Kamuzu Banda: Rais Mbabe Aliyewanyoa Nywele Wazungu kwa Lazima
Dunia imewahi kuwa na watu wababe mno! Unamkumbuka Hastings Kamuzu Banda? Namzungumzia yule aliyekuwa Waziri Mkuu na Rais wa Kwanza wa Malawi, aliyeitawala nchi hiyo tangu 1964 mpaka 1994, akidumu madarakani kwa takribani miaka 30.
Sasa unaambiwa, kipindi cha utawala wake, kulikuwa na sheria ya namna ya kuvaa kwa wanawake na wanaume pamoja na namna ya kunyoa nywele.
Kulikuwa na mwongozo wa serikali ambao kila mwananchi alipaswa kuufuata kuhusu mavazi. Wanawake hawakuruhusiwa kuvaa nguo zinazoangaza, nguo fupi, nguo zenye mipasuo, nguo zinazobana wala suruali.
Wanaume hawakutakiwa kufuga nywele ndefu, kufuga rasta wala kusuka! Sasa hapa ndipo utata ulipokuwa ukiibuka mara kwa mara.
Wananchi wa Malawi walikuwa wameshalielewa somo na walikuwa wakitii sheria bila shuruti lakini kwa wale wageni, hususan Wazungu, kulikuwa na shughuli kwelikweli.
Kulikuwa na maafisa wa polisi kwenye viwanja vyote vya ndege, kama unavyojua Wazungu wengi nywele zao ni ndefu, basi ikawa mgeni akiingia tu, wale maafisa wanakagua nywele zake na ikibainika ni ndefu, anawekwa pembeni kwanza.
Baada ya kuwekwa pembeni, mhusika alikuwa anatakiwa kuchagua moja kati ya mambo mawili! Kunyolewa nywele kwa lazima mpaka ziwe fupi kama sheria inavyotaka, au kurudi walikotoka mara moja!
Basi jamaa hawakuwa na ujanja, wakawa wanakubali kunyolewa huku wakinung’unika chini kwa chini!