KANISA la TFE KWA NEEMA lililopo Kiloleli wilayani Ilemela jijini Mwanza (almaarufu kama Kwa Askofu Mpemba) limeteketea kwa moto majira ya saa 6:00 usiku wa kuamkia leo, ambapo moto ulidumu kwa takribani saa nne.
Akizungumza kwenye eneo la tukio, Sajenti Daudi Mboyelwa ambaye ndiye alikuwa mkuu wa kikosi kutoka Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Mwanza, amesema taarifa za awali zimebaini chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika eneo la vyombo vya muziki ambavyo baadhi vilikuwa havijazimwa, hivyo vilichemka na kusababisha moto.
Mboyelwa ameongeza kuwa walifika eneo la tukio dakika chache baada ya kupewa taarifa toka kwa wadau wa kanisa hilo lakini moto ulikuwa tayari umeshika maeneo mengine na kusambaa.
Jeshi hilo lilishindwa kuanza zoezi la uzimaji moto kwa wakati wakisubiri shirika la umeme nchini (TANESCO) wafike hapo ili kukata nyaya za nguzo za umeme zinazoingia eneo hilo kuepusha majanga na madhara zaidi.
Ni baadhi tu ya viti vya plastiki ambavyo vilikuwa karibu na lango kuu la kanisa hilo, ambavyo walinzi walifanikiwa kuviokoa, lakini samani nyingine zote zimeteketea kwa moto ndani ya kanisa hilo kubwa lililojengwa kwa mabati, mbao na nondo.
Comments are closed.