The House of Favourite Newspapers

Kariakoo Dabi Piga Haooo!

0

PIGA haooo! Unaweza kusema hivyo kufuatia miamba ya soka hapa nchini ikionekana kutunishiana misuli kuelekea mchezo wa leo Jumamosi katika Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Simba na Yanga zinakutana kwa mara ya pili msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara kuelekea kwenye mbio za kusaka ushindi utakaowafanya kujiimarisha vizuri kwenye msimamo, ikumbukwe mchezo wao wa kwanza uliopigwa Novemba 7, mwaka jana ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Michael Sarpong alifunga kwa upande wa Yanga na Joash Onyango akaisawazishia Simba jioni kabisa.

 

Timu hizi kila moja inakutana na mwenzake ikiwa na makocha wapya, Simba ambao ni wenyeji wananolewa na Mfaransa, Didier Gomes wakati Yanga wao wana Mtunisia, Nasreddine Nabi, hawa wote wameinoa timu ya Al Merreikh ya Sudan msimu huu.

 

Tangu awasili ndani ya Simba, Didier Gomes ameonyesha kuwa muumini wa mfumo wa kucheza wa 4-3-3, 4-2-3-1 na muda mwingine ni 4-4-2 kutegemea na aina ya mpinzani ambaye anakutana naye.

 

Katika mifumo yote hiyo tegemeo lake zaidi ni viungo wake Luis Miquissone na Clatous Chama, ambao wamekuwa msaada mkubwa kwenye suala la kufunga lakini kutoa nafasi za mabao. Kwa jumla wao wamechangia mabao 36.

 

Nabi ana Yacouba Songne aliyehusika kwenye mabao 10.

Nabi ambaye ndiye anajenga utawala wake ndani ya Yanga, kwenye mechi mbili ambazo ameiongoza timu hiyo ile ya Azam FC na Tanzania Prisons ametumia zaidi mfumo wa 4-4-2 japo pia anauhusudu ule wa 4-1-4-1 na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ndiye amekuwa mhimili wake.

 

Simba ya Gomes ikiwa kwenye Uwanja wa Mkapa, hapo itaonyesha uwezo wa juu wa kupiga pasi na mbwembwe nyingi huku Nabi, yeye akiendelea kuingiza kile kilichopo akilini mwake kwa nyota wake japo inaonyesha anapenda kutumia mpira wa kushambulia zaidi kutoka pembeni.

 

Nikukumbushe kuwa, Nabi kwa upande wake ana hasira sana na mpinzani wake kwa sababu ndiye ambaye alichangia kufukuzwa kwenye kibarua chake kilichopita wakati akiwa anaifundisha Al Merrikh ya Sudan.

 

Nabi alisitishiwa kibarua chake kwenye timu yake muda mfupi tu baada ya kutoka suluhu na Simba ambayo benchini iliongozwa na Gomes. Hivyo, hii nafasi kwa Nabi kulipa kile alichofanyiwa nyuma.

 

Sasa mchezo wa leo unaonekana kama Simba wanapewa jeuri kubwa ya kushinda kutokana na uimara wa kikosi chao ambacho kimetinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Yanga ambao hawapewi nafasi wanaonekana kuwa na kiburi cha kutaka kuonyesha kuwa wanaweza kushinda dhidi Simba hata kama wanaonekana kama wepesi.

 

Wakizungumzia mechi ya leo, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola na yule wa Yanga, Nabi kila mmoja amemtambia mwenzake kupata ushindi kutokana na maandalizi ambayo wameyafanya.

 

Matola alisema: “Mchezo wa watani huwa na mabadiliko ya kiuchezaji mara nyingi lakini kwa upande wetu safari hii lazima tutabadilika ili tupate ushindi mzuri kwetu.

“Tutacheza soka la tofauti na miaka yote ambayo tumekuwa tukicheza na Yanga, tutacheza soka la kuvutia ambalo litatupa ushindi.”

 

Kwa upande wake, Kocha wa Yanga, Nabi alisema kuwa anaiheshimu Simba kutokana na wanachokifanya lakini kwa upande wao wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao wamefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

 

“Ni mchezo unaoibeba Tanzania kwenye suala la michezo, Simba naiheshimu kutokana na wanachokifanya ila kwa upande wetu tayari tumefanya maandalizi mazuri ili kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo,” alisema Nabi.

MARCO MZUMBE NA MUSA MATEJA

Leave A Reply