
Serikali imesisitiza kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu, laini zote za simu ambazo hazitakuwa zimejasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole zitafungwa.
Kutokana na msimamo huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amebakiza siku kadhaa kuanzia sasa kutekeleza uamuzi huo wa serikali.
Kamwelwe amesema hakuna tatizo linalowafanya watu washindwe kusajili na kwamba watakaoshindwa kufanya hivyo watakuwa wamekaidi hivyo watakosa mawasiliano.
Kamwelwe ametoa msimamo huo wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) linalotarajia kujengwa mkoani Arusha kwa gharama za Sh. bilioni 33.5. Utiaji saini huo ulifanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na PAPU.
Amesisitiza kuwa suala hilo si la masihara na badala yake watazifungia laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa kwa alama za vidole.
“Yaani hapa nasubiri siku ifike tu ili nizime laini na nitakata laini zote ambazo hazijasajiliwa. Lengo letu ni kupunguza uhalifu kwa njia ya simu. Unakuta mtu mmoja anamiliki zaidi ya laini 20, zote za nini?” Amehoji.
“Hakuna cha sintofahamu hapa, Desemba 31 tunakamilisha usajili na tutafunga laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa. Niwaambie umuhimu wa jambo hili, tumefanya hivi kwa sababu Watanzania wengi wanaibiwa fedha zao kutokana na utitiri wa laini,” amesisitiza.

