The House of Favourite Newspapers

Kabila Linalohusudu Vitambi, Linalotembea Utupu-5

0
Kabila la Bodi.

TUNAENDELEA kuwaletea Kabila la Bodi ambalo wanaume hutembea uchi wa nyama na kujinenepesha ili wawe na kitambi kisha kushindana, endelea:

Wanaume wengi wa kabila hilo huwa na maumbo makubwa kutokana na jinsi wanavyokula. Hata hivyo, tabia yao ya ajabu ni kwamba wengine huvaa shanga kiunoni.

Wanaume wa kabila hilo huchunga ng’ombe na mbuzi huku wanawake wakibaki majumbani wakitunza familia. Hata ujenzi wa nyumba zao dhaifu za miti na nyasi hujengwa na wanawake tena kwa kushirikiana.

 

Hata shughuli ya kukamua maziwa ya ng’ombe au mbuzi hufanywa na wanawake na kuna wengine huchukua maziwa hayo na kwenda kuuza mijini ambapo huko hurudi na mahindi au mtama ambao hutwangwa na kusagwa kwa kutumia jiwe ili kuwa unga badala ya kusaga kwa mashine kama wafanyavyo wananchi wa hapa nyumbani na kwingineko duniani.

Wakati wa kusaga mtama au mahindi kazi hiyo hufanywa kwa ushirika. Wanawake katika koo hujikusanya na kusaga huku kila mmoja akiwa na jiwe lake la kusagia.

 

Wanawake pia hufanya kazi ya kupigapiga ngozi ya mbuzi na kuipaka dawa maalum ili kuifanya kuwa laini na hutumika kama nguo za kujihifadhi au kubebea watoto wao migongoni.

Wanawake pia hujihusisha na kazi za kunyoa watoto na huwanyoa kwa mitindo maalum ambayo mingine ni kiduku kwa kutumia visu vikali, unyoaji huo huaminika kuwa baadhi ya mataifa wameuiga wakiwemo wasanii na wachezaji wa mpira wa kimataifa maarufu duniani.

 

Tofauti na wachungaji wa wanyama wa huku kwetu Tanzania ambao hutumia fimbo, wanaume wengi wa Kabila la Wabodi huwa na silaha za moto, yaani bunduki wakati wakiwa machungani.

Bunduki hizo mara nyingine huwa ni tozo za wakati wa ndoa, mwanaume anayeoa anaweza kupewa sharti la kuleta bunduki moja na akafanya hivyo lakini malipo ya ng’ombe kati ya 20 na 30 hufanywa na kwa wale ambao familia zao hazina mifugo mingi huruhusiwa kulipa kidogokidogo kama yafanyavyo mabenki huku kwetu wakopaji wanaporuhusiwa kulipa kidogokidogo fedha walizokopeshwa.

 

Wasichana ambao ni mabikira huvalishwa shanga maalum za kuwatambulisha na huheshimiwa sana katika jamii au koo zao.

Lakini kwa kawaida ya kabila hilo kila mmoja ambaye ana uwezo wa kutumia bunduki hujitahidi kuwa na silaha hiyo wakiamini kwamba wanakuwa salama zaidi wanapokuwa porini na mifugo yao kwani zinawasaidia kupambana na adui wakiwemo wanyama wakali kama simba au chui ambao watajaribu kuvamia wanyama wao.

 

Mara nyingi wanaume wanapokuwa porini wakijisikia njaa wakiwa mbali na kwao, wanachokifanya ni kumtoboa ng’ombe na kumtoa damu kisha huinywa kwa kuchanganya na asali ikiwa mbichi!

Wanaume hawa wa Kibodi hurina asali na wanapokuwa wakichunga wanyama wao, huwa na vyombo kwa ajili ya kunywea damu au kutumika wakati wa kurina asali hiyo.

NA MWANDISHI WETU NA MITANDAO

Itaendelea.

 

Leave A Reply