Kakolanya Atuma Ujumbe Muhimu Yanga

Benno Kakolanya

KIPA wa Yanga, Benno Kakolanya amewatumia salamu wenzake kwenye kikosi chake huku akiwataka wazidi kupambana ili kulinda nafasi wanayoishikilia kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Kakolanya ametoa kauli hiyo wakati hivi sasa Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 50 ikifuatiwa na Azam FC yenye 40, huku Simba ikiwa na pointi 33. Kakolanya ambaye hivi karibuni aliingia kwenye mgogoro na kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo, kwa sasa yupo nje ya kikosi hicho kutokana na kusimamishwa na kocha huyo.

 

Akizungumza katika kipindi cha Spoti House kinachorushwa na runinga ya mtandaoni ya Global TV kila Alhamisi, Kakolanya alianza kwa kuwapongeza wenzake kwa kuonyesha moyo wa kupambana kila wanaposhuka uwanjani, kisha akawaomba waongeze juhudi zaidi kwenye mechi zilizosalia ili waweze kuwa mabingwa wa ligi hiyo msimu huu.

 

“Nawapongeza wachezaji wenzangu wa Yanga kwa kuonyesha kupambana kusaka ushindi kwenye kila mechi, ninachowaomba waongeze juhudi zaidi kwa kuwa mechi bado nyingi, hivyo wasibwete kwa kuwa tunaongoza ligi kwa sasa.

 

“Kwa upande wangu, ninaamini Mungu atanisaidia na matatizo yangu na klabu yatakwisha na nitarejea kuungana na kikosi changu hivi karibuni kuendelea kukipambania ili tuchukue ubingwa msimu huu,” alisema Kakolanya. Kutazama mahojiano zaidi ya Kakolanya tembelea YouTube kisha ingia katika chaneli ya Global TV Online utashuhudia mahojiano yote kwa urefu.

Loading...

Toa comment