The House of Favourite Newspapers

KAFULILA: NILIVYOKUTANA NA MZIMU WA ESCROW

David Kafulila,

KUANZIA leo tutakuwa tunakuletea mfululizo wa tukio baya la kifisadi la Tegeta Escrow, litasimuliwa na mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila, mwanzilishi wa ufichuaji wa sakata hili, ungana naye:

 

Ilikuwa usiku mwingi, nimemaliza kusali natafuta usingizi, napitia baadhi ya SMS ambazo sikuweza kuzijibu siku nzima, nakutana na ujumbe wa mzee Adam Muhoza Mwami ambaye pamoja na uzee wake lakini amekuwa rafiki yangu kwa muda mrefu na siku zote aliguswa sana na namna nilivyosimama katika vita dhidi ya ufisadi!

 

“Nilikwambia mwanangu! Ukweli unaishi, sijali umepoteza mangapi kwa kusimamia ukweli ule lakini kikubwa leo Mungu amekufuta machozi, amekuvika nguo!

“Serikali ileile iliyokushughulikia kila kona na kwa namna zote kwa sababu ya kupigania maslahi ya nchi, leo imekuinua na kukiri hapa nyumbani kwenu Nguruka kwamba ulikuwa sahihi, na wote waliokupinga, kukuhujumu na hata kukuita majina ya wanyama (tumbili) kwa dharau na jeuri ya mamlaka ya kifisadi, leo Mhe Rais (John) Magufuli amesema hapa ‘matumbili’ ni wao wenyewe waliotumia mamlaka kutafuna hazina ya nchi na kuacha umasikini ukiumiza na kuangamiza wananchi wasio na hatia, wasiostahili mateso hata vifo,” ulisomeka ujumbe huo wa mzee Adam Muhoza Mwami!

 

Naam, Sakata la ufisadi wa takriban dola milioni 200 zilizokwapuliwa kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow litabaki kwenye kumbukumbu ya maisha yangu na kizazi changu kwa muda mrefu! Niliona picha halisi ya kinachoitwa “kupita kwenye uvuli wa bonde la mauti”!

Kila ninaposoma habari zinazoendelea kuhusu ama sakata lenyewe au wahusika, nasononeka sana na kubaki najiuliza ni lini habari za Tegeta Escrow zitafutika kama yalivyopata kuibuka baadhi ya mambo, yakatikisa mijadala na kisha kufutika kwenye vichwa vya habari! Ni lini?

 

Leo kuna kesi mahakamani kuhusu niliowataja wahusika vinara katika ufisadi huu; Harbinder Singh Sethi na James Lugemalira lakini mwisho wake ni lini? Kwa namna gani bado tuiachie mahakama!

Bado kuna kesi ya Rufaa ya Tanesco dhidi ya Standard Chartered Bank ya Hong Khong (SCB-HK) kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Kiuwekezaji (International Centre for Setllement of Investment Disputes- ICSID), haijulikani itakwisha lini na kwa namna gani!

 

Ndio maana kila nikiwaza mapana na marefu ya mnyororo wa ufisadi huu ambao asili yake ni mkataba wa kifisadi wa kuzalisha na kuuza umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya Independent Power Tanzania Limited ( IPTL), nawaza nchi hii kulikoni ikapita kwenye mfululizo wa matukio ya kifisadi kwenye mkataba mmoja kwa zaidi ya miaka 20 (kutoka mwaka 1995 mpaka 2015) bila kutokea kiongozi aliyeweza kusema basi! Imetosha!

 

Nafsi yangu inakiri sasa walau kuanzia mwaka 2017, Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli amethubutu na ameweza kuanza kukabili ufisadi huu ulioishi kama zimwi lisilokufa kwa kuhakikisha vinara wa ufisadi huu wanaweza kutiwa nguvuni bila dhamana kwa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha!

