Kagere Aapa Kufa na AS Vita Leo

Meddie Kagere

MSHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere ameahidi kufa na kupona kuitungua AS Vita kwenye mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa itakuwa muhimu kwa Simba kupata ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kwenda Robo fainali.

 

Kagere amefunga mabao matatu kwenye mechi za nyumbani za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi hivyo inaonyesha kuwa amekuwa na bahati kubwa. Mabao hayo alifunga dhidi ya JS Saoura mawili na Al Ahly moja.

 

Meneja wa Kagere, Patrick Gakumba ameweka wazi kwamba mteja wake huyo amemuahidi kufunga bao kwenye mechi hiyo ili azidi kupalilia kibarua chake.

 

“Vita kwake ni timu ya kawaida kama ilivyo timu nyingine ambazo huwa anazifunga, ameahidi kufanikisha hilo ili azidi kupalilia kibarua chake inavyopaswa ikiwa ni pamoja na kutimiza ule msemo wa mshambuliaji ni kufunga, namuombea kwa Mungu ili ahadi zake zitimie,” alisema Gakumba.

 

Kwa upande wake Kagere alisema: “Kwa sasa ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji nafasi ya kusonga mbele ila kikubwa tu nawaomba mashabiki wasione taabu kujitokeza uwanjani, waje kwa wingi watupe sapoti nina imani tutafanya vizuri.”

Stori na Khadija Mngwai, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment