The House of Favourite Newspapers

Kagere, Bocco wampa jeuri Mbelgiji kwa Waarabu

KASI ya safu ya ushambuliaji ya Simba, imempa jeuri Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems akitamka kuwa ana matumaini makubwa ya kuwafunga wapinzani wao JS Saoura nchini kwao Algeria.

 

Simba inatarajiwa kuvaana na Saoura Machi 9, mwaka huu huko Algeria katika mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa awali kushinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Safu ya ushambuliaji ya Simba inaongozwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco ambayo imefanikisha ushindi wa michezo minne migumu mfululizo dhidi ya Al Ahly 1-0, Yanga 1-0, African Lyon 3-0 na Azam FC 3-0.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema kuwa anafurahishwa na kasi hiyo ya ushambuliaji ambayo imeipa matokeo mazuri kutokana na kutimiza majukumu yao.

Aussems alisema, bado anaendelea kuifanyia kazi safu hiyo ya ushambuliaji ili kuhakikisha wanaendelea na kasi hiyo ya kufunga kwenye michezo ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapokutana na Saoura na AS Vita.

 

Aliongeza kuwa, kama washambuliaji hao wataendelea kucheza kwa kuelewana, basi ana matumaini makubwa ya kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo ya ligi na michuano ya kimataifa.

“Niwapongeze wachezaji wangu kwa matokeo mazuri ya mfululizo ambayo timu yangu imeendelea kuyapata, kila mmoja katimiza majukumu yake ya ndani ya uwanja.

 

“Matokeo hayo yananipa matumaini ya kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo ya ligi tutakapocheza na Lipuli na baadaye dhidi ya Saoura tutakapokuwa ugenini.

“Washambuliaji wangu wanacheza vizuri kwa kuelewana na kufanikisha ushindi wa nne mfululizo ambao tumeupata, hivyo bado ninaendelea kuwapa mbinu zaidi za kufunga ili kuhakikisha ninafanikisha ushindi katika michezo inayofuata ya ligi na michuano ya kimataifa,” alisema Aussems.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.