The House of Favourite Newspapers

KAMATI YA BUNGE YAKAGUA MRADI WA UPANUZI  JENGO LA UTAWALA DUCE

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimia na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof James Mdoe wakati alipowasili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE). 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na baadhi ya Viongozi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) wakielekea katika jengo la linalokarabatiwa.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakisikiliza taarifa ya maendeleo ya kazi ya upanuzi na ukarabati wa jengo la utawalakatika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Prof. Joyce Ndalichako na Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamojana viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na T eknolojia wakiwa katika picha ya pamoja.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeiagiza serikali kuhakikisha inafanikisha upatikanaji wa kiasi cha shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati na upanuzi wa jengo la utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

 

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Peter Serukamba Jijini Dar es Salaam baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa jengo hilo ambapo amesema kuchelewa kumalizika kwa wakati kunaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupanda
kwa gharama za vifaa.

 

Mhe. Serukamba amesema kiasi hicho cha fedha ni muhimu kikapatika kwa sasa ambapo kazi ya ujenzi na ukarabati ikiwa inaendelea kwani itasaidia pia kuondoa usumbufu.

 

“Kucheleweshwa kwa fedha zilizobaki zitafanya jengo hili kujengwa kwa gharama kubwa sana kwani vifaa vya ujenzi vinapanda, lakini pia haitakuwa vizuri kumalizia upande mmoja wa jengo watu waingie wafanye kazi baadaye wapishe ujenzi inakuwa ni usumbufu kwa watumishi” amesema Mhe. Serukamba.

 

Aidha, Mhe. Serukamba amekitaka Chuo hicho kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha maktaba ya Chuo hicho inakuwa kamilifu na kupewa kipaumbelea ili kuwa na maktaba inayojitosheleza kwa kuwa na eneo lenye ubora, vitabu vya kutosha ikiwemo vitabu vya electroniki. Vilevile ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuweka utaratibu wa wanafunzi wa DUCE kuweza kutumia maktaba ya kisasa iliyopo katika kampasi yake kuu pamoja na hayo kamati pia imeitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia madai ya watumishi katika Chuo kikuu cha Dar Salaam kwa ujumla na kuhakikisha madai stahiki yanalipwa.

 

Awali Rasi wa Duce, Prof. Bernadeta killian ameielezea Kamati hiyo kuwa mradi huo wa panuzi na ukarabati jengo la utawala unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa ujumla, kiasi ambacho kinajumuisha gharama za ujenzi, ukarabati, kuweka mifumo ya TEHAMA pamoja na samani za ndani za jengo hilo ambapo mpaka sasa bado kiasi cha
shilingi bilioni 1.1 kinahitajika ili kukamilisha. Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea mradi huo na ameahidi kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.

Comments are closed.