The House of Favourite Newspapers

Kahaba Kutoka China-15

0

Joshua alikuwa akiishi kwa wasiwasi sana toka siku ya mwisho ambayo alinusurika kufanyiwa kitu kibaya na Bwana Shedrack ambaye alionekana kuwa mwingi wa hasira. Kuanzia siku hiyo maisha yake yakabadilika kabisa, aliutambua vilivyo utata ambao alikuwa nao Bwana Shedrack, utata ambao alikuwa akiwafanyia vijana wengine ambao walikuwa wakimtaka binti yake, Rose.

Joshua alijua fika kwamba alikuwa amekwishaingia katika uhasama mkubwa na mzee huyo ambaye bado alikuwa akimtafuta kila siku. Hali ikazidi kuwa mbaya kwake kitu kilichompelekea kufanya jambo moja ambalo aliliona kuwa sahihi katika kipindi hicho, kutafuta chumba kingine na hatimae kuhama katika mtaa huo.

Katika kipindi ambacho alikuwa akitafuta chumba katika mtaa mwingine, alikuwa akichelewa kufika katika kile chumba chake kitu ambacho kilimfanya kuingia saa nane usiku katika kipindi ambacho aliona kwamba Bwana Shedrack asingeweza kuja kumuulizia. Maisha yake ya wasiwasi yalindelea zaidi na zaidi, kila siku alikuwa mtu wa kujificha ili kuukimbia uso wa Bwana Shedrack ambaye alijua fika kwamba bado alikuwa akimtafuta.

Siku zikaendelea kukatika huku akiendelea kuishi maisha ya kujificha mpaka pale ambapo akakamilisha mipango yake ya kuhama na kuhamia Kijitonyama, huko akaweza kuishi kwa amani, hakutaka watu wengi wapafahamu alipokuwa amehamia zaidi ya rafiki yake, Ally ambaye alikuwa akiishi chumba cha jirani katika nyumba ile aliyohama.

Maisha huko yakaendelea zaidi, muda mwingi  Joshua alikuwa akimfikiria Rose. Japokuwa makubaliano yao ambayo walikuwa wameyaweka yalikuwa ni kuzidi kuwasiliana katika kipindi ambacho wasingekuwa pamoja lakini katika kipindi hicho hali ilikuwa tofauti kabisa, Rose hakuwa akipatikana simuni jambo ambalo lilikuwa limemuweka Joshua kwenye wakati mgumu sana.

Joshua hakutaka kukata tamaa, kila siku alikuwa akijaribu kumtafuta Rose simuni lakini matokeo yalikuwa ni yale yale na wala hayakuweza kubadilika kabisa, kwamba Rose hakuwa akipatikana kabisa. Ukiachana na Rose, wakati mwingine alikuwa akiifikiria mimba ambayo alikuwa nayo Rose, kiu ya moyo wake katika kipindi hicho ilikuwa ni kumuona mtoto ambaye angezaliwa na Rose, mtoto ambaye alikuwa ni damu yake.

Joshua hakujua ni mahali gani ambapo alitakiwa kumuulizia Rose na hatimae kumpata. Alipokuwa akikumbuka mengi ya nyuma ndipo hapo alipoonekana kukumbuka kitu kwamba mara ya mwisho ambayo alikuwa akiagana na Rose alimwambia kwamba alikuwa akienda kuishi kwa rafiki yake ambaye alikuwa akiishi katika hosteli iliyokuwa maeneo ya Sinza makaburini.

Baada ya kulikumbuka hilo, Joshua hakutaka kuendelea kubaki chumbani kwake, alichokifanya ni kuanza kuelekea katika hosteli hiyo ili kuangalia kama angeweza kumpata mpenzi wake, Rose. Ndani ya daladala Joshua alikuwa na mawazo tele, alikuwa akimkumbuka sana mpenzi wake, Rose, alikuwa na hamu kubwa ya kuliona tumbo lake ambalo lilikuwa limembeba mtoto wake.

Daladala ambayo alikuwa ameipanda kuelekea Sinza haikuchukua muda mrefu, akafika Sinza Makaburini ambapo moja kwa moja akateremka na kisha kuanza kuangalia huku na huko kana kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani. Mbele yake kulionekana kuwa na nyumba za kawaida tu, hakuona kama alikuwa ameiona hosteli yoyote ile mbele ya macho yake. Alichokifanya ni kuwasogelea vijana ambao walikuwa pembeni na kisha kuanza kuongea nao.

