The House of Favourite Newspapers

Kaseja kuwabania Simba leo Mwanza

Juma Kaseja

WACHEZAJI wa zamani wa Simba kipa, Juma Kaseja na mshambuliaji, Elias Maguli leo wataiongoza KMC kuwavaa Wekundu hao Jijini Mwanza.

Simba itaingia uwanjani katika mchezo huo wakitoka kupata ushindi wa mabao 2-0 walioupata walipocheza juzi Jumanne na Alliance kwenye uwanja huo.

Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems alisema siyo mchezo mwepesi kwao kutokana na ubora wa wapinzani wao katika mechi za hivikaribuni, hivyo ataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

Aussems alisema kikosi chake kitakuwa na mabadiliko ya baadhi ya wachezaji ambao aliwapumzisha kwa makusudi katika mchezo uliopita wa ligi na Alliance kutokana na uchovu.

 

“Nimejaribu kutengeneza mzunguko wa wachezaji kucheza kwa zamu ili wapate muda wa kupumzika kutokana na mfululizo wa mechi tunazoendelea kuzicheza za ligi.

 

 

“Hivyo, ni lazima kikosi changu cha kesho kitakuwa na mabadiliko kidogo ya wachezaji ambao hawakucheza mchezo uliopita na Alliance.

 

“Kuhusu maandalizi ya timu yanaendelea vizuri, kikosi changu kinakabiliwa na majeruhi walewale Kapombe na Nyoni ambao wote wameanza mazoezi mepesi,”alisema Aussems ambaye wachambuzi kitakwimu wanampa nafasi kubwa ya kubeba Kombe.

 

Kocha Mkuu wa KMC, Etiene Ndayiragije alisema ; “Simba ni moja ya timu kubwa hapa nchini iliyokuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na uwezo mkubwa, lakini hiyo haitatufanya tuwahofie tutaingia uwanjani kwa ajili ya kupata ushindi.”

Comments are closed.