Kabla ya Kuingia Kwenye Ndoa, Tumbueni Kwanza Majipu

wedding2
VITABU vya dini vinatuambia, mke mwema anatoka kwa Mungu. Vinatufundisha kwamba, akili, nguvu na maarifa yetu si kitu. Ili uweze kumpata mwenza sahihi wa maisha unatakiwa kumuomba yeye ili akupe mtu ambaye mtaishi katika shida na raha.
Ni kosa kubwa sana kukosea kupata mwenza sahihi wa maisha. Ukiingia kwenye ndoa na mtu ambaye hana tabia njema ni hatari.

Atakuwa anakurudisha nyuma kila siku badala ya kusonga mbele. Inakupasa kujiridhisha sana ili kuweza kufanya uamuzi sahihi.
Hilo ndilo somo la leo ambalo nataka tulijadili siku ya leo. Kizazi cha sasa, watu wengi wamejikuta kwenye majaribu makubwa mara baada ya kuingia kwenye ndoa. Wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawajashughulikia masuala ya msingi.
Hayo masuala ya msingi ndiyo nayafananisha na majipu kama msemo wa sasa mjini. Mwanaume anaingia kwenye ndoa kwa sababu tu mwanamke aliyenaye ni mrembo. Ana mvuto, ana muonekano ambao akikatizanaye mbele ya marafiki zake, watachanganyikiwa kwamba ana ‘kifaa.’
Uzuri wa sura unamchanganya kiasi ambacho haoni sababu ya kumjua vizuri tabia mwenza wake. Kumbe mwenzake anakuwa ameficha makucha kwa wakati huo. Wanapoyaanza rasmi maisha ya ndoa, mwanamke anakunjua makucha.
Anaanza kuonesha tabia ambazo si njema. Mwanaume anachukizwa na hizo tabia. Nyumba inageuka uwanja wa mapambano. Kila siku ugomvi. Mwisho wa siku wanaamua kuachana. Kila mmoja anaishi kivyake, hiyo ndiyo inakuwa suluhu pekee kwao.
574813_380291178711125_603982457_nVivyo hivyo kwa wanawake. Mwanamke naye anaingia kwenye ndoa kwa sababu tu; mwanaume ni tajiri au ana muonekano mzuri. Anataka kuolewa na mtu mwenye fedha zake ili aweke heshima kwa marafiki zake. Awe anatembelea gari na kuishi katika nyumba nzuri bila kutoka jasho.
Matokeo yake mwanaume huyo anaonesha tabia ambazo si njema. Fedha zake zinageuka kuwa fimbo ya kumchapia. Anajiamulia anachotaka. Mtaani anakuwa balaa kwa wanawake. Kila anayemuona anataka awe wake.
Anafanya hivyo sababu ana mvuto. Anafanya hivyo kwa sababu ndiyo tabia yake. Anafanya hivyo kwa sababu ana jeuri ya fedha. Nyumbani panakuwa hapakaliki. Kila siku ugomvi. Mwanamke anaamua kuondoka, ndoa inapoteza uhai.
Marafiki zangu, kinachotakiwa kabla ya kufikia kwenye ndoa ni kushughulikia matatizo. Kwanza unapaswa kumjua huyo mwenzi uliye naye ni sahihi. Utamjuaje kama ni sahihi? Mchunguze kwa muda mrefu huku ukishughulikia tabia (tumbua majipu).
Wakati unamchunguza ukiwa unaishi naye, anza kutumbua majipu ambayo yatakusaidia kumjua vizuri mwenzako. Kama unaona kuna kitu hakipo sawa, hakuna haja ya kupindisha maneno, mueleze ukweli. Muambie kwamba tabia fulani si njema.
Akiirekebisha hiyo, mtumbue nyingine. Hicho ndiyo kipimo chako. Umjue mwenzako ni muaminifu? Ni mstamilivu? Mpime anaweza kuishi katika shida na raha? Mpe mitihani ya ugumu wa maisha uone anaichukuliaje.
Usisite kumueleza udhaifu wake katika kipindi ambacho mpo katika urafiki. Mueleze kadiri uwezavyo maana itasaidia kumjenga. Atambue kwamba wapi anakosea na kama ni muungwana, atajirekebisha na kutorudia tena tatizo hilo.
Itafika wakati mtakuwa mmeshashughulikia matatizo mengi. Kama mmoja atashindwa kubadilika, maana yake mtaachana mapema kabla hamjafikia safari. Mkivuka huko kote ina maana mtakuwa mnaelewana. Mnaweza kuishi pamoja.
Kitu cha msingi kabisa, wakati mkitumbua majipu hayo, mumtangulize Mungu mbele. Mumuombe awasaidie katika kila hatua mnayopiga na muweze kufikia hatua ambayo mnataka kuifikia, ndoa.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!


Loading...

Toa comment