Kampuni Ya Madini Ya Twiga Yaundwa Kulinda Rasilimali Za Watanzania (Picha +Video)
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli leo Januari 24, 2020 ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation, makubaliano ambayo yameunda Kampuni ya Twiga Minerals Cooperation Limited.
Mazungumzo hayo yaliyoanza tangu mwaka 2017 hatimaye yamefika mwafaka ambapo imeundwa Kampuni ya Madini ya Twiga kwa Serikali ya Tanzania kuwa na hisa asilimia 16 na kwamba faida itakayopatikana katika kampuni hiyo, zitagawanywa asilimia 50 kwa 50 kwa manufaa ya Kampuni husika ya Twiga.
Akizungumza baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Rais Magufuli amesema kuwa hiyo ni hatua kubwa kwa Watanzania baada ya mazungumzo hayo kufika mwafaka kuundwa Kampuni hiyo ya Twiga itakayokuwa na manufaa kwa Wananchi wa Tanzania katika rasilimali zao.
Rais Magufuli amesema huo ni ushindi mkubwa kwa Watanzania kutokana na hapo awali kudanganywa kuhsusu Madini hayo, “Barrick ni Kampuni kubwa duniani kufanya nao mazungumzo sio jambo dogo mwanzo Madini yalipokuwa yanachukuliwa Watanzania tuliamini ni mchanga, tunajiuliza swali kama ni mchanga kwa nini usafirishwe hadi nje ya nchi? baadae tulielewa kwamba ule haukuwa mchanga”, amesema Rais Magufuli.
Mikataba iliyosainiwa
Mikataba iliyosainiwa ni mkataba wa msingi wa makubaliano, menejimenti na utoaji huduma, mkataba wa wanahisa wa kampuni ya Twiga, mkataba wa wanahisa wa North Mara.
Mingine ni mkataba wa wanahisa wa Bulyankuru, mkataba wa wanahisa wa Buzwagi, mkataba wa maendeleo ya mgodi wa North Mara, mkataba wa maendeleo ya mgodi wa Bulyanhulu na mkataba wa maendeleo wa mgodi wa Pangea.
Aidha katika hafla hiyo, Mbutuka iliwasilisha barua ya maombi ya hisa kwa Barrick na Rais wa Barrick Mark Bristow ametoa hati ya mwanahisa kwa Serikali na kumkabidhi Magufuli.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi amesema katika makubaliano hayo Serikali imepewa hisa asilimia 16 ambazo hazibadiliki hata kama Barrick itaongeza mtaji.