The House of Favourite Newspapers

Kakolanya amtibulia kipa Mkongo Yanga SC

KIWANGO kikubwa kilichoonyeshwa na kipa wa Yanga, Benno Kakolanya ni kama kimemtibulia kipa mpya Mkongoman, Klaus Kindoki baada ya wachezaji nyota wa timu hiyo kummwagia sifa kipa huyo.

Kakolanya katika mechi mbili za hivi karibuni, ikiwemo ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger na ile ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, alionyesha kiwango kikubwa.

Kiwango cha kipa huyo kilimsababishia mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuf Manji kushindwa kujizuia na kummwagia sifa kipa huyo baada ya kuokoa michomo katika mchezo wa USM Alger.

Akizungumza na Championi Jumatatu, kiungo wa timu hiyo, Papy Kabamba Tshishimbi, alisema kuwa pongezi nyingi ziende kwa Kakolanya katika michezo hiyo miwili waliyocheza ambayo ushindi wao umetokana na mchango wake.

“Ipo wazi kabisa, Kakolanya amecheza vizuri katika michezo hii miwili tuliyocheza ukianzia huu tuliocheza wa ligi na ule wa kimataifa dhidi ya USM Alger,” alisema Tshishimbi.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Mkongoman, Heritier Makambo, alisema: “Pongezi nyingi ziende kwa Kakolanya katika mechi hii na Mtibwa, kwani licha ya sisi kutimiza wajibu wetu wa kufunga mabao, lakini yeye alitimiza wake wa kuokoa mabao katika goli letu.

“Pia, pongezi nyingine ziende kwa mabeki wetu Yondani (Kelvin) na Dante (Andrew Vincent) kwa kufanikiwa kuokoa na kupunguza mashambulizi golini kwetu,” alisema Makambo.

Naye kiungo kiraka Said Makapu alisema: “Mungu ambariki Kakolanya, kiukweli Kakolanya kafanya kazi nzuri katika mechi hii ya Mtibwa Sugar na matokeo yetu ya ushindi yametokana na yeye.”

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.