahamu.

 

NA MWANDISHI WETU NA MITANDAO | UWAZI

Leave A Reply