The House of Favourite Newspapers

Kampeni ya Kuelimisha Wanafunzi Kutojihusisha na Unywaji wa Pombe Yafika Kilimanjaro

0

Wanafunzi wa shule za sekondari wamehimizwa kujiepusha na unywaji pombe chini ya umri ili kujihakikishia wakati wao shuleni na kulinda afya zao.

Kampeni hii muhimu iitwayo SMASHED iliyoanzishwa katika Shule ya Sekondari ya Msasani katika mapambano dhidi ya unywaji pombe chini ya umri, ipo chini ya Serengeti Breweries Limited.

Programu hii inatumia tasnia ya uigizaji wa maigizo kuangazia suala linalojitokeza kwenye jamii la matumizi ya pombe chini ya umri na athari zake hasi kwa vijana waliopo mashuleni.

Kampeni hii imezinduliwa na Mkuu wa wilaya ya moshi Mheshimiwa Kisare Magori akimwakilisha Mkuu wa Mkoa  wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ambaye alisisitiza azma ya pamoja ya kulinda ustawi na mustakabali wa kizazi cha vijana wa Kitanzania.

Alisema, “ni faraja kuona kampuni ya bia ikipigania dhidi ya unywaji pombe chini ya umri, SBL wanatoa mfano mzuri sana kwa jamii.” Aliendelea kusema, “natumai kwamba tunaweza kujifunza na kushirikiana nao ili kulinda vizazi vyetu vijavyo dhidi ya unywaji pombe chini ya umri.”

Tanzania iko miongoni mwa nchi za Kiafrika ambapo vijana wengi huanza matumizi ya pombe mapema katika umri mdogo.

Utafiti uliofanywa mwaka 2019 katika mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro ulibaini kuwa kiwango cha matumizi ya pombe miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari wenye umri wa miaka 15 na zaidi kilikuwa kati ya asilimia 12.9 kwa wasichana mkoani Mwanza hadi asilimia 63.9 kwa wavulana mkoani Kilimanjaro.

Wakati kiwango cha matumizi ya pombe miongoni mwa wanafunzi wenye umri wa miaka 13–15 huko Dar es Salaam kilikuwa asilimia 5.6%.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo katika shule ya sekondari ya Msasani huko Moshi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi alisema, “SBL inafurahi kusaidia uanzishwaji wa programu ya SMASHED dhidi ya unywaji pombe chini ya umri kwani inaimarisha shughuli za kuhakikisha kwamba bidhaa zetu haziuuzwi au kutumiwa na watu walio chini ya umri wa miaka kumi na nane.”

“Programu hii inahusisha utoaji wa mafunzo muhimu kuhusu athari hasi za kunywa pombe chini ya umri kwa vijana na jamii kwa ujumla.

Programu hii inachanganya matumizi ya maonyesho ya maigizo na ushiriki wa wanafunzi katika mazingira ya kujifunza yanayowapa motisha ili kuwajengea uwezo, ujuzi, na ujasiri wa kufanya maamuzi yenye dhamiri nzuri na kuendelea kuwa na mitazamo chanya ya kujali na kutunza afya zao,” alisema Obinna Anyalebechi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL.

SBL iliandaa programu hiyo miaka miwili iliyopita ikitoa elimu kwa wanafunzi walio chini ya umri katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga ambapo kampuni hiyo iliweza kuwafikia zaidi ya wanafunzi 20,000 katika mikoa hiyo miwili.

Leave A Reply