“Mambo vipi!” Joshua aliwasalimia vijana wale ambao wakainua vichwa vyao kutoka katika drafti walilokuwa wakilicheza na kumwangalia Joshua.

“Poa” Vijana wale waliitikia na kisha kuyarudisha macho yao katika drafti lao.

“Samahani kidogo. Naomba niulize swali moja” Joshua aliwaambia vijana wale ambao wakaacha kucheza drafti na kisha kuanza kumwangalia usoni.

“Uliza tu”

“Kuna hosteli yoyote hapa karibu?” Joshua aliuliza huku akiangalia huku na kule.

“Hosteli? Mmh! Hapa ninachokijua ni kwamba kuna hosteli moja tu, tena ya wasagaji ipo hapo nyuma” Kijana mmoja alimjibu Joshua ambaye akaonekana kushtuka.

“Hosteli ya wasagaji?”

“Yeah! Hosteli ya wasagaji. Mbona umeshtuka sana kaka? Demu wako anaishi humo nini?” Kijana mmoja alimuuliza huku uso wake ukionyesha tabasamu.

“Hapana. Kuna mtu nataka kwenda kumuulizia”

“Nae anaishi humo?”

“Hapana. Nadhani alikuja mara moja tu”

“Basi sawa”

Kijana mmoja akaanza kumuelekeza Joshua mahali ambapo hosteli hiyo ilipokuwa ikipatikana, baada ya kuona kwamba maelekezo ambayo alipewa yalikuwa yamemuingia kichwani, akaondoka mahali hapo. Joshua akaanza kuzifuata njia zote ambazo alikuwa ameelekezwa mpaka macho yake kutua katika nyumba moja kubwa ambayo iliandika MARIA HOSTEL.

“Nadhani ndio hapa” Peter alisema na kisha kuanza kulisogelea geti. Alipolifikia, akaanza kuligonga.

Msichana mmoja aktokea na kisha kulifungua geti lile na macho yake kutua usoni mwa Joshua. Tabasamu kubwa likatoka usoni mwa msichana yule, sura ya uchangamfu ambayo alikuwa nayo Joshua ikaonekana kuziteka hisia zake kwa kipindi kifupi sana.

“Karibu” Msichana yule alimkaribisha Joshua.

“Asante. Samahani, kuna msichana nimekuja kumuulizia” Hoshua alimwambia msichana yule.

“Msichana yupi?”

“Anaitwa Rose”

“Rose! Rose yupi?”

“Alikuja kumuona msichana fulani mahali hapa”

“Msichana yupi?”

“Anaitwa Irene”

“Mmmh!”

“Kuna nini tena?”

“Kuna Irene wengi sana mahali hapa”

“Ninayemfahamu mimi ana makalio makubwa kwa nyuma, si mrefu sana, ni mweupe. Nilimuona siku moja tu akiwa na msichana wangu” Joshua alimwambia msichana yule.

“Daah! Huyo msichana anaitwa Irene Godfrey”

“Ok! Nadhani ndiye yeye! Nimemkuta?” Joshua aliuliza.

“Alifariki wiki iliyopita” Msichana yule alitoa jibu ambalo lilimchanganya sana Joshua.

“Alifariki?” Joshua aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa na jibu lile.

“Ndio. Ni wiki imepita toka afariki”

“Alikuwa anaumwa?”

“Hapana. Aliuawa”

“Daah! Kwa hiyo hata wewe haujui msichana wangu atakuwa amekwenda wapi?”

“Hapana. Msichana mwenyewe sijawahi hata kumuona” Msichana yule alimwambia Joshua.

Joshua akaonekana kuchoka kupita kawaida, maneno ambayo aliyazungumza msichana yule yakaonekana kumlegeza sana. Hakuamini kama kweli katika kipindi ambacho alikuja ndani ya hosteli ile alimkosa Rose, msichana ambaye alikuwa akitamani kumuona katika kipindi hicho. Joshua akabaki kimya kwa muda huku akionekana kama mtu ambaye alikuwa akijifikiria kitu fulani kichwani mwake. Kuondoka alikuwa akitamani kuondoka lakini hata kubaki napo alitaani kubaki, hakujua afanye nini.

