The House of Favourite Newspapers

Kambi ya Uturuki yampa jeuri Pluijm, atuma salamu Mazembe

0

pluijm

Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam
WAKIWA wana siku tatu tangu waingie kambini nchini Uturuki, Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm ameifurahia kambi hiyo huku akitamka kuwa hawaoni sababu ya kulikosa taji la Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo, iliondoka nchini alfajiri ya kuamkia Jumapili kuelekea Uturuki ilipokwenda kuweka kambi kwa ajili ya matayarisho ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya MO Bejaia ya Algeria unaotarajiwa kuchezwa Jumapili wiki hii.
Mchezo huo, unatarajiwa kupigwa saa 6:00 usiku kabla ya Yanga kurejea tena Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo itakayochezwa Juni 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema, kila mahitaji muhimu wanayapata kwenye kambi hiyo kwa ajili ya maandalizi yote ya ya mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho ikiwemo uwanja, malazi na chakula kizuri, hivyo haoni sababu ya kuukosa ubingwa huo.
Pluijm alisema, ameelekeza nguvu zake kwenye mchezo ujao dhidi ya MO Bejaia kuhakikisha wanashinda ugenini na tayari amechukua tahadhari mapema ikiwemo kubadili muda wa mazoezi na sasa wanafanya usiku badala ya jioni kwa kuwa anajua mechi itapigwa usiku.
Mholanzi huyo alisema, pia kutokana na hali ya hewa ya Algeria ni baridi hivi sasa, wameona kufanya mazoezi muda huo wa usiku kwa muda wa saa tatu hadi nne nne kwa siku ili kuendana na hali ya hewa ya huko.
Aliongeza kuwa, amefanya kikao na wachezaji wake kwa kuwataka kila mmoja kutimiza majukumu yake ya ndani ya uwanja kuhakikisha wanatimiza malengo yao wakiwemo nyota wapya wanne waliosajiliwa ambao ni Hassani Kessy, Juma Mahadhi, Vincent Andrew ‘Dante’ na Beno Kakolanya.
“Nimechukua tahadhari ya haraka na mapema kabla ya mchezo wetu wa kwanza dhidi ya MO Bejaia, kikubwa nilichofanya ni kubadili muda wa mazoezi tuliyokuwa tunafanya jioni na kuyapeleka usiku saa 6, hiyo ni baada ya kupata taarifa mchezo wetu unachezwa usiku.
“Hiyo ni moja ya tahadhari ili kuzoea mazingira, pia nimebadilisha muda huo kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya baridi baada ya kupata taarifa ya hali ya hewa ya huko.
“Kiukweli ninaifurahia kambi ya huku Uturuki ambayo ninaamini itatupa mafanikio kutokana na mahitaji ya msingi yenye umuhimu kuyapata ambayo ninaamini kama tungekuwepo huko Tanzania tusingeyapata ikiwemo uwanja mzuri, chakula na malazi wanachokipata wachezaji wangu,” alisema Pluijm.

Leave A Reply