The House of Favourite Newspapers

KAJALA ANAVYOKOSEA KUMGEUZA PAULA SHOSTI YAKE !

KUFAULU mtihani wa kidato cha nne kwa mtoto wa muigizaji maarufu Bongo, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ Sonia George aliyepata Division One, kumeibua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wengi walimpongeza lakini wapo washakunaku waliotaka kujua matokeo ya mtoto wa muigizaji Kajala Masanja, Paula.  

 

Wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018 walikuwa ni wengi sana, lakini cha kushangaza mara tu baada ya matokeo kutangazwa, wadau huko mitandaoni wamekuwa na shauku sana ya kujua Sonia na Paula wamepata nini?

 

Nikajiuliza kwamba, hivi ni watoto hao wawili tu waliofanya mtihani ambao ni wa mastaa? Na je, ni kwa nini watu wamekuwa na shauku ya kujua walichovuna wao na si wengine? Jibu likawa ni kwamba, maisha waliyokuwa wakiishi watoto hawa yalikuwa ya kistaa kutokana na ustaa wa wazazi wao.

Ikumbukwe kwamba, Sonia mama yake ni Monalisa na baba yake ni marehemu George Otieno ‘Tyson’ huku Paula akiwa ni zao la mastaa Paul Matthysse ‘P- Funk’ na Kajala. Kwa maana nyingine watoto hawa walikuwa ni mastaa pia na ndio maana walikuwa wakifuatiliwa sana.

Yapo mambo ambayo akifanya mtu wa kawaida wala haiwezi kuwa ni habari lakini akifanya  staa ni habari. Kwa mfano, staa akinaswa anakula ugali kwa kulumangia ni habari lakini jiulize ni wangapi ambao wanakula chakula hicho huko mtaani? Pia mtu wa kawaida anaweza kuonwa anajisaidia hadharani na isiwe ishu lakini leo hii Diamond akinaswa anajisaidia kichakani inakuwa habari kubwa tu.

 

Ndiyo maana kwenye hili la watoto wa mastaa, unaweza kushangaa kuna watoto wengi tu huko mtaani wamepata ‘division ziro’ kwenye mtihani huo wa kidato cha nne lakini wala hawawezi kuandikwa kwenye vyombo vya habari. Sasa jiulize leo Sonia angepata division mbaya ingekuwaje?

 

Bahati nzuri amefaulu na amekuwa akisemwa vizuri yeye pamoja na mama yake huko mtandaoni. Swali ambalo wengi sasa wanajiuliza ni kwamba, Paula kapata nini? Nilichosikia ni kwamba kapata division four ila sina uhakika na hilo.

Sasa tukiachana na hilo, katika siku za hivi karibuni nimekuwa mtembeleaji mzuri sana wa ukurasa wa Instagram wa Kajala. Kule mara nyingi sana nakutana na mapichapicha ya staa huyo akiwa na mwanaye Paula. Yaani wako happy, wanaonesha jinsi wanavyopendana.

Kwenye moja ya picha za Kajala aliandika; She’s not my baby anymore, she’s my bestfriend. (Siyo mwanangu tena, ni shosti wangu). Maneno hayo yanamaanisha kwamba, sasa hivi wao siyo mtu na mama yake, ni marafiki walioshibana. Sasa mtu anapokuambia flani ni rafiki yake unapata picha gani? Ni kwamba watu hao wanaweza kuazimana nguo, kwenda out pamoja na vitu vingine ambavyo marafiki wanafanyiana.

 

Lakini, unadhani ni sahihi Kajala kumchukulia Paula kama shosti wake hasa kwa ulimwengu wa sasa? Nauliza hivyo kwa sababu kwa mabinti zetu hawa ukiwaacha kuwafanya ni watoto, unaweza kushangaa wanafanya mambo ya kikubwa kama wanayofanya wazazi wao. Ikifikia hatua hiyo itakuwaje?

Sikatai staa kumgeuza mwanaye rafiki lakini urafiki huo uwe wa maneno tu kuonesha   jinsi mnavyopendana lakini katika uhalisia, Paula anatakiwa kubaki kuwa mtoto kwa mama yake ili aendelee kuonywa, kuelekezwa na kunyooshwa pale ambapo atapinda.

 

Kajala akimfanya Paula ni shosti wake, kuna wakati anaweza kumkuta kavaa nguo za ajabuajabu na akashindwa kumwambia au akamkuta anakunwya pombe akamkaushia, kwa nini? Kwa sababu kama wewe unakunywa pombe, huwezi kumzuia rafiki yako asinywe. Kama uvaaji wako ni wa kihasara, huwezi kumsema mwenzako ambaye naye anapenda kuvaa hivyo.

Kwa maana nyingine ni kwamba, kwa kuwa bado Paula anahitaji kuwa chini ya uangalizi wa Kajala, hawahitaji kuwa marafiki bali

wabaki kuwa mtu na mama yake. Ukimuangalia Paula, unaona kama amejanjaruka, tayari ameshautamani ustaa kiasi kwamba mama yake asipokuwa makini naye utashangaa kumuona tayari ni video queen kwenye nyimbo za wasanii au unaweza kumuona naye ameingia kwenye Bongo Fleva. Hii inawezekana kabisa kama hatapata mtu wa kumnyoosha kwenye njia iliyonyooka.

Ushauri wangu ni kwamba, kwa kuwa bado ni mtoto, bila kujali matokeo yake yamekuwaje, ajikite kwenye kusaka elimu. Kama anauhitaji ustaa, atakuja kukutana nao baadaye lakini sasa hivi asome kwanza.

 

Afuate nyendo za dada yake, Hanifa Daudi ‘Jennifer’, yule binti ambaye aliwika sana kwenye filamu alipokuwa akiigiza na marehemu Steven Kanumba. Binti huyo angetaka ustaa, leo hii angekuwa ameshaigiza filamu kibao kwa kuwa kipaji anacho lakini aliamua kuweka mambo ya sanaa pembeni, sasa hivi anapiga shule.

Ndicho anachotakiwa kufanya Paula na atafanikisha hili kwa msaada wa mama yake ambaye ndiye anatakiwa kumueleka njia sahihi za kupita akiwa kama mama yake na siyo shosti wake.

Comments are closed.