The House of Favourite Newspapers

Kajala, Wema wazichapa Klabu

0

wema3.jpgStori: Musa Mateja na Imelda Mtema
Piga nikupige! Mastaa wenye taito kubwa kunako tasnia ya filamu Bongo, Kajala Masanja ‘Kay’ (Pichani) na Wema Isaac Sepetu wanadaiwa kuzichapa laivu ndani ya klabu.

Tukio hilo la aina yake lilijiri usiku mnene wa kuamkia Novemba 16, mwaka huu ndani ya Klabu ya Escape One Mikocheni jijini Dar ambapo wawili hao walikuwa wamekwenda kutafuna bata lakini makamuzi hayo yalienda tofauti na dhamira za wacheza sinema hao na wengine baada ya kukumbana na zahama hiyo.

WEMA AANZA
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, mastaa hao walijikuta wakitifuana muda mfupi tu baada ya kukutana uso kwa macho ambapo ilisemekana kwamba Wema ndiye alianza kuzua timbwili.

WEMA ATINGA
Ilidaiwa kwamba, Wema alikuwa wa kwanza kuingia ukumbini hapo kabla ya Kajala kisha alikaa sehemu yake akiwa na ndugu, jamaa na marafiki zake ambao alikuwa akijiachia nao.

“Wema alikuwa ameongozana na dada yake, Nuru, Bite, Petit Man na warembo wengine wawili.“Wakiwa ukumbini humo walikuwa wakigongesha glasi za vinywaji huku wakiburudika kwa muziki mzuri uliyokuwa ukidondoshwa na Sky-light (band).

“Muda si muda, ghafla Wema alinyanyuka alipokuwa amekaa kisha kwenda jukwaani kumtunza kiasi cha zaidi ya shilingi elfu 50, mmoja wa waimbaji aitwaye Sam Machozi.
“Ishu hiyo aliifanya kwa mbwembwe huku akicheza na Sam Machozi akimrusha kwa maneno ya mbwembwe ya kummwagia sifa.

kajala.jpgKAJALA NAYE
“Dakika 20 baadaye, Kajala naye alitinga na timu yake ambapo walifika na kuketi jirani na walipokuwa akina Wema.

“Kama kawaida nao waliagiza vinywaji na kuanza kujimiminia huku mara kadhaa kila upande ukiteta mambo yake na kuachia vicheko vya kishambenga na kugongesha viganja.

“Wakati hayo yakiendelea na muziki kunoga, ghafla dada wa Wema (Nuru) alisikika akitukana mtu,” kilitiririka chanzo hicho na kuongeza:
“Kwa upande wake Kajala, naye alikwenda jukwaani kumtunza Sam Machozi. Kwa harakaharaka alimmwagia zaidi ya shilingi laki nne.

“Wakati Kay (Kajala) anafanya mbwembwe, meza ya akina Wema ikawa inamzomea.
“Kama hiyo haitoshi, wakati Kajala anarudi mezani, alipofika usawa wa meza ya akina Wema ndipo mtiti ulipoanzia.
“Unaambiwa Wema alimmwagia pombe Kajala kwa kutumia glasi. Hata hivyo, Kajala hakutaka shida, akachukua leso na kujifuta.

TIMBWILI LAZUA TAHARUKI!
“Wakati Kajala akijifuta, Wema alimrushia glasi iliyokuwa na pombe ambapo Kajala aliidaka na kuirudisha kwa kumrushia Wema lakini bahati mbaya ilimpiga kifuani mdogo wake Wema aitwaye Bite.

“Hapo ndipo timbwili lilipotibuka na kuzua taharuki kwani meza ya akina Kajala walisogea upande wa akina Wema huku watu wakiwahi kuwatuliza lakini tayari walikuwa wameshapeana kavukavu.”

Ilielezwa kwamba, sakata hilo lilinoga baada ya kuanza kurushiana makopo na chupa hadi mabaunsa walipoingilia kati na kutuliza ghasia huku burudani ikisimama kwa muda na watu kupigwa na butwaa na wawili hao kukatazwa kufika ukumbini hapo.

AMANI MZIGONI
Baada ya kunyetishiwa habari hiyo, gazeti hili lilimtafuta Kajala ambaye alipopatikana na kuulizwa juu ya timbwili hilo, alianza kwa kushangazwa na watu kwa kujiropokea mambo ambayo hawayajui na kuongea maneno ambayo hayakutokea.

KAJALA ASHINDWA KUJIZUIA
Kajala alisema kuwa, siku zote amekuwa akijiepusha kugombana na Wema au ndugu yake yeyote, kwani hata siku hiyo alijizuia vya kutosha lakini kama binadamu uzalendo ulimshinda hasa alipoona anashambuliwa kwa chupa.

“Sijawahi kuwaza kuna siku nitapigana na Wema au ndugu yake yeyote, hivyo hata hilo tukio nilijikuta namrudishia chupa baada ya kunimwagia pombe na sikujali hilo lakini akaona haitoshi akanirushia chupa ambayo nisingejikinga kwa mikono, leo ningekuwa na jeraha kubwa usoni,” alisema Kajala.

HADI KWA WEMA
Baada ya kumsikia Kajala, gazeti hili lilifunga safari hadi nyumbani kwa Wema, Kijitonyama jijini Dar lakini hakuwepo nyumbani na muda wote simu yake iliita bila kupokelewa.

Wanahabari wetu walifika eneo la tukio katika Ukumbi wa Escape One ili kujiridhisha kama kweli tukio hilo lilitokea mahali hapo walizungumza na mmoja wa wahudumu wa ukumbi huo aliyekiri kutokea kwa mtiti huo.

Hii si mara ya kwanza kwa Wema na Kajala kuzichapa laivu, mwaka juzi katika ukumbi wa burudani wa Maisha Club (sasa Maisha Basement) waliwahi kuzichapa laivu na kuamuliwa na watu.

Leave A Reply