The House of Favourite Newspapers

KAJALA; KUCHEZA NA MWANAO SAWA, ILA TIMING YAKO SIYO NZURI

KWAKO, Staa wa filamu za Kibongo, Kajala Masanja. Naamini upo poa kabisa, unaendelea kupambania maisha. Kwa upande wangu hapa mjengoni, ni mzima wa afya njema.

Nimerudi tena kwako Kajala, baada ya kukuandikia barua wiki tatu zilizopita, nikikufariji na kukushauri kuhusiana na matokeo ya mwanao Paula aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana.

 

Ni kweli hali haikuwa nzuri mitandaoni, ambapo watu walikuwa na maoni tofauti kutokana na matokeo hayo, huku wengi wakikushutumu kuwa wewe ni chanzo cha Paula kufeli. Sikuwa upande wao, hata sasa sipo upande wao, lakini umenifanya kwa upande fulani nitilie shaka namna unavyomlea mwanao.

 

Paula, wewe ni staa. Lakini ni mama, ambaye unapaswa kuandaa maisha ya baadaye ya mtoto wako. Maisha ya binadamu huandaliwa kwa kujazwa maarifa. Unatakiwa kuhakikisha mtoto wako anakuwa na maarifa ya kutosha.

 

Chanzo cha kwanza cha maarifa ni elimu. Ndiyo maana hata kwenye kitabu kitakatifu Biblia, kuna mstari umeandikwa: “Mshike sana elimu, usimwache aende zake, maana yeye ni uzima wako.” Ndiyo ukweli ulivyo.

Lakini kile kinachoonekana kwenye clip iliyosambaa mitandaoni ukikata mauno na mwanao, kinapunguza ile dhana ya kujaza maarifa kwa mtoto, badala yake unamjaza vitu visivyofaa.

 

Kabla sijaenda mbele zaidi, nikueleze tu kuwa hakuna kosa lolote kwa mama kucheza na kufurahi na mwanaye… ni mambo ya kawaida kabisa. Lazima mzazi kupata muda wa kufurahi na mtoto, lakini je, wanafurahia vitu gani?

Nakumbuka katika kipindi cha sekeseke kuhusu matokeo ya mwanao, mwandishi Amrani Kaima alipata kuandika makala katika gazeti la Uwazi, akikosoa namna unavyoishi na Paula kama shoga yako, badala ya mwanao.

 

Awali sikumwelewa vizuri Amrani, lakini niliposoma makala yake mpaka mwisho, akitoa mifano kadhaa, nikaona ukweli wa hoja yake, lakini sasa imekuja kudhihirika baada ya kusambaa kwa clip hiyo.

Pengine linaweza lisije jambo baya, ila watu watakuuliza; kwa nini ulirekodi?

Unaweza ukajibu kirahisi tu, kwamba umerekodi kwa faida yako mwenyewe na labda ulitaka kuja kuitazama baadaye, swali litakalofuata litakuwa, kwa nini uliisambaza mitandaoni?

 

Kajala, nakukumbusha wewe ni staa na una kazi kubwa ya kulinda ustaa wako, lakini hakikisha ustaa wako hauharibu future ya mtoto wako. Kuna mambo ya kumsitiri mtoto. Katika kipindi kama hiki ambacho gumzo ni matokeo yake haikupaswa kusambaa video ya namna ile.

Hiyo inatafsiri kuwa ni kweli huzingatii namna bora ya kumlea mwanao. Lazima ujitofautishe wewe na mwanao; wewe ni maarufu na kuonekana kwenye mitandao ni jambo la kawaida, usimwache mwanao naye azagae mitandaoni.

 

Ok! Unaweza kupiga naye picha ‘decent’ labda ya kumtakia heri kwenye jambo fulani au matembezini, ni kawaida kwa mzazi na mwana. Lakini siyo kama vile. Umewafanya watu wapate cha kuongea na kiukweli wataongea sana. Utawazuia vipi wakati mwenyewe umewafikishia?

Jitafakari upya Kajala, lakini kwangu mimi naamini unayo nafasi kubwa bado ya kurekebisha hayo madoa na ukaendelea kuwa mama bora. Paula anakutegemea sana kwa maisha yake ya baadaye. Wewe ndiye wa kumpa mwanga na njia za kupita ili kufikia maisha mazuri.

 

Usimpeleke mwanao kwa jamii ya mitandao ya kijamii ambayo hujipa mamlaka ya kufuatilia kama ndiyo wazazi wake. Ukifuatilia utagundua kuwa wanafuatilia kwa sababu mweyewe uliwapelekea mwanao. Vipi kama ungetunza faragha yenu? Nakushauri angalia namna mpya ya kuishi na mwanao ukionyesha kuwa wewe ni mzazi na siyo rafiki tu!

 

Nakutakia mema.

Yuleyule, Mkweli daima,

……………………

Joseph Shaluwa

Maoni & Ushauri

+255 718 400 146

 

KUTOKA MSIBANI – “Godzilla Alinifukuza Sitamsahau”

Comments are closed.