Kagere Atuma Vitisho kwa Yanga

MUITE Meddie Kagere baada ya kuanza ligi kwa kufunga mabao mawili amesisitiza kuwa sasa anataka kufunga kila mchezo atakaocheza ukiwemo ule wa watani zao, Yanga.

 

Kagere ambaye ni raia wa Rwanda, msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu akitupia mabao 23 kimiani na juzi ameanza kuhesabu akaunti yake ya mabao baada ya kufunga mawili dhidi ya JKT Tanzania katika ushindi wa mabao 3-1 ambao Simba ilipata.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kagere alisema kuwa kikubwa alichopanga ni kutumia vema kila nafasi atakayoipata ya kufunga mabao katika mechi ya ligi ili kuhakikisha anatimiza malengo aliyojiwekea ya kuutetea ubingwa wa ligi, pia kulichukua Kombe la FA.

 

Aliongeza kuwa tofauti na majukumu aliyonayo ya kufunga mabao, pia amepanga kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wenzake bila ya kuangalia ufungaji bora anaoutetea katika msimu huu.

 

“Nafahamu mashabiki wa Simba bado wanamaumivu ya kuondolewa Caf ambayo sisi yanatuumiza na yatachukua muda mrefu kuondoka kichwani mwetu, kwani tulikuwa tuna matarajio makubwa ya kufika mbali Caf zaidi ya msimu uliopita.

 

“Lakini ndiyo matokeo, hivyo basi hasira zangu zote nazielekeza kwenye ligi na kama mshambuliaji nachukua majukumu yote ya kuhakikisha timu inapata ushindi ili tuutetee ubingwa wa ligi, pia kuchukua Kombe la FA.

“Hivyo, nilichopanga ni kutumia vema kila nafasi nitakayoipata uwanjani ikiwemo kufunga na kutengeneza mabao bila ya kuangalia ufungaji bora kwangu siyo muhimu sana.

“Muhimu kwangu ni kuchukua makombe ambacho ndiyo kitu cha msingi kilichonileta Simba, hayo mengine yatajulikana mwishoni mwa msimu ikitokea nimekuwa mfungaji bora, basi nitashukuru,” alisema Kagere.

 

AVUNJA, AWEKA REKODI YAKE

Wakati akishangilia mabao hayo mawili, Kagere ameweka rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi msimu huu kwenye ligi kuu. Mshambuliaji huyo, alifunga bao dakika ya kwanza na sekunde ya 15 akiunganisha pasi nzuri ya ndani ya 18 kutoka kwa Mzamiru Yassin.

Kutokana na bao hilo la mapema msimu huu, Kagere anakuwa amevunja rekodi yake ya msimu uliopita ambapo alifunga bao la mapema dhidi ya Prisons katika dakika ya pili na sekunde ya 15.

 

AUSSEMS ROHO KWATU KWA KAGERE

Naye Kocha wa Simba, Patrick Aussem alimzungumzia Kagere ambapo alisema: “Pongezi nyingi ziende kwa Kagere ambaye alianza vizuri ligi kwa kufunga mabao mawili pekee, hivyo ninatarajia kumuona akiendelea kufunga mabao mengi zaidi ya msimu uliopita.”

 

RAGE AKAZIA UFUNGAJI BORA

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amesema kasi aliyoanza nayo mshambuliaji huyo anampa asilimia mia moja ya kutwaa tena tuzo ya mfungaji bora katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

“Sina shaka na uwezo wa Kagere, amekuwa mpambanaji uwanjani na shughuli yake inaonekana anapokuwa kazini, nampa asilimia 100 za kuchukua tuzo nyingine msimu huu.

 

“Ujue ukimzungumzia Kagere, huyu ni mshambuliaji bora pale Simba na ataisaidia tena kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita, naomba tu asipate majeraha kwani atayafanya yaleyale ya msimu uliopita.

 

“Kagere ni sawa na Cristiano Ronaldo, angalia namna anavyofunga mabao kwa vichwa, miguu, yaani amekamilika kila idara na chenga anapiga, wawili hawa hawana tofauti yoyote ile.”


Loading...

Toa comment