The House of Favourite Newspapers

Kampuni Ya Bima Ya Strategis Yapongezwa Kwa Kubuni Na Kuja Na Bima Mpya Ya ‘Makasha’

0
Mkurugenzi wa Uthibiti wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bw. Abubakar Ndwata (katikati) akishuhudia uzinduzi wa bima ya makasha ijulikanayo kama ‘container insurance’ Jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Wengine kutoka kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Strategis Dr. Flora Minja, Afisa Mtendaji Mkuu (bima za mali na majanga) Bw. Jabir Kigoda, Mkuu wa kitengo cha Bima wa NMB Bank, Martin Massawe na Meneja Mwandamizi wa Uhusiano-SMEs wa NMB Bank, Bw. Donatus Richard.

Kampuni ya Bima ya Strategis imepongezwa kwa ubunifu wake wa kuja na huduma mpya ya bima ya makasha ijulikanayo kama ‘container insurance’ kwa lugha ya kigeni. Pongezi hizo zilitolewa wiki hii na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi kutoka mamlaka ya Usimamizi wa Bima ndugu Abubakar Ndwata ambaye alikuwa akimuwakilisha kamishina wa bima Tanzania Dr. Baghayo Saqware katika uzinduzi wa huduma hii mpya ya kipekee hapa nchini.

“Natoa wito kwa makampuni mengine ya bima yaige mfano huu na wabuni bidhaa nyingine ambazo zitakidhi mahitaji ya soko. Na simaanishi waige kwa kutoa huduma kama hii ya bima, bali waje na huduma ambazo zitasaidia kukuza soko na wakati huo huo kutatua changamoto kwa walaji wa bima. Aidha, kwa kupitia huduma hii mpya ya bima, Strategis Insurance imethibitisha kuwa ni kampuni inayoongoza katika soko’’. Alisema mkurugenzi huyo kutoka mamlaka ya bima Tanzania Ndugu Abubakar Ndwata

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Strategis Bw. Jabir Kigoda alisema wanafarijika mno kuwa kampuni ya kwanza ya bima kuanzisha huduma hii ya bima. ‘’Leo kampuni ya bima ya Strategis inaweka historia kwa kuwa kampuni ya kwanza nchini kuzindua aina hii ya bima. Tunaamini huduma hii itawanufaisha sana wafanyabiashara kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wamekuwa wakitakiwa kuweka amana kila ambapo wamekuwa wakitaka kutumia makasha (makontena). Vile vile bima hii itakwenda kusaidia juhudi za kukuza uchumi wa nchi kwasababu sasa wafanyabiashara wataweza kuwekeza fedha zao katika maeneo mengine badala ya kuziweka kama amana’’ Alisema Bwana Kigoda.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyabiashara  waliohudhuria uzinduzi huo wameipongeza kampuni  ya bima ya Strategis kwa kubuni na kuja na suluhisho la   kudumu kwa kile ambacho kilikuwa kinawatatiza kwa miaka yote. Wafanyabiashara hao wanaamini sasa bima hii itakwenda kuwapunguzia gharama za uendeshaji na pia kuwapa nafasi ya kuwekeza pesa zao katika maeneo mengine ili kukuza mitaji na biashara zao.

Wafanyabiashara hao wamedai kwamba kwa sasa wanataka elimu kuhusu bima hiyo mpya ienezwe nchi nzima kwa haraka ili wasafirishaji wengi wa mizigo wanaokodi makasha (makontena) waifahamu na kuitumia ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa.

Bima hiyo mpya ilizinduliwa na kampuni ya bima ya Strategis wakishirikiana na benki ya NMB siku chache zilizopita katika hafla ya aina yake katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa usafirishaji wa mizigo majini na nchi kavu, mamlaka ya meli Tanzania (TASAC),Wafanyakazi toka kampuni ya bima Strategis na NMB.

“Huu ni ubunifu wa hali ya juu na ndicho tulikuwa tunahitaji kama wasafirishaji wa mizigo kwenda au kutoka nchi mbalimbali. Kuna haja kubwa ya ujumbe huu kuwafikia wenzetu kote nchini ili wanufaike nayo. Tumekuwa tunaweka pesa nyingi (amana) ili kuweza kukodi makasha ambayo tunayatumia katika kusafirisha mizigo kwenda kwa wateja wetu” alisema Ulrich Mwinyiechi ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Integer Intra Traders Ltd.

Aliongeza kuwa hii ni zawadi kubwa kwa wasafirisaji kutoka kwa Strategis Insurance na kuwapongeza kwa kuwa wabunifu siku zote kutokana na bidhaa zao zinazokidhi mahitaji ya soko.

Mkurugenzi Mtendaji wa KMJ, Karim Jamal alisema “wasafirishaji wa mizigo wamekuwa wakisubiri bidhaa hiyo kwa muda mrefu na hatimaye kampuni ya bima ya Strategis imesikia kilio chao kwa kubuni suluhisho la kudumu kwa matatizo yaliyokuwa yanawakabili.

“Tumekuwa tukiweka fedha nyingi kama amana (deposit) kwa makasha tunayosafirishia mizigo endapo majanga yoyote yatatokea lakini bima hii mpya sasa itakuwa mkombozi wetu,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Afrika Wakawaka, Sung Tao, alisema hana haja ya kufikiria mara mbili mbili kuhusu bima hiyo mpya  kutokana na gharama kubwa ambazo walikuwa wanaingia kusafirisha makasha ya mizigo.

“Bima hii mpya imekuja muda mwafaka kabisa na tunaishukuru sana kampuni ya bima ya Strategis kwani gharama sasa zitapungua kwa kiasi kikubwa na fedha hizo tunaweza kuwekeza katika shughuli nyingine za kuimarisha uchumi,” alisema.

Kwa upande mwingine, Afisa mtendaji kiongozi wa kampuni ya bima Strategis Dr Flora Minja alisema kuwa ripoti za wachumi zinaelekeza kwamba Uchumi wa nchi yetu unazidi kuimairika na unatarajiwa kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5-6% kwa mwaka.  Mojawapo katika sababu zinazotegemewa kuchangia ukuaji huu ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi/ kanda mbali mbali duniani.  Kwa kuangalia ni sehemu gani ambayo kampuni ingeweza kuchangia ukuaji huu, Strategis, iligundua pengo katika kipengele cha usafirishaji wa bidhaa kwa kontena, ambapo wafanyabiashara walikuwa wanakutana na majanga yanayohusika na usafirishaji wa mizigo yao kwa kontena. Alisisitiza Dr Minja.

Strategis Insurance imekuwa ikitoa huduma za bima  hapa nchini kwa zaidi ya miaka 20 sasa, zikiwemo bima za vyombo vya moto, bima za safari, bima ya usafirishaji wa majini, bima za majanga ya moto, bima za mali, bima za wakandarasi, bima ya afya na nyinginezo nyingi.

Leave A Reply