The House of Favourite Newspapers

Karatasi za Kupigia Kura Zanzibar Zawasili

0
Karatasi za kupigia kura kwa ajili ya marudio ya uchaguzi wa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Machi 20, ziliwasili jana mchana visiwani hapa.

Karatasi hizo zilipokewa na watendaji mbalimbali wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wakiongozwa na mkurugenzi wake, Salim Kassim katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Mkurugenzi huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa jumla ya karatasi 5,385 ndizo zilizowasili.
Kassim alisema karatasi hizo zimechapishwa katika kiwanda cha Unprint cha Durban, Afrika Kusini na ziliwasili hapo kwa ndege yenye Na EW-364TG ya nchi hiyo. Alisema karatasi hizo pamoja na vifaa vingine vitasambazwa vituoni Machi 18, mwaka huu.
Kassim alisema katika karatasi hizo za kupigia, yapo pia majina ya wagombea wote tisa wa vyama vya upinzani waliokwishatangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.
Miongoni mwa wagombea hao ni Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, ambaye ametangaza kujitoa.
Uchaguzi huo wa marudio, pia unaelezwa kugomewa na waangalizi wa kimataifa na hata wale wa ndani.
Mbali na CUF vyama ambavyo pia vimeeleza kutoshiriki uchaguzi huo ni Chaumma, Chama cha Kijaamii (CCK), APPTMaendeleo, ACT-Wazalendo, Jahazi Asilia, Demokrasia Makini, NRA na SAU.
Kassim alipotakiwa kueleza sababu za ZEC kuchapisha karatasi za kura zenye wagombea waliotangaza kususia uchaguzi huo wa marudio, alijibu kuwa yeye si msemaji.
Akizungumzia gharama za uchaguzi huo wa marudio, mhasibu wa ZEC, Yussuf Ali Hassan alisema utagharimu Sh4.5 bilioni tofauti na ule wa Oktoba 25, mwaka jana uliofutwa ambao uligharimu kiasi ya Sh5.3 bilioni.
Picha za ujio wa Makatarsi na huyo anayeonekana hapo ni Mkurugenzi wa ZEC Salim Kassim Ali akitoa maelezo ya kuwasili kwake uwanja wa ndege Zanzibar.
Leave A Reply