“OK! Nashukuru” Joshua alimwambia msichana yule na kisha kuondoka mahali hapo.

Akili yake haikukaa sawa kabisa katika kipindi hicho, yule mtu ambaye alikuwa amemfuata ndani ya hosteli ile alikuwa amemkosa na hakujua ni kwa namna gani angeweza kumpata mtu huyo, Rose. Moyoni hakujisikia kuwa na furaha kabisa, muda wote alionekana kuwa na majonzi kupita kawaida. Kitendo cha kumkosa Rose kilimaanisha kwamba asingeweza kumuona tena kwani hata kwenda kumuulizia nyumbani kwao lingekuwa suala gumu kutokea.

Kuanzia siku hiyo Joshua hakuonekana kuwa na furaha, muda mwingi alionekana kuwa mpweke. Joshua hakutaka kuendelea na kazi katika kipindi hicho, kitu alichoamua ni kuanza kufanya biashara tu. Mara kwa mara alikuwa akitoa mizigo ya viazi mkoani Mbeya na kisha kuileta jijini Dar es Salaam na kuiuza kitu ambacho kilionekana kumpatia fedha ambazo zilionekana kumtosha.

Joshua hakuonekana kuridhika, mara kwa mara alikuwa akibadilishabadilisha biashara kutokana na misimu kadhaa ya mazao kwa jinsi ilivyokuwa ikienda katika kipindi husika. Kujituma kwake, kuangaika kwake pamoja na kujitolea muda wake mwingi katika kufanya biashara vilikuwa vitu ambavyo vilimfanya kujipatia kiasi cha fedha na kisha kuanza kujenga nyumba yake mwenyewe.

Kila siku Joshua akawa mtu wa kuingiza fedha, kila siku akawa mtu wa kupokea oda za watu mbalimbali ambao walikuwa wakitaka mazao husika katika kipindi husika cha mazao fulani. Kutokana na kuwa na fedha za kutosha, wanawake nao hawakubaki nyuma, kila siku walikuwa wakijitahidi kwa nguvu zao zote kutaka kumuingiza Joshua katika mikono yao.

Joshua hakuonekana kuwa mwanaume mwepesi kukamatika na wasichana hao, kila siku mawazo yake yalikuwa kwa msichana wake, Rose ambaye alikuwa mjauzito. Moyoni mwake tayari alijihesabia kuwa baba na hivyo hakutakiwa kuangaika na wasichana wengine ambao walikuwa wakiendelea kujigonga kwa kasi. Japokuwa alikuwa mbali na Rose lakini kila siku moyo wake ulikuwa ukimwambia kitu kimoja kwamba msichana Rose bado alikuwa mpenzi wake na kama ingetokea siku wakaonana basi angeweza kumwambia wafunge ndoa na hatimae kumlea mtoto wao pamoja.

Mwaka wa kwanza ukakatika na mwaka wa pili kuingia. Mwaka wa pili ukaisha na mwaka wa tatu kuingia lakini wala Joshua hakuweza kumuona msichana wake, Rose. Moyo wake uliendelea kuwa na maumivu makali, mawazo juu ya Rose na mtoto wake yalikuwa yakimwandama kila siku katika maisha yake. Kuna wakati alikuwa akijifikiria kumchukua msichana mwingine na hatimae kufunga ndoa lakini kila alipokuwa akimfikiria zaidi Rose, wazo hilo lilikuwa likimtoka kwa wepesi sana kichwani mwake.

Mwaka wa nne ukaingia lakini bado hali iliendelea kuwa vile vile, hakuweza kumuona Rose. Maisha ya nyumbani kwake yalionekana kuwa si mazuri japokuwa alikuwa na kila kitu. Nyumba yake kubwa hakuiona kuwa na thamani, gari lake la kutembelea hakuliona kuwa na thamani na hata biashara zake pia hakuziona kuwa na thamani katika kipindi hicho. Rose pamoja na mtoto wake ambaye wala hakuwahi kumuona ndio walikuwa watu ambao walionekana kuwa na thamani kuliko kitu chochote katika maisha yake kwa wakati huo.

