Kartra

Kahata Aigomea Simba, Akwea Pipa Arudi Kwao

IMEELEZWA kuwa kiungo mchezeshaji wa Simba raia wa Kenya, Francis Kahata ameshindwa kufikia muafaka mzuri na timu yake katika dau la usajili huku fasta akikwea pipa kurejea nyumbani kwao nchini Kenya.

 

Kiungo huyo juzi rasmi alimaliza mkataba wake wa miaka miwili ya kukipiga Simba aliyojiunga nayo msimu wa 2019/2020 akitokea Gor Mahia ya nchini Kenya kama mchezaji huru.

 

Nyota huyo hivi karibuni jina lake lilikatwa katika usajili wa Ligi Kuu Bara na nafasi yake kuchukuliwa na Mzimbabwe Perfect Chikwende aliyejiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo msimu huu.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Simba imeshindwa kufikia muafaka mzuri wa kumuongezea mkataba baada ya kushindwana katika maslahi kwenye pande hizo mbili.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa uongozi wa Simba ulimpa mkataba aliotakiwa kusaini bure huku wakiboresha mshahara wake wa kila mwezi pekee, kitendo ambacho amekikataa kiungo huyo kabla ya juzi jioni kukwea pipa kurejea kwao.

Aliongeza kuwa upo uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kutorejea tena kukipiga katika timu hiyo msimu ujao baada ya kushindwa kufikia muafaka mzuri.

“Kahata kaondoka tangu jana (juzi) jioni baada ya kushindwa kufikia muafaka mzuri na viongozi wa Simba kutokana na kukataa ofa aliyowekewa mezani.“Kikubwa viongozi wa Simba walitaka kumpa mkataba wa miaka miwili bila ya dau la usajili huku wakimboreshea sehemu ya mshahara wake, kitendo hicho amekikataa na kupanda ndege kurudi kwao,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mkuu wa Mahudhui wa Simba, Ally Shatry kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Sina uhakika sana hilo la kurejea nyumbani kwao Kenya.

 

“Kama amerejea kwao, basi yatakuwepo makubaliano kati ya kocha Gomes (Didier) na mchezaji mwenyewe, kwani kama unavyofahamu mchezaji huyo jina lake liliondolewa katika usajili wa ligi na badala yake kuweka katika michuano ya kimataifa.

 

“Hivyo, huenda kocha kamruhusu kurejea kwao kwa ajili ya mapumziko kwani hivi sasa hatushiriki michuano ya kimataifa, tumebakiwa na ligi na FA pekee na yeye hatumiki, kuhusiana na kuachwa sijapata taarifa rasmi kwa viongozi wangu wa juu,” alisema Shatry.

STORI: MUSA MATEJA NA WILBERT MOLANDI


Toa comment