Kampuni ya Boeing yasitisha matumizi ya ndege zote za 371

 

KAMPUNI ya kutengeneza ndege ya Boeing ya Marekani iliyotengeneza ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka hivi karibuni, imesitisha matumizi ya ndege zote aina hiyo baada ya wachunguzi kubaini ushahidi mpya katika eneo ambako ndege ya Ethiopia Airlines ilianguka.

 

Kampuni hiyo ya Marekani imesema itasitisha usafiri wa ndege zote 371 zinazohudumu. Shirika linalosimamia usafiri wa anga nchini Marekani (FAA), limesema ushahidi mpya pamoja na data mpya za satelaiti zimechangia uamuzi huo wa kupiga marufuku kwa muda usafiri wa ndege hizo.

 

FAA awali lilisisitiza ndege ya Boeing 737 Max 8 ni salama wakati mataifa mengine yakipiga marufuku usafiri wa ndege hizo. Ajali hiyo siku ya Jumapili karibu na jijini Addis Ababa ilisababisha vifo vya watu 157.

 

Ni ajali ya pili kuwahi kushuhudiwa ya ndege hiyo chapa Max 8 katika miezi mitano baada ya ajali nyingine nchini Indonesia mwaka jana Oktoba iliosababisha vifo vya watu 189.

 

FAA lina kundi la maofisa wanaochunguza mkasa huo katika eneo ambapo ajali ya shirika la ndege la Ethiopia ilipotokea likishirikiana na bodi ya kitaifa ya usalama wa safari.

 

Dan Elwell, kaimu msimamizi katika shirika hilo la FAA, amesema Jumatano:   “Imebainika wazi kwa pande zote kwamba safari ya ndege ya Ethiopia ilikaribiana na namna ilivyoshuhudiwa kwa ndege iliyoanguka awali ya Lion Air .”

 

Ameongeza kwamba “ushahidi tuliopata katika eneo, umefanya kuwa na uwezekano mkubwa kwamba hata njia ya ndege ilikaribiana na ile ya Lion Air”.

 

 

Rais Donald Trump awali alitangaza kwamba shirika la FAA litatoa tangazo la dharura kufuatia “taarifa mpya na ushahidi tuliopokea kutoka eneo la mkasa na kutoka maeneo mengine kupitia malalamiko mengine tofauti.”

 

Marekani ni nchi ya hivi karibuni kusitisha usafiri wa ndege hiyo ya Boeing 737 Max yakiwemo mataifa mengine kama Uingereza, Umoja wa Ulaya, China India na Australia ambayo yote yameamua kusitisha usafiri wa ndege hizo.

 

Kufikia leo, msimamo wa FAA ni kwamba ukaguzi umeonyesha “hakuna matatizo ya mfumo wa utendaji kazi” na kwamba hakuna msingi wa kusitisha usafiri wa ndege hizo.

 

Boeing, mtengenezaji wa ndege hizo imesema “inaendelea kuwa na imani kubwa katika usalama wa ndege za 737 Max”.

 

Hata hivyo, limeongeza baada ya mashauriano na FAA na bodi ya taifa ya usalama wa safari kwamba imeamua kupiga marufuku safari za ndege hizo “kutokana na kutambua umuhimu wa tahadhari na katika kutoa hakikisho kwa umma wanaotumia ndege kuhusu usalama wa ndege hizo.”

 

Dennis Muilenburg, rais, mkurugenzi mtendaji na mwenyekiti wa Boeing, amesema: “Tunafanya kila tuwezalo kuelewa chanzo cha ajali hizo na wachunguzi, tutatuma vifaa vya usalama zaidi na kuhakikisha kwamba hili halifanyiki tena.”

 

Sara Nelson, rais wa muungano wa wahudumu wa ndege – CWA, amesema: “Maisha ya watu siku zote ndio muhimu zaidi. Lakini hadhi ya bidhaa kuu ipo hatarini pia. Na bidhaa hiyo si tu Boeing. Ni Marekani.”

 

Hisa za Boeing zimeongezeka hadi kufikia  $377 kila moja kufuatia tangazo hilo. Hata hivyo, thamani ya kampuni hiyo katika soko imeshuka kwa takriban Dola bilioni 26 tangu kutokea mkasa wa ajali hiyo ya ndege ya Ethiopia siku ya Jumapili.

 

Loading...

Toa comment