Mpaka mwaka wa tano unaingia, bado hali haikuwa imebadilika, iliendelea kuwa vile vile. Joshua akaonekana kuchoka, Joshua akaonekana kukata tamaa kuendelea kusubiri, uamuzi ambao alikuwa ameamua kuuchukua katika kipindi hicho ni kutafuta msichana ambaye alionekana kufaa kuwa mke. Hilo halikuwa tatizo kwake, kwa sababu wasichana walikuwa wengi waliokuwa wakimfuatilia, akaanza kuwafikiria wasichana kadhaa, wasichana ambao aliamini kwamba walikuwa wametulia na kisha kuanza kuwachuja.

Zaidi ya wasichana kumi na mbili wakaja kichwani mwake, akaanza kumfikiria mmoja baada ya mwingine. Mchujo ulikuwa mkali kichwani mwake mpaka pale ambapo alimpata mmoja ambaye akaonekana kufaa kuwa mke wake, huyu aliitwa Debora.

Kwa haraka sana Joshua akachukua simu yake na kisha kuanza kulitafuta jina la Debora, alipolipata akaanza kumpigia simu. Lengo lake katika kipindi hicho lilikuwa ni kupanga miadi na Debora waweze kuonana sehemu fulani ambako huko angemwambia ukweli kwamba alikuwa akitaka kumuoa kwa sababu alikuwa msichana ambaye alimuona kufaa kuishi nae na kumzalia watoto pamoja na kutengeneza familia iliyokuwa na upendo.

Debora alipoambiwa kukutana na Joshua, kwanza moyo wake ukafurahi, hakuamini kwamba mwanaume yule mwenye pesa, mwanaume ambaye alikuwa akimfikiria kila siku ndio ambaye alikuwa amempigia simu na kutaka kuonana nae. Hiyo ikaonekana kuwa bahati kwa Debora, bahati ambayo kamwe hakutakiwa kuiacha ipite.

“Kesho saa ngapi?” Debora alimuuliza Joshua simuni.

“Saa moja usiku. Utakuwa na nafasi?”

“Ndio. Muda wote nina nafasi. Wewe tu Joshua” Debora alimwambia Joshua.

“Kama muda wote una nafasi, kwa nini tusifanye hata leo saa kumi na moja na nusu jioni?” Joshua aliuliza.

“Hakuna tatizo. Panga pa kukutania” Debora alimwambia Joshua.

“Naomba tuonane pale Travertine hotel. Nina mengi ya kuongea nawe siku ya leo” Joshua alimwambia Debora ambaye bila shaka akakubaliana nae.

Siku hiyo ikaonekana kuwa siku njema kwa Debora, muda mwingi alikuwa akijifikiria ni aina ya mavazi gani ambayo alitakiwa kuyavaa siku hiyo. Kila vazi ambalo alikuwa akilifikiria aliliona kutofaa kuvaliwa siku kama hiyo. Alitamani kuonekana mpya machoni mwa Joshua, hata kama katika kipindi cha nyuma alikataa kuwa wake, siku hiyo alitaka kuhakikisha kwamba mwanaume huyo anakuwa wake na hatimae mambo mengine kufuata.

Saa kumi na moja na dakika ishirini Debora alikuwa akiingia ndani ya eneo la hoteli ya Travertine. Macho yake yalipotua usoni mwa Joshua ambaye alikuwa amekaa katika moja ya viti vilivyozunguka meza iliyokuwa na vinywaji, tabasamu pana likaonekana usoni mwake. Joshua akainuka kutoka kitini na kisha kumsogelea Debora na kumbusu shavuni.

“Unanukia vizuri” Joshua alimwambia Debora ambaye alikuwa akitabasamu tu.

“Asante”

“Manukato gani tena?” Joshua alimuuliza debora.

“La Laspinho” Debora alijibu.

“Mmh! Yananukia vizuri sana”

“Hata wewe pia unanukia vizuri pia”

“Najua. Ila sikushindi wewe Debora” Joshua alimwambia Debora.

Hapo hapo Joshua akamuita mhudumu ambaye akafika mahali hapo na kisha kumuagiza vinywaji. Siku hiyo kwake ikaonekana kuwa siku maalumu ambayo alitakiwa kuzungumzia suala moja tu, ndoa na kisha kumsikiliza Debora angesema nini juu ya hilo. Kwake, hakuwa na wasiwasi kabisa, kitu ambacho alikuwa akikiamini ni kimoja tu kwamba msichana Debora asingeweza kukataa katika kipindi ambacho angemwambia ombi la kuwa mke wake wa ndoa.

