The House of Favourite Newspapers

KABLA HATA YA MWAKA MMOJA MADARAKANI… JOKATE SI YULE

UKIAMBIWA mambo aliyoyafanya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Urban Mwegelo tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo, miezi minane iliyopita, utashangaa na kuona si yule unayemfikiria.

AMEFANYAJE?

Mkuu huyo wa wilaya (DC) amefanya mambo mengi makubwa ambayo waliomtangulia kuongoza wilaya hiyo walishindwa kuyafanya. Akizungumza na Gazeti la Ijumaa katika mahojiano maalum alipotembelea ofisi za gazeti hili, Sinza-Mori jijini Dar, mapema wiki hii, DC Jokate alisema kwa kushirikiana na wenzake wilayani humo ameweza kufanya mengi kwa manufaa ya wananchi.

ELIMU

Alisema kuwa japokuwa kipaumbele chake ni elimu, lakini kuna mengi amegundua yapo wilayani kwake na ameanza kuchukua hatua ili kuwanufaisha wananchi.

TOKOMEZA ZIRO

Akizungumzia elimu, DC Jokate alisema tayari ameanzisha Kampeni ya Tokomeza Ziro ambayo inalenga kuwafanya wanafunzi wilayani humo kuongeza ufaulu ambapo wamepania kufanya michango ili waweze kujenga shule ya sekondari ya wasichana wilayani humo.

MIMBA ZA UTOTONI

Alisema kuwa, changamoto kubwa iliyopo wilayani kwake ni mimba za utotoni kwa wanafunzi, jambo ambalo limechangiwa na baadhi ya wazazi ambao hushirikiana na watu wanaowapa mimba wanafunzi na kushindwa kutoa ushahidi wa kuweza kuwatia hatiani wahalifu kwa madai kwamba akifungwa, mtoto wao atakosa matunzo.

Alisema kuwa, nia ya kuanzisha Kampeni ya Tokomeza Ziro, kampeni ambayo itazinduliwa katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, Machi 30, mwaka huu na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassani, inawahusu Watanzania wote kwani akisomeshwa mtoto wa Kisarawe ni sawa na amesomeshwa Mtanzania mwingine yeyote. “Niwaombe Watanzania kujitokeza siku hiyo ya Machi 30, mwaka huu pale Mlimani City kuchangia elimu wilayani Kisarawe kwa sababu kumsomesha mtoto wa Kisarawe ni sawa na kumsomesha Mtanzania mwingine yeyote,” alisema Jokate.

AGUNDUA MADINI

Kuhusu fursa, DC Jokate alisema wilayani kwake amegundua kuwa kuna madini ya kaolin na chokaa ambayo yanaweza kutoa ajira kwa wakazi wa wilaya yake. “Tayari nimeshazungumza na kamishna wa madini kuhusu suala hilo la madini hayo na ameweza kutoa ushirikiano mkubwa, naamini hili nitafanikiwa,” alisema mwanadada huyo.

KILIMO YUMO

Alisema fursa nyingine ambayo ipo wilayani kwake ni kilimo cha korosho na tayari amefanya mipango ya kuhakikisha kunakuwa na kiwanda kikubwa cha kubangua korosho.

“Kiwanda hicho kitakuwa kikubwa na kitaweza kubangua korosho tani 200,000 ambazo ni nyingi, hiyo itaongeza ajira kwa wananchi wangu wa Kisarawe,” alisema DC Jokate. Aliongeza kuwa, tayari kuna wananchi wana mikorosho na atafanya kila linalowezekana kuhakikisha zao hilo linaongeza wilayani kwake na amewakaribisha wananchi kuwekeza katika nyanja hiyo.