 

Muda ambao mkataba huu wa IPTL uliozaa ufisadi wa Escrow uliishi bila kuchukuliwa hatua madhubuti ni simulizi ya kusisimua na kuumiza! Ni ushahidi kwamba nchi hii ilipita kipindi kirefu ambacho dola ilikuwa na mafungamano makubwa na mafisadi kwa kiwango cha juu kabisa kiasi kwamba ilikuwa ngumu kwa dola kukabili ufisadi kikamilifu!

 

Ndio msingi wa kuamua kusimulia kuhusu jambo hili na yote yaliyotokana sanjari na namna misingi ya dola na vyombo vyake vilivyotikiswa na kutikisika kama sio kuyumba na hata kuanguka! Uhai wa mzimu huu wa ufisadi wa IPTL na baadaye Escrow ni mfano mmoja kuthibitisha kwamba misingi ya dola yetu ya Tanzania ama haikuwepo au ilikuwa imekwisha vunjika kitambo!

 

Kama nilivyosema kwamba ufisadi wa Escrow ni sehemu tu ya mkataba wa kifisadi wa miaka 20, uliosainiwa kati ya Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya IPTL mwaka 1995.

Mkataba huu ulikuja kama hatua ya serikali kukabili tatizo la upungufu wa umeme uliotokana na ukame mkubwa miaka ya 1994, na kwa sababu kama nchi tulitegemea umeme wa maji, ukame ulisababisha Serikali kutafuta mbadala wa umeme wa maji.

 

Ndio sababu ya Serikali mwaka 1994 kutuma ujumbe mahususi kwa kazi hiyo nchini Malaysia kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu katika sekta binafsi kuzalisha na kuuza umeme!

Zaidi nchi hiyo ilikuwa sehemu ya ushirikiano wa kihistoria wa South South Cooperation, ambapo Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwenye ushawishi mkubwa! (Mwl. Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa South South Commission).

Ni matokeo ya safari hiyo, ikapatikana Kampuni ya Merchmar kutoka Malaysia iliyoonesha utayari wa kutekeleza jukumu la kuzalisha umeme. Hata hivyo, kutokana na mazingira ya kisheria wakati huo, ikawa lazima kampuni hiyo itekeleze jukumu hilo kwa kushirikiana na kampuni ya mzawa.

Hapo ndipo James Rugemalira alivyoingia picha katika mnyororo huu wa mkataba wa IPTL na hatimaye ufisadi wa Escrow!

 

Rugemalira ambaye awali alipata kuwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alitumia kampuni yake ya VIP Engineering and Marketing kuingia ubia na kampuni hiyo ya Malaysia ya Merchmar na kuunda kampuni ya kufua na kuuza umeme ya IPTL.

Hivyo Kampuni ya IPTL ilisajiliwa mwaka 1995 Tanzania kama kampuni yenye hisa10 kupitia Mamlaka ya Usajili wa Makampuni (BRELA), ambapo kampuni ya Rugemalira ilikuwa na hisa tatu au asilimia 30 ya hisa na Kampuni ya Merchmar ilikuwa na hisa saba au asilimia 70 ya hisa hizo.

 

Kama nilivyogusia awali, IPTL ilikuwa ni mkataba wa kifisadi tangu mwanzo wake kwani wawekezaji hawa wa IPTL hawakuwa na mtaji wala sifa za kupata mtaji kwa wakati. Ndio sababu mradi haukukamilika kwa wakati ingawa nchi ilihitaji umeme kwa dharula.

IPTL ilishindwa kuzalisha kwa wakati na badala yake kukamilisha ujenzi wa mradi miaka mitatu baadaye, yaani mwaka 1998 kutoka mwaka1995 mkataba uliposainiwa kati yake na Tanesco.

 

Mkataba huu wa IPTL ulikuwa wa kuzalisha na kuuza umeme kwa Tanesco kwa miaka 20 na kwamba baada ya hapo mitambo inakuwa mali ya Tanesco!

Jambo baya kabisa katika mkataba huu ilikuwa ni kile kilichoitwa tozo ya gharama ya uwekezaji (capacity charges), tozo hii ilikuwa ya kwanza tangu Tanzania ianze kuingia mikataba.

Je, nini kiliendelea wiki ijayo!

Comments are closed.