The House of Favourite Newspapers

Kagere Amuota Kakolanya, Mwenyewe Acheka Kwa Dharau

Meddie Kagere.

MEDDIE Kagere amesema haikuwa bahati yake kuwafunga Yanga huku akisisitiza kwamba Beno Kakolanya ni kipa.

Katika mchezo huo uliopigwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na matokeo kumalizika kwa suluhu, Kakolanya ndiye aliibuka shujaa kutokana na umahiri wake wa kuokoa hatari zilizokuwa zikielekea golini kwao.

 

Kagere ambaye mashabiki wa Simba walikuwa wakimwaminia kwamba atakinukisha, ni kati ya wachezaji waliokosa nafasi za wazi katika mchezo huo uliojaa upinzani mkubwa baada ya shuti lake alilolipiga ndani ya 18 kupaa huku mashabiki wakiamini kuna mkono wa mtu.

 

Kagere alisema kipa huyo alijitahidi kumsoma yeye na washambuliaji wenzake Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya ambao wote walipata nafasi za kufunga na kushindwa kuzitumia vema.

 

“Tulicheza vizuri lakini hatukuwa na bahati ya ushindi katika mchezo huo na hilo lipo wazi kabisa kwa kila shabiki aliyejitokeza uwanjani kuangalia mchezo huo.


“Naweza kusema kipa wao alitusoma vizuri kabla na baada ya mchezo ndiyo maana alionekana kuokoa hatari nyingi golini kwao, kiukweli yeye ndiye aliyesababisha ile sare,” alisema Kagere.

 

Lakini Kakolanya alipoambiwa maneno hayo akacheeka na kujibu kwamba; “Kwangu baada ya mchezo ule uliopita ni fursa ya kuzidi kujifua na kuonyesha uwezo zaidi katika michezo yetu ambayo inakuja. Ninataka kuwa na uwezo zaidi ya hapa na niwe msaada mkubwa kwenye timu kwa kuzuia kufungwa na wapinzani wetu.”

 

Kipa huyo ambaye kabla ya kutua Yanga alikuwa Tanzania Prisons amegusia kwamba kabla ya mechi yoyote ya timu yake mama yake amekuwa akimwombea kwa kufunga ili aweze kushinda jambo ambalo alilifanya hata kwenye mechi na Simba ambapo alifunga kwa siku tatu.

 

STORI: WILBERT MOLANDI

Comments are closed.