“Atakubali tu” Joshua alijisemea katika kipindi ambacho alikuwa akinywa juisi huku akimwangalia Debora.

****

Wote walibaki wakiangaliana kwa macho ya kimahaba, katika kipindi hicho kila mtu alionekana kuvutiwa na mwenzake, walikuwa wakiangaliana huku wakipeana tabasamu kuonyesha ni jinsi gani walikuwa wamevutiana. Mpaka chakula kinaletwa mahali hapo, kila mmoja alikuwa akitumia muda wake kumwangalia mwenzake kwa macho ya kisiri. Ni kweli walikuwa wamependana, ni kweli katika kipindi hicho kila mmoja alionekana kuvutiwa na mwenzake.

Joshua alijua fika kwamba msichana Debora alikuwa akimpenda sana na alikuwa akimpenda zaidi ya alivyokuwa akifikiria lakini katika kipindi hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kuanzisha mazungumzo yake kumwambia Debora kwamba alikuwa akitaka sana awe mke wake wa ndoa. Katika macho yake, Debora alionekana kuwa mwanamke mzuri, mwanamke ambaye alistahili kuwa na mtu kama yeye, mtu mwenye pesa za kununulia kila alichokuwa akikitaka.

“Hallooow” Joshua aliita mara baada ya kuona ukimya umetawala mahali hapo.

“Hallow” Debora aliitikia na kisha kuanza kucheka.

Moyo wa Joshua ukamlipuka, damu yake ikaanza kuzunguka kwa kasi mwilini mwake, tabasamu ambalo alikuwa amelitoa Debora likaonekana kumtetemesha moyo wake kupita kawaida. Uzuri wa Debora ukaonekana kuwa mara nne ya ule uzuri ambao alikuwa nao, tabasamu lile likaonekana kuuteka zaidi moyo wa Joshua. Akajikuta akizidi kumpenda Debora, akajikuta akizidi kumpenda msichana huyo ambaye katika kipindi hicho alionekana kuwa mzuri hata zaidi ya Malkia wa kipindi kirefu kilichopita, malkia ambaye alikuwepo katika nchi ya Misri, malkia aliyeweza kuolewa na kaka zake wa damu, malkia mrembo ambaye alikuwa akijulikana kuwa mrembo zaidi ya wanawake wote duniani, malkia Cleopatra.

“Debora” Joshua alijikuta akiita kwa sauti ya chini, sauti ambayo ilielezea kile kilichokuwa moyoni mwake.

“Abeee” Debora aliitikia kwa heshima zote.

“Nilisahau kukwambia kitu kimoja” Joshua alimwambia Debora ambaye alikuwa akitabasamu muda wote hali iliyomfanya Joshua kuchanganyikiwa zaidi.

“Kitu gani?”

“Umependeza mno Debora. Nani alibuni hayo mavazi yako?” Joshua alimuuliza Debora ambaye akaacha kula na kisha kuanza kujiangalia.

“Nilinunua dukani wala hayakubuniwa na mwanamitindo yeyote yule” Debora alijibu huku akiendelea kuliangalia vazi alilokuwa amelivaa.

“Hivi kwa uzuri wote huo Debora, kweli kuna wanaume walishindwa kuja kwako na kukwambia kwamba wanakupenda?” Joshua alimuuliza Debora.

“Walikuja wengi”

“Ukawaambiaje baada ya kukwambia wanakupenda?”

“Nilichukulia kawaida tu kwa sababu sikuwa tayari kuolewa wala kuingia katika mahusiano” Debora alitoa jibu ambalo kwa kiasi fulani likamfanya Joshua kubadilika.

“Haukuwa tayari kuingia kwenye mahusiano?” Joshua aliuliza huku akionekana kushtuka kidogo.

“Yeah! Ilikuwa zamani”

“Ila sasa hivi iko vipi?”

“Kwa sasa nipo tayari” Debora alitoa jibu ambalo likamfanya Joshua kushusha pumzi nzito.

