The House of Favourite Newspapers

Kakolanya ampeleka straika Simba

UNAMKUMBUKA yule straika aliyewapiga chenga mabeki wote wa Yanga pamoja na kipa wao matata, Beno Kakolanya kabla hajafunga? Kama umemsahau basi huyo ni Vita lis Mayanga wa Ndanda FC. Simba wamemsajili mchezaji huyo kutokana na umahiri wake alioonyesha kwenye goli la Kakolanya pamoja na mengine.

 

Straika huyo alimfunga Kakolanya katika pambano kati ya Yanga na Ndanda FC lililopigwa Uwanja wa Taifa Novemba 4, mwaka jana na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Mayanga ‘amesinya’ mkataba na Simba na msimu ujao mapema kabisa atavaa uzi mwekundu pale Msimbazi lakini klabu hiyo inaruhusiwa kumuongeza kwenye mechi za kimataifa inazoendelea nazo kwa sasa akiwa bado na Ndanda.

 

Yaani kwa lugha ya mtaani wanasema analala Mtwara anacheza Dar. Vitalis amejifunga mkataba wa mwaka mmoja na nusu na vigogo hao wa Simba ambao wenyewe wamemuacha kwanza amalize msimu huu wa 2018/19 akiwa na klabu yake ya Ndanda kabla ya kumchukua msimu ujao. Usajili wa mshambuliaji huyo umefanywa siri na Simba lakini Spoti Xtra, limepata taarifa kwamba Mayanga amesaini mwaka na nusu.

Spoti Xtra, lilimpata Mayanga mwenyewe ambapo alisema: “Kwa sasa niko Shinyanga na klabu yangu ya Ndanda FC tukiwa tunajiandaa na mechi na Stand United.” “Ni kweli nimesaini mkataba na Simba, nimesaini mwaka mmoja na nusu na klabu hiyo lakini kwa sasa bado niko Ndanda FC. “Mambo mengine siwezi kuyazungumzia kwa sasa, ila jua nimesaini Simba basi,” alisema Mayanga.

 

Spoti Xtra, lilimtafuta Katibu wa Simba, Dk Anord Kashembe alijibu kwa ufupi tu “amesajiliwa” bila ya kuongeza neno lingine. Hadi anatua Simba, straika huyo ambaye amewahi kuichezea Stand United ya Shinyanga amefunga jumla ya mabao saba sawa na washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi. Mabao hayo ya Mayanga amezifunga timu za Ruvu Shooting (moja), Mtibwa Sugar (mawili), Singida United (moja), Biashara (moja), African Lyon (moja) na JKT Tanzania (moja).

MARTHA MBOMA NA SAID ALLY

Comments are closed.