The House of Favourite Newspapers

Kampuni Binafsi za Ulinzi Zisizofuata Sheria Kukiona

0

Wakati Jeshi la Polisi nchini likianza ukaguzi wa Kampuni binafsi za ulinzi, Wadau wameliomba Jeshi hilo kutoa mafunzo kwa walinzi wa kampuni hizo ili kuwe na mfanano wa utendaji kazi.

Hayo yamejiri leo Novemba 17, 2023 jijini Mwanza wakati wa kikao kazi cha Mkuu wa Usimamizi wa Kampuni binafsi za ulinzi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Ulrich Matei na viongozi wa kampuni binafsi za ulinzi mkoani hapa.

Akiongea na wakurugenzi, wamiliki na wasimamizi wa kampuni binafsi za ulinzi, SACP Matei amesema lengo la kikao hicho ni kukumbushana mambo ya msingi ambayo yanatakiwa kuzingatiwa ili kuboresha tasinia ya ulinzi.

“Natoa pongezi za dhati kwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa kwa kikao alichokifanya wiki mbili zilizopita nilikiona kupitia vyombo vya habari kati ya Jeshi la Polisi na kampuni binafsi za ulinzi kilikuwa kizuri sana” alisema SACP Matei

“Aliweka mikakati ambayo wote tumezingatia ili kukabili changamoto zinazotukuta, hongereni sana” amesisitiza Matei

Kupitia kikao hicho, SACP Matei ametoa rai kwa makamanda wa Polisi nchini kuiga mfano wa Kamanda Mutafungwa na timu yake kwa kufanya vikao na kampuni binafsi za ulinzi.

Aidha, Mkuu huyo wa usimamizi wa kampuni binafsi za ulinzi amezitaka kampuni zisizo na sifa ya kutoa huduma hiyo ya ulinzi kusitisha mara moja mpaka pale zitakapokidhi vigezo.

“Nitoe rai kwa makamanda wote wa Jeshi la Polisi Nchini, kupitia kitengo cha Polisi Jamii watoke ofisini na wasaidizi wao kwenda kwenye maeneo yao ili kupata takwimu sahihi ya kampuni zinazofanya kazi kwenye maeneo yetu na askari wanaolinda pamoja na kumbukumbu zao” amesema Matei

Kwa upande wake, Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Sarige ameahidi kuendeleza usimamizi thabiti kwa kampuni hizo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa kampuni zitakazo shindwa kufuata sheria.

Naye, Eliasi Mgono kutoka Kampuni ya The Dovas Security Mwanza, amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura kwa kuanzisha kitengo cha Polisi Jamii kwani kimelisogeza Jeshi karibu na Jamii.

Kwa upande wake, Samsoni Iyombe ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Magayane Security amesema kuwa, kuna Changamoto ya upungufu wa wahitimu wa Jeshi la akiba (Mgambo) kwani kampuni binafsi za ulinzi ni nyingi lakini watu wenye sifa za kuajiriwa hakuna, hivyo akatumia nafasi hiyo kuomba mamlaka zinazohusika kuwasaidia kuandaa vijana wengi ili kuondoa kero hii.

Hata hivyo, Aman Nasoro Mkurugenzi wa Kampuni binafsi ya ulinzi ya Amaka ameliomba Jeshi la Polisi nchini kuanzisha kitengo cha kutoa elimu kwa walinzi wa kampuni binafsi za ulinzi ili kuwa na watendaji wanaofanana kama askari Polisi walivyo Mikoa yote.

“askari wa Mkoa wa Katavi na wa Mwanza wako sawa kiutendaji lakini askari wa kampuni binafsi za ulinzi hawafanani kiutendaji kutokana na tofauti ya mafunzo wanayoyapata sehemu tofauti” amesema Nasoro

Leave A Reply