“Nimelifurahia jibu lako” Joshua alimwambia Debora ambaye tabasamu halikumuisha usoni mwake.

Muda wote huo Joshua alikuwa akizunguka huku na kule. Japokuwa alikuwa akipiga stori nyingi lakini alikuwa akitaka kufika sehemu moja tu, sehemu ambayo ilikuwa ni kumwambia kwamba alikuwa akimpenda. Maongezi yake katika wakati huo yalifanana na mtu ambaye alikuwa akitaka kwenda Afrika Kusini, ila njia alizokuwa akipita ni kuelekea Kigoma, kuingia Burundi na Kongo na mwisho wa siku kusafiri tena kuelekea Zimbabwe na kisha kuingia nchini Afrika Kusini.

Maongezi yake yalikuwa marefu sana na wakati kulikuwa na njia fupi, njia ambayo ingemfanya kufika pale alipokuwa akitaka tofauti na muda ambao alikuwa akiutumia kuzunguka huku na kule. Japokuwa moyo wake ulikuwa ukiamini kwa aslimia mia moja kwamba Debora asingeweza kupindua lakini badio alikuwa na kijihofu moyoni mwake, siku hiyo alishangaa kuona ujasiri wote ambao alikuwa nao moyoni mwake ukiwa umempotea kabisa.

“Kuna kitu ningependa kukwambia jioni ya leo” Joshua alimwambia Debora.

“Kitu gani?” Debora aliuliza swali ambalo lilimfanya Joshua kushusha pumzi ndefu na nzito.

“Nimetokea ku…….” Joshua alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, simu yake ya mkononi ikasikika ikianza kuita.

Akanyamaza, alichokifanya ni kuichukua simu ambayo ilikuwa mfukoni mwake na kisha kuanza kuangalia kioo, namba ilikuwa ngeni kabisa. Hakuonekana kujali sana, alichokifanya ni kuipokea simu na kisha kuipeleka sikioni.

“Hallow” Joshua aliita huku akionekana kujiamini.

“Unaongea na kituo kikuu cha polisi cha Osterbay” Sauti ya upande wa pili ilisema.

“Polisi?” Joshua aliuliza huku akionekana kushtuka.

“Ndio. Polisi”

“Kuna nini tena. Mbona umenitisha?”

“Unahitajika kituoni” Sauti ya upande wa pili ilijibu.

“Mungu wangu! Kituoni kufanya nini tena? Kuna baya lolote nililolifanya? Mbona kila siku ninalipa kodi kila ninapoleta mizigo yangu!” Joshua alisema huku akionekana kuwa na hofu.

“Unahitajika mahali hapa. Upo wapi kwa sasa?” Sauti ya p[olisi iliuliza.

“Nipo Magomeni”

“Sawa. Tunahitaji ndani ya dakika thelathini uwe umefika mahali hapa” Polisi yule alimwambia.

“Kuna amani afande?”

“Ndio. Hautakiwi kuhofia kitu chochote kile”

“Oooopppsss..! Nakuja” Joshua alisema na kisha kukata simu.

Amani yote ambayo alikuwa moyoni mwake ikaonekana kupotea, simu ambayo ilikuwa imeingia kutoka polisi ikaonekana kubadilisha hali yote ya furaha ambayo alikuwa nayo na kuingiwa na hali ya hofu. Kwanza kabla hajaongea chochote kile na Debora akaanza kufikiria kuhusiana na biashara zake ambazo alikuwa akizifanya, alionekana kuwa na hofu kila wakati.

Akaanza kuwafikiria madereva ambao walikuwa wakiendesha magari yake kwa kuona kwamba inawezekana walikuwa wamesafirisha mirungi pamoja na bangi na hivyo magari yake kukamatwa na yeye kuhitajika kituo cha polisi. Kila kitu ambacho alikuwa akikifikiria mahali hapo kikaonekana kumtia hofu, hakukuonekana kuwa na amani hata mara moja.

“Kuna nini tena?” Debora alimuuliza Joshua mara baada ya kukata simu.

“Simu kutoka polisi” Joshua alisema huku akionekana kuwa mnyonge.

“Wamesemaje?”

“Wananihitaji sasa hivi” Joshua alimjibu debora.

“Mmmh! Kiamani au?”

