The House of Favourite Newspapers

KAMA MBABAISHAJI KWANINI, UNG’ANG’ANIE PENZI LAKE

Related image

ASSALAM alaikum mpenzi msomaji wangu wa safu hii. Ni matumaini yangu kwamba kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku.  

 

Mpenzi msomaji wangu, asilimia kubwa ya watu wako katika ulingo wa mapenzi. Wapo walio katika ndoa, wapo walio katika uchumba na kuna wale wenzangu na mimi ambao bado wapo katika hatua ile ya urafiki wa kawaida.

 

Niliodhamiria kuwazungumzia wiki hii ni wale walio na wapenzi wababaishaji ambao wapo katika penzi lisilokuwa na nyuma wala mbele. Yaani mtu anakuwa na mpenzi wake kwa muda mrefu lakini hawana malengo yoyote zaidi ya kuliendesha penzi kisanii huku siku zikisogea.

 

Huwa najiuliza, ni kupendana kwa aina gani huko ambako watu wanakaa kwa muda mrefu lakini hata siku moja hawajawahi kuzungumzia suala la kuja kuishi pamoja kama mke na mume?

 

Inaniuma sana pale ninapowaona baadhi ya wasichana wakizinguliwa na wapenzi wao, yaani hawana sauti ya kuhoji juu ya hatma ya maisha yao, hali inayoashiria kuwa, hawako na watu sahihi. Sasa kwa nini wewe msichana usiwe na msimamo na maisha yako? Kwa nini ukubali kuburuzwa wakati wewe pia una haki ya kujua mustakabali wa maisha yako ya baadae? Au hutaki kuipata ile heshima ya kuwa mke wa fulani?

 

Mimi nadhani ni vyema ukamweleza kabisa huyo mpenzi wako kwamba, sawa kakupenda lakini huu sio wakati wa kuchezeana na kuachana, ana malengo gani ya baadaye na wewe? Ukiona anajiumauma na kutokupa majibu ya msingi, huna sababu ya kuendelea kuwa naye bali muache na uangalie utaratibu mwingine.

 

Tatizo walilonalo wasichana wengi ni kushindwa kujizuia pale mmoja anapotokea kumzimia mwanaume fulani, yaani anakuwa hasikii la kuambiwa na yuko tayari kwa lolote kiasi cha kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yake.

Related image

Sidhani kama una sababu ya kujishusha kiasi hicho, wewe ni mwanamke unayestahili kuwa na mwanaume ambaye baada ya kipindi flani atasema maneno haya: “Nimekuwa na wewe kwa muda mrefu, nimekusoma tabia zako na nimegundua kuwa una kila kigezo cha kuwa mke wangu wa maisha.”

 

Akishakutamkia maneno hayo, unakuwa na nguvu sasa ya kumpenda zaidi, kumthamini na kumfanyia kila kitu ambacho kitamfanya aamini kuwa amempata mwenza wa kweli. Kwa kufanya hivyo naamini penzi lenu litadumu na kujikuta mnatimiza ndoto zenu. Mpenzi msomaji wangu, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kujilaumu kwa nini wamewapenda walionao sasa.

 

Wapo ambao wamepoteza maisha yao kwa sababu tu ya mapenzi, wapo waliochanganyikiwa, kuathirika kisaikolojia na wengine kuachishwa kazi kwa sababu tu ya mapenzi. Kimsingi mapenzi ni hatari sana hasa pale unapojikuta umedondokea sehemu ambayo hukustahili. Lakini sasa, licha ya mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu bado tunaambiwa kwamba, utakuwa peke yako kwa muda flani tu wa maisha yako lakini mwishowe utalazimika kutafuta mwenza ambaye utaishi naye katika maisha ya mume na mke.

 

Suala kujiuliza ni kwamba, kama huyo unayempenda haonyeshi dalili za kuja kukuoa, kuna ulazima wa kuendelea kung’ang’ania penzi lake? Mimi nasema, hakuna ulazima wa kuendelea kuwa naye bali unatakiwa kumuacha na kuangalia maisha yako. Kamwe usikubali kuwa mtumwa wa mapenzi. Usikubali kulia kila siku kisa mwanaume.

 

Nalazimika kusema hivyo kwa sababu, mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba ukifanya uchunguzi wa haraka haraka utabaini kuwa, wengi wanachezeana tu. Si ajabu huyo uliyenaye anaonesha kukupenda ile mbaya lakini amini usiamini inawezekana ni gelesha tu na wala hana penzi la dhati moyoni mwake dhidi yako.

 

Ndio maana inashauriwa kuwa unapotokea kumpenda mtu fulani na yeye akakutamkia kwamba anakupenda, kuwa na imani kwamba ana penzi la dhati kwako kisha endelea kufanya utafiti katika kila analolifanya. Kama wewe ni mjanja utabaini tu kama umepata au umepatikana.

Ni hayo tu kwa leo, tuonane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.

Comments are closed.