The House of Favourite Newspapers

KAPTENI HILDA: MWANAMKE WA KWANZA KUENDESHA NDEGE NCHINI

Hilda Wendy Ringo

KUNA kazi ambazo wanawake kamwe hawawezi kuzifikiria kuzifanya maana baadhi ya wengi wao watakuambia nataka kufungua duka la vipodozi, mwingine atakwambia saluni na hata maduka ya nguo lakini kamwe huwezi kusikia kwa wingi kuwa mwanamke anataka kazi ya kuendesha ndege yaani ‘Rubani’ lakini hilo limewezekana kwa Kapteni Hilda Wendy Ringo mwenye umri wa miaka 35 sasa.  

 

Hilda amekuwa mwanamke wa kwanza kati ya wanawake wa Kitanzania waliopeperusha bendera yetu vizuri nje ya nchi baada ya kurusha ndege aina ya Boeng na Air Bus na kuweza kutengeneza historia ya aina yake na kujijengea heshima ya kutosha kabisa.

 

ELIMU YAKE

Hilda alipata elimu yake ya sekondari katika Shule ya Tambaza ya jijini Dar es Salaam na baadaye Chuo Cha Urubani cha Progress Flight Academy cha jijini Pretoria, Afrika  Kusini. Ni mwanamke wa kujivunia katika nchi yetu kwa sababu amekuwa akirusha ndege yaani rubani. Amewahi kuhojiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini na kuhusu kazi yake hiyo anasema; “Kurusha ndege ni jambo zuri linalofurahisha.”

 

MAISHA YAKE NA UZOEFU WA KAZI HIYO

Rubani Hilda alianza kurusha ndege akiwa na umri wa miaka 22 lakini sasa anarusha ndege hapahapa nchini katika Kampuni ya Precision Air. Ana uzoefu mkubwa na kazi hiyo ya urubani kwa sababu ameifanya kwa zaidi ya miaka 10 sasa na ni mwanamke wa kwanza Mtanzania kurusha ndege aina ya Boeing na Airbus.

WAZO LA KUWA RUBANI ALILIPATAJE?

Anasema wazo la kuwa rubani lilimuingia katika akili yake akiwa bado mdogo baada ya kujiuliza maswali mengi kama vile ndege ambayo ni chuma na mabati inawezaje kupaa angani? Anasema swali hilo  lilimjia wakati anasafiri mara kwa mara na wazazi wake akitokea Kilimanjaro kuja Dar es Salaam akitumia Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) lilipokuwa linatamba katika anga ya Tanzania enzi hizo.

 

ANAWAAMBIA NINI WANAWAKE WENZAKE?

“Tanzania ina hazina kubwa ya wanawake si tu kupitia kwenye elimu nzuri, mtu anayoweza kuitumia kuwa ana kipaji kama yeye na kwenda sehemu mbalimbali yeye binafsi au kwa kupitia taalum yake.” Ushauri wake kwa watu wote hasa wasichana anasema kuwa wafanye kazi zao sawasawa na taaluma yao itawalipa vyema.

 

Hilda anawataka wanawake kuacha tabia ya kukaa bila kufanya kazi kwa kutoa visingizio vingi sana, badala yake anasema kuwa wanatakiwa  kufanya kazi kwa bidii ili wasibaki nyuma kwani anaamini kuwa wanawake wengi ndio wanaoweza kusimama kila sehemu na wakafanya maajabu makubwa.

AIPONGEZA SERIKALI YA JPM

“Kwanza ningependa sana kupongeza serikali yetu kuwa na ndege maana lilikuwa ni tatizo nchini kwetu lakini sasa tumeweza kulifufua upya Shirika la Air Tanzania, maana nilikuwa nafadhaika sana tukilinganisha na nchi jirani ya Rwanda ambayo imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi lakini sasa wametuzidi katika kuendesha shirika la ndege na sasa wanalo lao, Air Rwanda ambalo ndege zake husafiri hadi Dubai na kuunganisha hadi Uingereza,” anasema Kapteni Hilda.

 

VIPI KUHUSU FAMILIA

Hilda ameolewa, ana mtoto mmoja wa kiume aitwaye Aichi na anaishi nchini Nigeria kwa sasa.

Makala: Imelda Mtema

Comments are closed.