Karibu Music Festival kuunguruma Bagamoyo mwezi ujao
Ofisa Mauzo wa Kampuni ya K.I.CO na mratibu wa tamasha hilo, Ernest Biseko (katikati) akiongea na waandishi wa habari.
Kutoka kushoto ni, Msanii wa Raggae atakayetumbuiza siku hiyo, Jhikolabwino Manyika, mratibu wa tamasha hilo, Ernest Biseko, Meneja Uvumbuzi wa Serengeti Breweries Ltd, Attu Mynal (wapili kulia).
Wanahabari wakiwa makini katika mkutano huo.
TAMASHA La Kimataifa la muziki lijulikanalo kama Karibu Music Festival, linatarajiwa kuunguruma kuanzia Novemba 7 mpaka 9, mwaka huu katika Viwanja vya Mwanakalenga, Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es Salaam, mratibu wa tamasha hilo, Ernest Biseko, amesema kuwa tamasha hilo linaratibiwa na Karibu Cultural Promotions Organization (KCPO) pamoja na Legendary Music Entertainment and Promotions Co.Ltd.
Biseko amesema tamasha hilo linatarajiwa kuwa la aina yake likiwashirikisha watoto na watu wazima huku ikiwa ni mara ya pili kufanyika hapa nchini na litakuwa na kauli mbiu isemayo “Fahari ya Tanzania”.
Aliongeza kuwa, tamasha hilo lina lengo la kukuza muziki wa Kiafrika na kuonesha tamaduni za Kiafrika kwa dunia nzima kupitia jukwaa la muziki litakalokutanisha wanamuziki kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Aidha, Biseko amesema wadau mbalimbali wa muziki kutoka dunia kote watakutana na kubadilishana uzoefu wa kikazi na kufungua milango kwa wasanii wachanga, kukuza mtandao wa marafiki na kujifunza vitu vipya kutoka kwa wasanii wa nje ya nchi.
Biseko amewataja baadhi ya wasanii watakaoshiriki katika tamasha hilo kutoka nje ya Tanzania ni, Papa Wemba, Sarabi Band, H-Art The Band,Yuzzo and Frontline Band.
Kutoka Tanzania ni, Jhiko Manyika (Jhikoman) akiwa na band yake ya Afrikabisa, Tomgwa Ensembe, Misoji Nkwambi (Mshindi wa BSS 2008), Ze Spirit, Isha Mashauzi, Damian Soul na band yake, Juma Nature, Msafiri Zawose na band yake.
Vilevile amesema kuwa kiingilio cha tamasha hilo kitakuwa, Tsh. 2500/= watoto 5000/= watu wazima, ukinunua tiketi getini 7000/= pamoja na upande wa VIP Tsh 30,000/=
(NA DENIS MTIMA/GPL)