Kagere, Molinga Matatani, Wameondoka Nchini
TAMKO la Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kuwataka wachezaji wakiwemo wa kimataifa wanaocheza soka hapa nchini kutoondoka nje ya mipaka ya nchi hii ikiwa ni sehemu ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona, baadhi ya wachezaji akiwemo Meddie Kagere na David Molinga wa Simba, wapo matatani.
Hivi karibuni baada ya Serikali kutangaza kuzuia mikusanyiko isiyokuwa ya lazima katika kujikinga na maambukizi hayo ambayo ni tishio duniani, ligi zilisimamishwa ikiwemo Ligi Kuu Bara kwa kipindi cha siku 30 kuanzia Machi 17, mwaka huu.
Karia amesema kuwa wachezaji na wafanyakazi wote wa klabu za hapa nchini ambao wametumia mapumziko
hayo kwenda makwao hususan nje ya nchi, hawatawapokea watakaporejea.
“Tumetoa mapumziko kama Serikali ilivyoelekeza, lakini tunawaambia viongozi wa klabu kuwa hatujatoa likizo, nimeshapata taarifa baadhi ya klabu ambazo zina wachezaji wa kigeni au wafanyakazi wa kigeni wanafanya matayarisho ya kuwaruhusu kwenda kwao.
“Kwa hiyo kufanya hivyo itakuwa kinyume na maelekezo ya Serikali, kwa sababu watakapoenda nje sisi hatutawaruhusu tena kurudi hapa, tukiwaruhusu tutakuwa tunafanya mchezo, hivyo hatutawaruhusu kushiriki tena kwenye michezo yetu,” alisema Karia.
Mpaka jana Jumamosi, kulikuwa na taarifa kwamba wachezaji wa Simba, Meddie Kagere ameelekea kwao Rwanda
na Sharaf Shiboub yupo Sudan. Upande wa Yanga, ilitoka taarifa kwamba mshambuliaji wa timu hiyo, David Molinga raia wa DR Congo, ameelekea nchini Ufaransa kuonana na familia yake, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael naye ameomba ruhusa ya kwenda kwao Ubelgiji.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fedrick Mwakalebela, amesema: “Kama kauli hiyo ya Rais wa TFF itakuwa hivyo, ni dhahiri sisi tutapata athari kubwa kwani mchezaji wetu David Molinga na Kocha Luc Eymael wameomba ruhusa na tayari wamesafi ri. “Tutawasiliana na TFF na endapo watashindwa kutusaidia kwa namna yoyote basi hatutakuwa na namna ya kuangalia njia nyingine.”
STORI NA MUSA MATEJA, CHAMPIONI