“Alivyosema ni kiamani lakini sidhani. Hiyo ni mbinu mpya wanayoitumia polisi pindi wanapotaka kukukamata” Joshua alimwambia debora.,

“Sasa unahisi kuna kitu gani kimetokea huko?”

“Mmh! Sijui. Yaani hapa naanza kufikiria biashara zangu. Hawa madereva wangu watakuwa wamefanya kitu. Haiwezekani iwe hivi. Nimefanya biashara kwa miaka zaidi ya mitatu, sijawahi kuitwa na polisi kituoni” Joshua alimwambia Debora.

“Inabidi uende kuwasikiliza kwanza”

“Mmmh! Sijui nifanye nini. Ngoja nikupeleke nyumbani kwanza” Joshua alimwambia Debora.

Mazungumzo yalikuwa yamekwishaingia doa, katika kipindi hicho zile hali za mapenzi ambazo walikuwa nazo katika kipindi kifupi kilichopita zikaonekana kupotea. Badala ya mzunguko wa damu wa Joshua kuwa mkubwa kutokana na hisia za kimapenzi alizokuwa nazo juu ya debora, katika kipindi hicho mzunguko ule ukabadilika, haukuwa ukizunguka kwa kasi kwa sababu ya hisia za kimapenzi, ulikuwa ukizunguka kwa kasi kwa sababu moyo wake ulikuwa umejawa na hofu kubwa.

Walipotoka mahali pale, wakaingia ndani ya gari na kisha kuanza kumpeleka Debora Mwananyamala alipokuwa akiishi. Ndani ya gari kila mmoja alionekana kuwa kimya, hofu kubwa bado ilikuwa ikiendelea kuutawala moyo wake, hakuamini kwamba kulikuwa na polisi ambao walikuwa wakikuita kituoni kiamani, kichwa chake kiliamini kwamba kila polisi ambaye alikuwa akikuita kituoni alikuwa akikuita kwa sababu ulikuwa umefanya kosa fulani na hivyo walikuwa wakitaka kukukamata kirahisi bila kuangaika kutembea mpaka kuchoka au kuchoma mafuta ya gari lao.

“Safari njema Joshua. Kuwa makini barabarani” Debora alimwambia Joshua mara baada ya kumteremsha katika mtaa wa mwananyamala maeneo ya Komakoma.

“Hakuna tatizo. Take care” Joshua alimwambia Debora.

Joshua hakutaka kupoteza muda wake mahali hapo, japokuwa alikuwa na wasiwasi mwingi lakini hakuonekana kuwa na jinsi, ilimpasa kwenda katika kituo cha polisi kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea. Njiani, kama kawaida yake hakuonekana kuwa na furaha kabisa, kitu ambacho kilimfanya kumuita Debora na kuongea nae katika kipindi hicho alikuwa ameachana nae huku akiwa hajamwambia kile alichotaka kumwambia, hiyo ilimuuma sana.

Kutoka Mwananyama Komakoma mpaka katika kituo cha Osterbay wala hakikuwa mbali, akafika na kisha kuanza kueleka katika kaunta ya kituoni hapo. Alipofika, akajitambulisha na kumwambia polisi aliyemkuta katika kaunta ile kwamba alikuwa amepigiwa simu na kuambiwa alikuwa akihitajika katika kituo hicho.

“Wewe ndiye Joshua?” Polisi yule aliyekuwa kaunta alimuuliza.

“Ndio mimi”

“Sawa. Ingia ndani ya chumba hicho” Polisi yule alimwambia Joshua ambaye alionekana kuwa na wasiwasi zaidi.

Maneno aliyoambiwa kuingia ndani ya chumba kidogo kilichokuwa katika kituo kile yalionekana kumuogopesha zaidi. Kwanza akageuka nyuma na kisha kuangalia nje, polisi kadhaa walikuwa wametulia katika viti vyao wakipiga stori tu. Katika kipindi hicho ni wazo moja tu ndio ambalo lilikuwa likimjia kichwani mwake, wazo lililomtaka akimbie mahali hapo na kurudi alipotoka.

