The House of Favourite Newspapers

Kariakoo Dabi… Mataifa 13 Kuvuja Jasho kwa Mkapa

0

WAHENGA wanasema “dalili ya mvua ni mawingu” na ndivyo itakavyokuwa Septemba 25, mwaka huu ambapo kipyenga rasmi cha Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 kitapulizwa kwa kuchezwa mechi ya Ngao ya Jamii ambayo ni kiashiria cha kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

 

Mechi hii huwakutanisha bingwa wa ligi na yule wa FA kwa msimu uliopita, kwa msimu huu itawakutanisha Simba ambao ni mabingwa wa ligi na Yanga ambao walishika nafasi ya pili kwenye fainali ya ASFC baada ya kupoteza mbele ya Simba kwa bao 1-0.

 

Mchezo huo wa fainali ya michuano ya ASFC ulipigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, huku mchezo huo wa Ngao ya Jamii ukitarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Mechi hii inasuburiwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini ili kuona wachezaji wapya wa timu hizo, lakini nje ya hapo mechi hii ina vitu vingi ambavyo unatakiwa kufahamu kama makala haya yanavyokuchambulia.

 

VITA YA MATAIFA 13

Usichokijua ni kuwa mechi hii inakutanisha wachezaji kutoka mataifa 13 tofauti ya Afrika. Mataifa ambayo yatashiriki mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ni Tanzania, Mali, Ivory Coast, Burkina Faso, Uganda, Burundi, DR Congo, Malawi, Ghana, Rwanda, Zambia, Senegal na Kenya.

 

Mchezaji anayetoka Ivory Coast ni Pascal Wawa, Burundi ni Saido Ntibazonkiza, Rwanda ni Meddie Kagere, Senegal akiwa ni Pape Ousmane Sakho, Zambia ni Rally Bwalya, na Burkina Faso ni Yacouba Songne.

 

Wengine ni Djigui Diarra na Sadio Kanouté kutoka Mali, Malawi wanataka Duncan Nyoni na Peter Banda, Uganda ni Khalid Aucho na Thaddeo Lwanga huku Kenya akiwepo Joash Onyango.

 

Mastaa kutoka DR Congo ni Chriss Mugalu na Henock Baka, Jesus Moloko, Heritier Makambo, Yannick Bangala, Shaban Djuma na Fiston Mayele. Waliobaki ni Watanzania.

 

MORRISON NA MUKOKO OUT

Kiungo mshambuliaji wa Simba Bernard Morrison raia wa Ghana na kiungo mkabaji wa Yanga Mukoko Tonombe raia wa DR Congo watakosekana kwenye mchezo huu kutokana na kutumikia adhabu zao.

 

Kwa upande wa Mukoko anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye mchezo wa fainali ya ASFC dhidi ya Simba huku Morrison akitumikia adhabu ya kifungo cha mechi tatu baada ya kufanya vitendo vilivyoashiria utovu wa nidhamu kwenye mchezo huo.

 

MATOKEO YA PRE SEASON

MECHI ZA KIRAFIKI ZA SIMBA

Simba 0-1 TP Mazembe

Simba 1-1 Olympic Club de Khourigba

Simba 2-2 AS Far Rabat

Simba 0-0 Coastal Union

Simba 2-1 Fountain Gate FC

MECHI ZA KIRAFIKI ZA YANGA

Yanga 1-2 Zanaco

Yanga 3-1 Friend Rangers

Yanga 1-0 Pan African

Yanga 3-1 DTB FC

 

BENCHI LA UFUNDI

Kocha Mkuu wa Simba ni Didier Gomes (Ufaransa), makocha wasaidizi; Seleman Matola (Tanzania) na Thierry Hitimana (Rwanda), Kocha wa makipa ni Milton Mendv (Brazil).

Kocha wa utimamu wa mwili ni, Adel Zrane (Tunisia), Meneja wa timu: Patrick Rweyemamu, Mchua Misuli: Jallow Bakari, daktari wa timu ni Yassin Gembe na mtunza vifaa ni Hamis Mtambo wote wa Tanzania na Fareed Cassiem wa Afrika Kusini.

Kwa upande wa Yanga benchi lao litaongozwa na Kocha Mkuu: Nassredine Nabi (Tunisia), kocha wa makipa ni Razack Siwa (Kenya) na kocha wa utimamu wa mwili Helmi Gueldich (Tunisia) na daktari ni Shecky Mngazija (Tanzania).

LEEN ESSAU, Dar es Salaam

 

 

Leave A Reply