The House of Favourite Newspapers

Kajala umri unasogea, tulizana sasa!

0

KWAKO muigizaji wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja. Bila shaka uko poa na unaendelea na shughuli zako za kila siku. Vipi mwanao Paula naye hajambo? Baba yake je?

Ukitaka kujua afya yangu, mimi namshukuru Mungu. Naendelea kupambana na kazi zangu za kila siku ili kuhakikisha tonge linakwenda kinywani.

Dhumuni la kukuandikia barua hii ni kutaka kukukumbusha kwamba unapaswa kufanya vitu sahihi katika muda muafaka. Mwishoni mwa wiki iliyopita niliona habari katika moja ya magazeti Pendwa ikionesha kwamba una uhusiano na staa wa Bongo Fleva, Abbott Charles ‘Quick Rocka’.

Uzuri mimi sikuwa mgeni sana wa habari hiyo maana nimeshatonywa mara kwa mara kuwa unaonekana nyumbani kwa msanii huyo maeneo ya Sinza jijini Dar. Ni jambo jema, mapenzi ni kikohozi, kuficha huwezi.

Nimepewa taarifa za jinsi ambavyo mnajiachia bila kificho. Mnaonekana mmeelewana kwelikweli.

Kilichonishangaza, licha ya mwanaume huyo kuonekana kukolea hadi kukuchora mwilini mwake, bado umemkana katika vyombo vya habari kuonesha kwamba hakuna mapenzi kati yenu.

Sitaki kukulazimisha ukubali lakini mazingira mnayoonekana, hakuna kificho, yanaashiria kabisa nyinyi ni wapenzi.

Kuficha kwako si kubaya lakini najaribu kujiuliza utaficha penzi hadi lini? Faida za kuficha ni nini? Umri unazidi kusonga mbele, haurudi nyuma kwa nini usiamue moja? Kwa nini usitulizane na kujenga maisha ya kweli kama kweli unampenda Quick Rocka?

Kama si huyo kuna mwingine, si vibaya pia ukaamua moja. Muanike hadharani na yeye atambue kwamba hakuna mwingine zaidi yake.

Wewe ni mama sasa hivi wa mtoto mkubwa tu, Paula. Haipendezi kuendelea kurukaruka. Haipendezi kutokuwa na msimamo.

Mwanao anapaswa kukuona wewe kama mfano. Kuishi kwa kufichaficha uhusiano kunaleta tafsiri mbaya katika jamii. Kwamba huenda huna mmoja, ndiyo maana unaamua kuficha ili ulionao wasije wakajijua kwamba wapo wengi.

Juzikati nimeona umepangisha nyumba nzuri, una kampuni yako, ni vyema sasa ukaheshimu umri wako na kuandaa maisha mazuri ya baadaye. Kumfundisha mwanao Paula kwamba maisha ni nini na anapaswa kuishi vipi ili na yeye aje kuwa mama wa familia hapo baadaye.

Yale mambo ya kujirusha, kwenda katika kumbi mbalimbali za starehe sasa kidogo upunguze au usiyape nafasi kabisa.

Waachie wale wanaochipukia na wao wafanye hayo ili baadaye nao waje kushtuka na kutengeneza maisha. Naamini maisha yako yamepitia changamoto nyingi, huu si muda mzuri sana wa kukukumbusha lakini itoshe tu kukwambia, tulia!

Ni matumaini yangu kwamba wewe ni muelewa, utayafanyia kazi mawazo yangu na Mungu akubariki, tuone mabadiliko ya kweli.

Mimi nduguyo katika kazi,

Erick Evarist

Leave A Reply