Kitendo cha kuambiwa kwamba aingie ndani ya chumba kile kilionekana kama kujikamatisha kirahisi na kizembe sana, kujikamatisha katika hali ambayo hakutarajiwa kuifanya kabla. Kichwa chake kikawa kikiuliza maswali yasiyokuwa na majibu, moyo wake ukagawanyika, upande mmoja ulimwambia aingie lakini upande mwingine ulikuwa ukimkataza kufanya hivyo kwa kuwa lilikuwa kosa ni sawa na kuliwasha pipa kwa petroli na wewe kujiingiza mzima mzima.

“Samahani afande. Kuna usalama?” Joshua alimuuliza polisi yule huku akianza kutokwa na kijasho chembamba.

“Mbona unaogopa?”

“Dada, hakuna mtu anayekuwa na amani mara anapoambiwa anahitajika polisi. Unakuwa na amani gani na wakati kitendo cha kuingia hapa tu umebakiasha hatua moja ya kueleka jela? Yaani ukitoka hapa unakwenda mahakamani na kisha kuingia jela kwenyewe. Naomba uniambie. Kuna amani?” Joshua alimuuliza polisi yule.

“Yeah! Kuna amani” Polisi yule alimwambia Joshua.

Japokuwa alikuwa amehakikishiwa amani lakini moyo wake ukaopnekana kulipinga hilo. Kwa hatua za taratibu zilizojaa wasiwasi akaanza kusogea ndani ya chumba kile, alipoufikia mlango, akaingia.

Macho yake yakatua kwa mwanamke mmoja, mwanamke ambaye alikuwa na uhakika kwamba alikwishawahi kumuona sehemu fulani kipindi kirefu kilichopita, ukiachana na mwanamke huyu, pembeni kulikuwa na mwanamke mwingine wa Kichina. Joshua akaonekana kushtuka, mwanamke ambaye alikuwa amemuhitaji kwa muda wa miaka mitano, leo hiyo alikuwa mbele yke akiwa amebeba mtoto, akajihisi furaha kubwa moyoni mwake, wasiwasi wote ambao alikuwa nao ukaonekana kupotea ndani ya sekunde moja, kwa kasi ya ajabu, mwanamke yule akamuweka mtoto chini na kumsogelea na kisha kumkumbatia huku kila mmoja akianza kulia.

“Rose….Rose…Rose…” Joshua aliita huku akiwa amekumbatiana na Rose na machozi yakimtoka.

“Joshua. Joshua mpenzi. Hatimae nikutana na wewe” Rose alimwambia Joshua.

Kila mtu akabaki kimya mahali pale wakiwaangalia wapendao hao ambao walikuwa wakilia huku wakiwa wamekumbatiana. Kukutana kwa mara nyingine lilikuwa ni tukio ambalo hakulitegemea mtu yeyote yule katika kipindi hicho, kwao ukaonekana kuwa kama muujiza, wakati mwingine wote walionekana kuwa kama wapo ndotoni ambapo baada ya muda kidogo wangeamshwa na alamu za simu zao kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao nyingine za kila siku.

“Hivi ni wewe Rose?” Joshua alimuuliza Rose akiwa amemtoa kifuani mwake, akawabaki akimwangalia.

“Ni mimi. Ni mimi Joshua” Rose alimwambia Joshua na kisha kukumbatiana tena.

Siku hiyo ikaonekana kuwa furaha kubwa katika maisha yao, hakukuonekana kuwa na mtu ambaye aliamini kile ambacho kilikuwa kimetokea mahali hapo, kwao, bado ilionekana kuwa kama ndoto moja kubwa ambayo ingewasisimua katika maisha yao yote.

“Mtoto…” Joshua alisema na kisha kumwachia Rose.

Macho yake yakatua usoni mwa Lydia ambaye alikuwa amesimama pembeni kabisa ya miguu ya mama yake huku ane akiangalia kile ambacho kilikuwa kikitokea. Hakujua sababu ambayo ilimpelekea mama yake kukumbatiana na mwanamume ambaye hakuwa akimfahamu kabisa. Joshua akachuchumaa na kisha kumwangalia Lydia usoni.

“Malkia wangu” Joshua alimwambia Lydia huku akimwangalia, machozi yalikuwa yakiendelea kumtoka, akashindwa kuvumilia, akajikuta akimkumbatia Lydia ambaye akaanza kulia huku akitaka aachiwe kutoka katika mikono ya baba yake, Joshua.

 

Leave A Reply