ALINDA MISITU

DC Jokate alisema kuwa, licha ya fursa hizo, wilayani kwake kuna hifadhi ya misitu minne muhimu kwa taifa ambayo Serikali ya wilayani kwake inaisimamia. Alisema miongoni mwa vipaumbele alivyotangaza ni kuifanya wilaya hiyo kuwa ya kitalii, jambo hilo linawezekana kutokana na rasilimali za vivutio zilizoizunguka na ili kufikia lengo lake, alisema atahakikisha analinda vyanzo vyote vya asili ikiwamo misitu ambayo imeachwa iharibiwe kwa muda mrefu.

Alikumbusha kuwa rasilimali hizo zinatumika vibaya huku zikiwa na umuhimu mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi na ikiwa na umuhimu wa kipekee katika kumkinga mwanadamu dhidi ya athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira. Katika kuonesha dhamira yake ya kuifanya Wilaya ya Kisarawe kuwa eneo linalovutia kitalii, DC Jokate aliongoza operesheni iliyokwenda sambamba na ukaguzi wa misitu na kuondoa wavamizi waliokuwa na makundi ya mifugo.

Mkuu huyo wa wilaya alifananisha rasilimali ya misitu iliyopo katika eneo lake sawa na mapafu ambayo yanategemewa kulinda uhai wa mikoa mingine jirani kama Dar na kutaka kila kiongozi atekeleze wajibu wake ili kufikia azma hiyo. “Wakazi wa Dar ili mpate mvua na mvute hewa nzuri, lazima mtutegemee sisi wa Kisarawe tunaolinda misitu minne wilayani kwetu ikiwemo ya Kazimzumbwi na Ruvu Kusini ,” alisema Jokate.

Dhamira ya DC Jokate imetangazwa katika kipindi ambacho taifa linaimarisha mikakati mbalimbali itakayowezesha kujitegemea huku Serikali ikiboresha miundombinu inayovutia shughuli za utalii katika maeneo mbalimbali. Takriban kila kijiji nchini kuna vivutio vya utalii ambavyo kutokana na kukosa usimamizi vimetelekezwa na hivyo kutokuwa na mchango wowote katika kuinua maisha ya wananchi na kuchangia pato la taifa.

Badala ya kutegemea mgao kutoka kwa wawekezaji wa shughuli za utalii, halmashauri za wilaya zinatakiwa kuboresha vivutio vyao na kuviendekeza ili viwe vyanzo vya mapato vinavyoaminika kama inavyodhamiriwa na mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.

Baadhi ya wadau wa utalii nchini wanasema dhamira ya DC Jokate ya kutaka kulifanya eneo lake kuwa na mvuto wa kiutalii inatakiwa kuungwa mkono na kila wilaya kwa kuwa inajenga msingi wa vyanzo vya mapato na kuchochea ukuaji wa ajira.

MICHEZO

Kuhusu michezo, DC Jokate alisema ana mpango wa kuwajengea wananchi wa Kisarawe kiwanja kwa ajili ya mpira wa kikapu mara hali ya fedha itakapokuwa nzuri.

ALIPOTOKA

Kabla ya kuingia katika siasa na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate aliwahi kushiriki mashindano ya urembo ya Miss Tanzania 2006 na kushika nafasi ya pili, alijiingiza katika ujasiriamali ambapo alifungua kampuni yake ya Kidoti Loving ambayo inadili na bidhaa mbalimbali za urembo ikiwemo nywele. Jokate ana shahada ya sanaa katika Sayansi ya Siasa na Falsafa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na ameingia kwenye siasa kupitia chama tawala (CCM) akiwa mmoja wa vijana wa UV-CCM.

Baadaye alipata fursa ya kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM). Jokate pia alikuwa miongoni mwa wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Pamoja na kuchukua fomu Jokate hakufanikiwa kupata fursa hiyo. Mwaka 2018 haukuanza vizuri sana katika shughuli zake za kisiasa kwani aliondolewa katika wadhfa wa kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM). Na hii ni baada ya kuwapo kwa mzozo juu ya wadhifa huo tangu alipopata fursa hiyo.

Stori: ELVAN STAMBULI, IJUMAA

Comments are closed.